Yanga kuitoa Zamalek, kwa maandalizi gani?

Jamii Africa

KAMA historia ina chochote cha kujirudia, basi kinaweza kujitokeza katika mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu kati ya wawakilishi wa Tanzania, Yanga, na mabingwa wa Misri, Zamalek.

Timu hizo zitapambana Februari 18, 2012 katika mchezo wa kwanza utakaofanyika jijini Dar es Salaam, ambao kwa mtazamo wa wataalamu wa soka, ni mchezo wa upande mmoja.

Kwa Yanga, historia imejaa majonzi kwani rekodi zote zinaonyesha kwamba haijawahi kuifunga timu yoyote kutoka Misri tangu mwaka 1982 ilipoanza kupambana na timu za huko kwenye michuano yoyote ya Afrika.

Kati ya mechi 10 ambazo Yanga imepambana na timu za Misri, haijawahi kushinda hata moja – iwe nyumbani au ugenini – zaidi ya kuambulia sare nne na vipigo sita vya aibu.

Aibu yenyewe ni kubwa zaidi kwa sababu katika mechi hizo, uwezo wa Yanga kufunga umeonekana mdogo mbele ya Waarabu hao wa Afrika Kaskazini kwani imewahi kufunga mabao matatu tu huku ikishindiliwa mabao 22 kwenye mechi hizo 10.

Siyo nia ya mwandishi kuikatisha tamaa Yanga, hasa kwa kuzingatia uzalendo, lakini makala haya yanataka kutathmini mtihani uliopo kwa wawakilishi nao na hali halisi ilivyo.

Daima Yanga imeonakana kuwa mnyonge kwa timu za Misri hata inapocheza nyumbani, na mara mbili imepata kufungwa nyumbani.

Kwa bahati nzuri au mbaya, timu hiyo ya Jangwani imepambana na timu tatu tu za Misri katika historia yake – ikiwa imecheza na Al Ahly mara sita na kufungwa mechi tatu, huku ikilazimisha sare mara tatu nyumbani. Lakini kwa jumla ya mechi zote hizo sita (nne zikiwa katika Klabu Bingwa na mbili za Kombe la Shirikisho), imefungwa mabao 14-1!

Imewahi kucheza na Ismaily kwenye Klabu Bingwa Afrika mwaka 1992, lakini ikafungwa nyumbani 2-0 na kulazimisha sare ya 1-1 mjini Ismailia.

Kwa sasa inapambana na Zamalek kwa mara nyingine ikiwa inakumbuka jinsi kigogo hicho cha Misri kilivyoifunga jumla ya mabao 4-0 kule Cairo baada ya kuwa imelazimisha sare ya 1-1 mjini Dar es Salaam katika Kombe la Washindi Afrika mwaka 2000.

Rekodi ya Yanga katika michezo ya kimataifa hairidhishi wala kufurahisha, inakera na inakinaisha kuizungumzia. Ni mara tatu tu katika historia yake imewahi kufanya vizuri – mwaka 1969 ilipotolewa na Asante Kotoko kwa shilingi, na mwaka 1970 ilipofungwa 2-0 na Kotoko kwenye Uwanja Huru mjini Addis Ababa baada ya kutoka sare mechi zote mbili. Mara zote mbili timu hiyo ilitolewa kwenye robo fainali.

Mara ya tatu ilikuwa mwaka 1998 wakati kikosi kilichoundwa na akina Edibily Lunyamila kilipofanikiwa kufuzu katika hatua ya makundi (robo fainali) ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ukiacha kiwewe cha kuvurunda kwenye mechi za kimataifa, Yanga kwa ujumla haina ubavu mbele ya timu kutoka Afrika ya Kaskazini. Haina kabisa na siyo suala la ushabiki wala kukosa uzalendo.

Iwe kwenye michuano ya Afrika ama ile ya Afrika Mashariki na Kati, timu hiyo daima huwa haitambi mbele ya timu kutoka Sudan, Misri, Tunisia, Libya au Morocco ambazo imewahi kukumbana nazo.

Kati ya mechi 26 ilizocheza na timu kutoka ukanda huo, Yanga imeshinda mechi moja tu, ikilazimisha sare 12 na kufungwa 13! Unawezaje kusema hii ni rekodi ya kujivunia ama kujifariji kuwa timu hiyo inao ubavu wa kuiondoa mashindanoni Zamalek?

Ubavu wa kufunga mabao wenyewe ni mdgo, kwa sababu katika mechi zote hizo imefunga mabao 15 tu huku ikibugizwa mabao 48. Kama safu ya ushambuliaji ni butu, au ukuta wake ni legevu, hilo wanalijua makocha wanaoinoa timu hiyo.

Katika kipindi hiki ambacho inasubiri kuikabili Zamalek jijini Dar es Salaam, timu hiyo inasikitisha, kwa sababu haijafanya maandalizi ya maana chini ya kocha Mrsebia Kostadin Papic.

Tangu kuanza kwa mwaka huu, Yanga imecheza mechi tano tu, ambazo yenyewe inazihesabu kama ndizo za maandalizi dhidi ya Zamalek.

Kikosi cha Yanga!

Huwezi kujiamini kusema kwamba umekomaa na uko tayari kuikabili timu kama Zamalek, ambayo imewekeza zaidi ya bilioni ………. kwa usajili na Ligi ya Mabingwa, ukitegemea mechi za Bonanza la Mapinduzi Cup, ambako pia hujafanya vizuri.

Katika mechi tatu ilizocheza kwenye Kombe la Mapinduzi mjini Zanzibar, Yanga ilifungwa mechi mbili na kushinda moja tu. Ilianza kufungwa bao 1-0 na Miembeni kabla ya kuifunga Kikwajuni 2-0, lakini ikakutana na kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Azam FC na kutolewa mashindanoni.

Katika mechi za kirafiki, Yanga ilifanikiwa kuifunga Sofapaka ya Kenya kwa mabao 2-1 jijini Dar es Saalam, lakini katika mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Moro United, Yanga ilinusurika kipigo dakika za mwisho iliposawazisha na kufanya matokeo kuwa 2-2.

Mvurugano uliopo, kwamba kocha Papic anasema hapati ushirikiano, huku viongozi wakiendeleza ‘football fitina’, kwa maana ya siasa katika soka la Tanzania, hakuna mategemeo ya Yanga kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa. Hakuna. Huu ndio ukweli wenyewe na hauhitaji miujiza kuuthibitisha. Pengine, tusubiri tuone.

Mechi za Yanga na timu za Misri:

P        W       D       L        GF     GA

10      0        4        6        3        22

 

Yanga na timu za Afrika Kaskazini:

P        W       D       L        GF     GA

26      1        12      13      15      48

2 Comments
  • Hakika yaliyosemwa kuhusu YANGA ni ya kweli kabisa ingawaje sisi wapenzi wa mpira wa miguu tunasema mpira unadunda, Lakini kwa hili nadhani utadundia gorini kwa YANGA. YANGA VIONGOZI si dhani kama kweli mna nia ya kuendeleza soka la timu yetu bali naonaa kama mnatengeneza mazingira ya ninyi wenyewe kujiinua kiuchumi. Nasema hivyo kwa sababu mbili kuu.
    1.Mimi kama shabiki mkereketwa na mpenzi wa YANGA sikuona kabisa makosa ya Kocha SAM TIMBE ambaye mara baada ya kujiunga na YANGA aliipatia KOMBE LA TUSKER, na ubingwa wa Tanzania, lakini akaambuliwa kutimuliwa na kashfa nyingi
    2.Huyu mserbia naye hampatii ushirikiano wa kutosha kiasi kwamba yuko “frustrated” je hapo unatarajia nini?
    Hebu Viongozi YANGA jirekebisheni kwani mliingia kwa GIA KUBWA sasa mwashangaa nini

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *