Yabainika: Wasichana wenye umri wa miaka 20 – 25 hushambuliwa zaidi na UKIMWI nchini Tanzania

Jamii Africa

MAABUKIZI ya Virusi vya Ukimwi yako juu kwa wasichana wenye umri kati ya miaka 20 na 25 kuliko walio chini ya umri huo, FikraPevu inaandika.

Inaelezwa kwamba, maambukizi kwa wasichana wa rika hilo la miaka 23-24 yamefikia kiwango cha asilimia 6.6 ambayo ni kubwa kulinganisha na rika jingine.

Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto za mwaka 2011-2012, zinaonyesha kwamba, maambukizi kwa wasichana wa rika la kati ya miaka 15-19 yako chini zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa wasichana wa umri wa miaka 15-17 ni asilimia 1.1 tu, huku wenye umri wa miaka 18-19 huathirika kwa asilimia 1.5.

Kiwango hicho kinazidi kuongezeka na kufikia asilimia 3 kwa wasichana wenye umri wa miaka 20-22.

Dakta Regina Mkoma wa Hospitali ya Rufaa ya Temeke jijini Dar es Salaam ambaye anajihusisha na na masuala ya Ukimwi, amesema sababu kubwa inayowafanya watoto wa kike kuathirika zaidi na Virusi vya Ukimwi wakiwa katika umri wa miaka 20- 25 ni uhuru wa kupitiliza.

Dk. Mkoma anasema uhuru huo humfanya msichana afanye atakacho wakati anapokuwa katika umri huo wa kupevuka, hivyo kujihusisha zaidi na vitendo vya ngono bila kuchukua tahadhari.

“Ikumbukwe kuwa umri huu ni ule ambao vijana wengi huwa katika elimu ya juu hivyo uhuru huongezeka kwa kutokuwa karibu na wazazi au walezi, hivyo kujiamulia mambo wayatakayo kutokana na mazingira waliyopo,” anasema Dk. Mkoma.

FikraPevu imebaini pia kwamba, wasichana wa umri huo wanapokuwa vyuo, wengi wao huwa na wapenzi zaidi ya mmoja kwa sababu ya tamaa na kipato ili kukidhi mahitaji yao, jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wa afya zao.

Dk. Mkoma ameongezea kuwa vijana wa umri wa miaka 20-25 hujihusisha zaidi na masuala ya ngono kuliko walio kati ya umri wa miaka 15-19, hali ambayo husababisha urahisi wa kuambukizwa Virusi vya Ukimwi.

Aidha, amesema tamaa za mahitaji mbalimbali, vishawishi, pamoja na makundi yasiyofaa pia huchangia wasichana hao kujiingiza uhusiano wa ngono na kuwa katika hatari ya kuambukizwa Ukimwi.

“Kitaalam umri huu wa miaka 20-25 kwa wasichana ndio ambao hali ya kijinsia na ukuaji huwa kisababishi kikubwa kwani wanakuwa wanahemka kimahaba (sexual active) kuliko miaka 15- 19, wakikutana na marafiki wasiofaa, wakiwa na uhuru wa kupitiliza, wakipata vishawishi, inakuwa rahisi kujiingiza katika masuala ya ngono, tena zisizo salama, na hatimaye kupata Virusi vya Ukimwi,” ameongeza.

Aidha, Dk. Mkoma ameshauri kwamba, ili kupunguza maambukizi hayo kwa vijana ni vyema kutoa elimu inayojitosheleza kuhusiana na Ukimwi kwa rika hilo.

Katika suala la kibailojia, Dk. Mkoma ameshauri wasichana wapewe elimu zaidi juu ya ngono salama na tahadhari yao binafsi.

Wakati Sera ya Afya ya mwaka 2007 kuhusiana na Ukimwi nchini Tanzania inasisitiza kuiweka huru nchi na magonjwa kama Ukimwi, lakini hali inaonekana kuwa tete kwa wanajamii wengi huku mipango ya serikali ikishindwa kutekelezwa ipasavyo kwa kinachoelezwa kuwa ufinyu wa bajeti.

Sera hiyo inafafamua: “Serikali inapambana na janga la Ukimwi na magonjwa mengine ya kuambukiza na yasiyoambukiza, kwa kuanzisha na kutekeleza mikakati maalum ya kuelimisha jamii ili kupunguza maambukizi mapya, kujikinga na kuchukua hatua ya matibabu sahihi mapema.”

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Masuala ya Watoto (UNICEF) linaonyesha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi sita zinazoongoza kwa idadi kubwa ya vijana wanaoathirika na Ukimwi duniani ikifuatiwa na Kenya, Nigeria, Afrika Kusini, Msumbiji na India kwa mwaka 2015.

Ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Uganda imejitahidi kutatua tatizo hilo kwa kuanzisha program mbalimbali za kuelimisha vijana walio kati ya umri wa miaka 15-25 huku pia ikitoa mbinu nyingi za kujikinga na Ukimwi.

Kauli mbiu ya Shirika la Kupambana na Ukimwi la Umoja wa Mataifa (UNAIDS) kuhusu mkakati wa kupambana na Ukimwi inasisitiza sufuri tatu (“three zeros”) ikimaanisha, ambapo sufuri ya kwanza ni kutokuwepo na muathirika mpya wa Virusi vya Ukimwi, sufuri ya pili kutokuwepo na unyanyapaa kwa waathirika wa Ukimwi na sufuri ya mwisho ni kutokuwepo na vifo vinavyohusiana na Ukimwi.

Hali hiyo inazilazimu serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kutafuta mbinu mbadala ili kuyafikia malengo hayo.

Afya Bora na Ustawi ni lengo namba tatu la Malengo ya Maendeleo Endelevu Duniani (SDG) ambapo azma yake ni kupambana na magonjwa mbalimbali ukiwemo Ukimwi, hususan kwa vijana walio katika umri wa miaka 15-24.

Kutokana na changamoto mbalimbali, hali inaonekana kuwa ngumu kwa Tanzania kulifikia lengo hilo kwa kupunguza idadi ya maambukizi pamoja na kuwapatia waathirika dawa za kupunguza makali ya Ukimwi.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani kuhusu Ukimwi za mwaka 2015 zinasema kuwa inakadiriwa zaidi ya watu milioni 36.7 wanaishi na Virusi vya Ukimwi duniani, huku Bara la Afrika likiongoza kwa idadi kubwa ya waathirika ambayo ni 25.5 milioni.

Wagonjwa wengi kati ya hao wako Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi za ukanda huo.

Hata hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS) linasema nusu ya kundi linaloathirika na Ukimwi duniani ni vijana, hususan walio kati ya umri wa miaka 15-24.

Nayo Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) inasema kuwa kwa kuzingatia Sera ya Taifa ya Afya na ya dunia Tanzania inaweza kuondoa maambukizi mapya ya Ukimwi.

Kauli mbiu ya WHO wakati wa Siku ya Ukimwi Dunia kwa mwaka 2016 ambayo hufanyika kila Desemba Mosi ilisema kuwa mpaka kufikia mwaka 2030 kusiwepo na Ukimwi duniani.

Ili kufikia malengo hayo, serikali inatakiwa kuweka jitihada zaidi ili kuondoa tatizo hilo kwa kuongeza bajeti kwenye Wizara ya Afya, hasa mipango ya maendeleo ya kukabiliana na Ukimwi na magonjwa nyemelezi ili kuokoa maisha ya vijana wengi, ambao ndio nguvu kazi ya Taifa lolote duniani.

3 Comments
  • nimeupenda uandishi huu wa stori kwasababu umejaa viambatanisho  vinavyoonyesha ubora wa stori

  • Elimu ya Afya bado haijawekewa mkakati,ikumbukwe umri huu vijana wanakuwa huru kutokana na wazazi kuwaona wameshakuwa watu wazima. Lakini pia umri huu ni wa vijana kuwa katika elimu ya juu.

    Naishauri serikali pamoja na mashirika binafsi kuanza kutoa elimu ya afya vyuoni kama sehemu ya kuwakumbusha vijana ambao tunaamini wanajua.

    Na hii ni kwasababu vijana wengi wanapoanza mahusiano wanakuwa makini sana na matumizi ya kinga ila baada ya mda hujisahau na kwenda peku.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *