Zifahamu  sababu za kisayansi, kiuchumi za ndege kupakwa rangi nyeupe

Jamii Africa

Kama umewahi kupanda au kuiona ndege, utakuwa umegundua kuwa ndege nyingi zina rangi nyeupe. Hata kama zimepakwa rangi nyingine lakini nyeupe haiwezi kukosa. Lakini umewahi kujuuliza kwanini ndege nyingi zina rangi nyeupe? Makala hii itakufungua macho na kukuonyesha sababu lukuki na faida za kupaka rangi nyeupe kwenye chombo cha usafiri wa angani.

Sababu za kisayansi

Rangi nyeupe inaakisi mwanga wa jua na kuongeza mng’ao zaidi lakini  rangi za aina nyingine zinafyonza mwanga sio rahisi kuonyesha mng’ao.

Kama utaipaka ndege yako aina  nyingine ya rangi na sio nyeupe, itafyonza mwanga na kuongeza joto ndani ya ndege, jambo ambalo unapaswa kuliepuka. Rangi nyeupe kwa upande mwingine, inaakisi (reflect) mwanga wa jua na kuzuia joto kujiimarisha kwenye ndege.

Hili ni jambo zuri sio tu kama ndege iko angani, hata kama imesimama kwenye njia yake kwasababu itachukua muda mfupi kupoa baada ya kutua kwenye ardhi yenye joto na mazingira yenye jua kali. Baadhi ya ndege zinahitaji kufunikwa kwa rangi nyeupe ili kuendana na muundo wa mashine inayoiwezesha kupaa.

 

Urahisi wa kukagua nyufa na hitilafu

Ndege hukaguliwa mara kwa mara ili kubaini nyufa, mipasuko na aina nyingine za hitilafu kwenye tabaka la ndege (hii hufanyika kwasababu za kiusalama).  Ni rahisi kubaini nyufa kwenye tabaka la ndege kwasababu nyufa huonekana zaidi kwa rangi nyeusi kuliko rangi nyeupe.

Kwa kuongezea ni kuwa rangi nyeupe inasaidia kubaini alama za msuguano na kuvuja kwa mafuta kwasababu viashiria hivyo huacha alama au mchirizi mweusi.  Pia ndege nyeupe ni rahisi kuiona hata kama imeanguka au imepata hitilafu au ajali ndogo hasa nyakati za usiku au kwenye maji mengi.

 

Sababu zisizo za kisayansi

Sio sababu zote zilizotajwa kwenye makala hii ni za kisayansi kuhusu ndege kuwa na rangi nyeupe. Zipo sababu zingine ambazo haziwezi kupuuzwa. Mfano wa sababu hizo ni:

Kupaka rangi ni gharama

Katika taaluma ya usafiri wa anga, kuipaka rangi ndege sio sawa na kupaka rangi ukuta wa nyumba. Inahitaji uwekezaji wa fedha, rasilimali watu na muda. Kuipaka ndege aina ya Boeing Airbus kokote kule hutumia siku mbili hadi saba kutegemea na bajeti yako.

Rangi nyingi inahitajika ndani ya ndege ambako abiria na mizigo inakaa. Kwa muktadha huo, gharama za uendeshaji wa ndege zinaongezeka licha ya kampuni nyingi kukwepa gharama kadiri inavyowezekana lakini ni muhimu rangi ya kutosha ipakwe ndani na nje ya ndege.

 

Thamani ya ndege nyeupe huongezeka kwenye soko

Ikiwa umeipaka ndege yako rangi tofauti na nyeupe kwa madhumuni ya kuuza, tarajia kupata bei ndogo ukilinganisha na ndege yenye rangi nyeupe. Dhumuni la kampuni yoyote ni kupunguza gharama kadiri inavyowezekana. Wakinunua ndege isio na rangi nyeupe, watalazimika kuipaka tena rangi nyeupe ili kupata faida zaidi kwa kuuza bei ya juu baada ya kununua kwa bei ndogo.

 

Rangi nyeupe haififii haraka

Ikiwa ndege itapaa angani, inapita kwenye hali ya hewa tofauti tofauti na kama haina rangi nyeupe, muonekano wake utafifia haraka ambapo wamiliki watalazimika kuipaka rangi mara kwa mara ili kung’alisha muonekano wake. Ndege nyeupe ikiwa angani haionyeshi utofauti hata kama itakaa angani kwa muda mrefu.

Hata hivyo, zipo kampuni ambazo zina ndege zenye rangi mbalimbali, kama unayoiona hapo chini.

Wakati mwingine mtu akikuuliza kwanini karibu ndege zote zina rangi nyeupe? Mwambie sio tu kuna sababu za kisayansi lakini hutumia gharama ndogo. Kama wanavyosema, rangi nyeupe inaenda na kila kitu, ni kweli?

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *