Wenje aunguruma Mwanza; akana kupokea ‘ongezeko’ la posho

Jamii Africa

Mbunge wa Nyamagana Jijini Mwanza, Ezekiel Dibogo Wenje (CHADEMA), akifafanua jambo kwa waandishi wa habari juu ya nyongeza ya posho za wabunge kutoka sh. 70,000 hadi sh. 200,000, muda mfupi baada ya kumaliza mkutano wake wa hadhara uliofanyika uwanja wa Sahara jijini humo jana.

MBUNGE wa Jimbo la Nyamagana Jijini Mwanza, Ezekiel Dibogo Wenje (CHADEMA), ametoboa siri ya namna Serikali inavyotaka kulitumia Bunge la Katiba mpya, ambapo amesema mpango uliopo ni kuhakikisha Wajumbe wengi wa Bunge hilo kutoka CCM wanaipitisha Katiba mpya kwa mtindo wao wa ndiyoo, kama ambavyo wamekuwa wakitumia siku zote Bungeni.

Kufuatia hali hiyo, Wenje ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema taifa, ameonya kwamba hali hiyo huenda ikaleta machafuko nchini, na kwamba ili kuepusha hali hiyo lazima Rais Jakaya Kikwete ateuwe idadi sawa ya wajumbe kutoka vyama vyote vya siasa vyenye wabunge na visivyo na wabunge Bungeni, madhehebu ya dini, taasisi na makundi yoye ta kijamii.

Wenje ameyasema hayo jana jioni Jijini Mwanza, wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara aliouandaa kwa ajili ya kukabidhi madawati 500 kwa shule za jimbo hilo, uliofanyika katika uwanja wa Sahara katikati ya jiji hilo, na kuhudhuriwa na maelfu ya watu, na kuwaonya Machinga kuondoka mara moja katika maeneo ya barabara za Nyerere, Pamba na Kenyeta, kama walivyokubaliana.

Alisema, suala la uundwaji wa Katiba mpya ni nyeti sana na linagusa maisha ya Watanzania, hivyo Serikali lazima iwe makini zaidi katika kutekeleza azma na matakwa ya wananchi wake, na kwamba kati ya wajumbe wote 565 wa Bunge la Katiba, wengi wao watatoka CCM wakiwemo wa CUF ambapo alisema upo uwezekano mkubwa Katiba hiyo kupitishwa kwa ushabiki.

“Rais asiwe kiraja katika suala hili la Katiba mpya, aache kabisa. Chadema tunataka asijaze wajumbe wengi kutoka CCM…na iwapo wajumbe wengi watatoka CCM na CUF, basi katiba itapitishwa kwa ndiyooo!.

“Kwa hali hiyo, inaweza ikachochea hasira za wananchi. Na sisi wabunge wa Chadema tunakwenda Bungeni kupigania haya pamoja na sheria ya kuzuia watu wasiujadili muswada wa Katiba ifutwe. Wakikataa tutaitisha maandamano ya kutorudi majumbani hadi kieleweke”, alisema Wenje.

Katika mkutano huo ambapo mbunge huyo alitangaza mikakati kabambe ya kupunguza kama si kumaliza kero za wananchi wa Nyamagana, alisema: “Sheria ya sasa juu ya Katiba mpya iliyosainiwa na Rais ni hatari kuliko hata sheria za wakoloni. Na kama sheria hii haitafanyiwa marekebisho, tutaitisha maandamano na safari hii hatutarudi nyuma kamwe”.

Akizungumzia ongezeko la posho za Wabunge kutoka sh. 70,000 hadi sh. 200,000 kwa kila mbunge katika kikao cha siku moja, mbunge huyo wa Nyamagana ambaye katika Uchaguzi Mkuu uliopita alimwangusha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, alimtuhumu Spika wa Bunge, Anne Makinda juu ya kauli yake kuhusu ongezeko hilo.

Alisema, anachojua wabunge hawapewa nyongeza hiyo ya posho, na kwamba kauli ya Spika wa Bunge, ililenga kuupotosha umma na ilitolewa kisiasa zaidi, na kwamba kauli ya Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah ipo sahihi na haina upotoshaji wowote.

“Mfano mimi hapa Wenje sijaiona kwenye akaunti yangu hiyo nyongeza ya 200,000 aliyoisema Spika. Kashililah ndiyo yupo sahihi maana posho hazijaongezwa. Na kama kuna wabunge walishapewa hizo posho labda wa CCM”, alisema Wenje alipotakiwa kutoa ufafanuzi zaidi na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa mkutano wake huo majira ya saa 12:40 jioni.

Kuhusu mikakati ya kimaendeleo jimboni humo, mbunge huyo anayejiita mtoto wa ‘Mama Ntilie’, alisema licha ya kutumia zaidi ya sh. milioni 30 kutengeneza madawati 500, Halmashauri ya Jiji la Mwanza ipo kwenye mchakamchaka wa kutengeneza madawati 800 yatakayogharimu sh. milioni 44, na kati ya hayo Jimbo la Nyamagana litapewa madawati 400 na Ilemela madawati 400.

Mbali na hayo, alisema zaidi ya sh. milioni 300 zilizopunguzwa kwenye posho za watumishi wa halmashauri ya jiji, zimepangwa kuelekezwa katika ununuzi wa madawati hivi karibuni, na kwamba michango holela shuleni ni marufuku, ikiwa ni pamoja na uchangiaji wa madawati iwe sh. 30,000 badala ya sh. 60,000 zilizokuwa zikitozwa hapo awali.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza.

3 Comments
  • WENJE KAZA BUTI ISIWE NGUVU YA SODA WASAIDIENI WANA NZEGA WAAMKE KUTOKA GIZANI WAMETEKWA NA CCM

  • CCM BILA UFUSKA,UZANDIKI,UFISADI NA KILA AINA YA UOZO INAWEZEKA? KAMA INAWEZEKANA BASI SIO CCM NINAYOIFAHAMU MIMI NA WATANZANIA KWA UJUMLA

  • wenje songa mbele kaka vijana tunawasoma nyie ili 2015 tupate nguvu tugombee ubunge tulete changes but kwa nini ccm wakitoa hizo nyongeza ya posho msipokee halafu mkaanzisha mfuko maalumu katika majimbo yenu ya kuwasaidia jamii kama kusomesha yatima na wakinamama wanaojifungua kwa kukosa pamba na wembe

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *