WASWAHILI wanayo misemo mingi inayotawala maongezi kuhusu safari. Wapo wanaosema ‘msafiri kafiri’ wakimaanisha ni kawaida kwa mtu anayesafiri kukutana na madhila awapo safarini. Wengine husema ‘safiri uone’ wakimaanisha unaposafiri, yapo mengi unayoweza kuona tofauti na usiposafiri.
Hapo humaaisha kwamba unaposafiri kuna mengi utayaona.
Hiyo ni baadhi tu ya misemo inayotumika kusadifu safari ya mtu. Kwa miezi miwili ya Oktoba na Novemba, mwaka jana (2012), nilisafiri na kuishi katika wilaya nne tofauti zilizoko kwenye mikoa mitatu tofauti.
Niliishi katika wilaya ya Ikungi – Singida, Londoni-Manyoni, Mpwapwa-Dodoma na Kilosa- Morogoro.
Kwenye mzunguko huo, nilikutana na changamoto mbalimbali za maisha kwenye kila wilaya ambapo nilijifunza na kujua mambo kadhaa kuhusu maisha ya wakazi wa maeneo niliyoishi.
Mfereji uliotengenezwa kwa ajili ya usafirishaji maji kwa wakulima wa mto Lumuma, wilayani Mpwapwa
Safari yangu ilianzia kijiji cha Londoni, katika wilaya ya Manyoni, mkoani Singida. Kijiji hicho kipo takriban kilometa 100 kutoka Singida mjini au kilometa 800 hivi unapotoka Dar es Salaam.
Katika kijiji hicho, niliishi kwenye eneo la wachimbaji madini wadogo, lakani kazi yangu niliifanyia kijiji jirani cha Sambaru ambacho kiko katika wilaya mpya ya Ikungi.
Maisha yangu ya kila siku katika kijiji cha Londoni yalikuwa ya kulala, lakini kikazi niliamkia wilaya tofauti.
Umbali wa kutoka Londoni hadi Sambaru ni kilometa tano, lakini ili ufike katika migodi ya wachimbaji madini wadogo (ambayo hivi sasa imefungwa) inalazimu utumie takriban dakika 10, huku ukipanda mlima mkali.
Kwa ujumla, Londoni ni kijiji kidogo kilichojikusanya pamoja ambacho ni makazi ya wachimbaji madini wadogo, madalali na wanunuzi wa dhahabu. Pia ni mahali pekee ambapo unaweza kupata baadhi ya bidhaa za dukani kama vile sukari, maji ya kunywa ya chupa, nguo na unga.
Vilevile sehemu hiyo ndiyo yenye vibanda vya vinywaji moto ambapo unaweza kupata bia za aina mbalimbali kwa bei ya kuruka.
Mathalan, bia za aina zote huuzwa kwa sh. 3,000 badala ya sh. 2,000 ilhali maji ya chupa yanayouzwa sehemu nyingi sh. 400-1000, kwa Londoni yanauzwa sh. 700 hadi sh. 1,700.
Tofauti na Sambaru, katika kijiji hicho kuna huduma za vyakula. Sahani moja ya wali kwa sasa inauzwa sh. 2,500 na kwa nyakati fulani huuzwa zaidi ya hapo pale ‘wahemeaji’ wa madini wanapoongezeka. Pia hicho ndicho kijiji pekee katika sehemu hiyo ambapo unaweza kupata malazi.
Vijiji jirani na Londoni vya Sambaru, Mang’onyi, Mwau na Mahambe havina ‘gesti’. Sehemu hiyo kuna vibanda viwili vilivyogeuzwa kuwa nyumba za wageni, kila kimoja kikiwa na ‘vyumba’ saba. Mtu anayetaka chumba hulazimika kulipa sh. 5,000 kwa siku.
Pamoja na huduma hizo ambazo hazipatikani Sambaru, starehe za muziki na bendi zinazoambatana na wacheza shoo hupatikana mara moja-moja.
Kwa ujumla kati ya vijiji hivyo viwili (Sambaru na Londoni), hapa ndipo mahali panapokimbiliwa na wengi, hususan watu wanaojihusisha na shughuli za madini ya dhahabu.
Wenyeji wanasema zamani katika kijiji hicho dhahabu zilipatikana kwa wingi na pia starehe za aina mbalimba hazikukosekana, ndiyo maana kikaitwa Londoni.
Kwa upande wake, Sambaru ni kijiji ‘kilichosambaa’ nyumba zikiwa zimejengwa mbali mbali. Sifa pekee ya kijiji hicho ni kuwa na ukwasi wa madini ya dhahabu, kikiwa kimezungukwa na migodi na shughuli mbalimbali za madini.
Ukifika katika kijiji hicho ambacho ‘hakifanani’ na ukwasi huo kutokana na umasikini uliokithiri, utakutana na nyumba nyingi za majani zilizojengwa kwa udongo.
Hata hivyo usishangae sana kusikia ngurumo za mitambo ya kusaga mawe, kuosha mchanga na wachimbaji wadogo na wakubwa wanaopishana kusaka mali.
Sambaru ndipo penye kampuni za uchimbaji madini zinazotafiti na kuchimba, pamoja na kuosha dhahabu. Miongoni mwa kampuni hizo ni Mpondi Mining, Shanta Mining na Lake Victoria Mining.
Vijana wakiangalia kwa kutumia zana duni kama mchanga waliochimba unaweza kuwa na madini ya dhahabu katika kijiji cha Sambaru, wilayani Ikungi, mkoa wa Singida
Pia wapo wajasiriamali wengi wadogo wanaomiliki leseni za uchimbaji dhahabu walizozipata kutoka Wizara ya Nishati and Madini.
Ukiondoa kampuni za Shanta Mining na Lake Victoria Mining, ile ya Mpondi Mining inajihusisha na uoshaji mchanga na imekuwa ikinunua vifusi vya mchanga vya zamani ambavyo waliokuwa wamiliki walikuwa wakiviosha mara kwa mara ili kutoa dhahabu.
Pamoja na utiriri wa shughuli za madini, Sambaru inabaki kuwa sehemu ya kutafutia pesa, lakini matumizi ya fedha hizo yanafanyika sehemu nyingine, na kwa sehemu za huko, basi watu huenda kutumia kipato chao Londoni.
Mwanamke akiokota mabaki ya mawe madogomadogo katika kijiji cha Sambaru kwa ajili ya kwenda kuyasaga ili kusaka madini ya dhahabu
MPWAPWA NA KILOSA
Kama ilivyokuwa katika wilaya za Ikungi na Manyoni, safari yangu iliyofuatia ilinifikisha kwenye wilaya za Mpwapwa mkoani Dodoma na Kilosa, Morogoro na hiyo ilikuwa mwezi Novemba, mwaka jana (2012) ambapo niliishi wiki tatu katika kijiji cha Lumuma-Kilosa, ila kazi nilifanyia Lufusi-Mpwapwa. Kila siku, asubuhi, niliamka Lumuma na kwenda Lufusi, umbali wa kilometa sita.
Wenyeji wa sehemu hii wanasema zipo Lumuma mbili ambazo zinatenganishwa na mto ambao ndio uliobeba jina hilo, hiyo ikiwa na maana kwamba ukiwa upande wa pili wa mto ni Lumuma ya Mpwapwa na upande mwingine wanaiita Lumuma-Kilosa.
Hivyo ndivyo walivyozowea kutaja maeneo hayo, na kila upande una shule inayoitwa Lumuma.
Kwa wenyeji hao, mto huo ndiyo rasilimali kubwa na pekee wanayojivunia, maana ndipo shughuli zao nyingi za kilimo zinapofanyika.
Kando ya mto huo, wanalima vitunguu, maharage, mahindi na mpunga. Wakati mwingine shughuli hizo hufanyika mwaka mzima, wakibadilisha tu utaratibu wa kuandaa mashamba na upandaji wa mazao.
Kwa ujumla uchumi wa vijiji hivyo viwili pamoja na vingine vya Kitati, Mafwene, Nkhumbulu, Kidete na Msowelo unategemea bonde la mto huo usiokauka.
Kama ilivyo kwa Londoni-Manyoni, kijiji cha Lumuma-Kilosa kina huduma chache ambazo hazipatikani katika kijiji jirani cha Lufusi. Katika kijiji hicho kuna nyumba za kulala wageni tatu, baa moja na maduka kadhaa yanayouza takriban bidhaa zote za dukani.
Maisha katika vijiji vyote vya sehemu hiyo yanategemea zaidi shughuli za kilimo, hasa cha vitunguu, ambapo vijana ndio waliojikita kwenye kazi hiyo.
Wenyeji wanasema kilimo cha vitunguu ndicho mkombozi wao kiuchumi na hukitumia kusomesha watoto na kuendesha maisha ya kila siku. Kilimo cha mazao mengine wanakitegemea kwa chakula pekee.
“Hapa usipolima vitunguu wewe huonekani na huwezi kukaa na sisi mezani (kunywa).” anasema Abdallah Ibrahim, kijana ambaye nilikutana naye baa akinywa bia yake.
Kwa Ibrahim na baadhi ya vijana, kilimo cha vitunguu na biashara ya zao hilo ndicho kinachowapa jeuri ya kuweza kununua bia kwa sh. 2,500 na kutembea mitaani wakiwa wamebeba maji ya chupa kubwa za maji ya kunywa yanayotengenezwa viwandani.
Camera yako iko powerful naona picha zako ziko clear!