Zitto azitaka taasisi za manunuzi kuchunguza zabuni ya ujenzi wa ndege wa Chato

Jamii Africa

Serikali imeshauriwa kuimarisha mifumo ya utoaji taarifa kwa kuzijengea uwezo taasisi zake na  kuboresha  sheria ili kuongeza uwazi na uwajibikaji wa viongozi katika rasilimali muhimu za taifa.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika Mdahalo wa Demokrasia uliondaliwa na Twaweza, Mbunge wa Kigoma Mjini,  Zitto Kabwe amesema  serikali imepiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa lakini inapaswa kujiendesha kwa uwazi na kuruhusu taasisi zake kuwajibika katika manunuzi na matumizi ya fedha za umma.

“ Moja ya jambo ambalo linaisaidia sana serikali kukabiliana na ufisadi ni uwazi kwasababu inatoa uhuru kwa wananchi kutoa taarifa na kuweza kuzifanyia kazi”, amesema Zitto.

Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo amesema usiri wa serikali unawanyima wananchi haki ya kupata taarifa muhimu za miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo katika maeneo yao.

Ameongeza kuwa mfumo wa uwazi na uwajibikaji unaanzia kwenye taasisi ambazo zimewekwa kisheria kusimamia rasilimali za nchi zikiwemo Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mamlaka wa Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) na Kamati za Bunge kufanya kazi kwa uhuru na kutoa mapendekezo yao juu ya uboreshaji wa changamoto zilizopo katika jamii.

“ Taasisi za uwajibikaji kama Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, kamati muhimu za Bunge za Mahesabu  kama hazina uwezo wa kufanya shughuli zao kwa uwazi na uhuru maana yake kwamba baada ya awamu hii kutoka na kumaliza muda wake tutakuwa na kazi ngumu sana ya kupambana na madhira ya ufisadi kama yanavyoshughulikiwa sasa hivi”, amesema Zitto.

Amesema serikali ya awamu ya nne ilijitahidi kuimarisha taasisi zake za uwazi na uwajibikaji ambazo ziliibua ufisadi mkubwa kama Tegeta Escrow, Richmond, Meremeta ambao uliligharimu taifa mabilioni ya fedha.

Ameitaka serikali kuendeleza utamaduni  huo na kuondoa dhana ya usiri katika uendeshaji wa shughuli zake.

“Wito wangu ni lazima kuendeleza zile  juhudi  za uwazi na ujenzi wa taasisi ambao umeanza ili taasisi ziendelee kuwa huru kwaajili ya kuweza kuibua mambo kama haya”, ameshauri Zitto.

Mbunge wa Kogoma Mjini, Zitto Zuberi Kabwe akifuatilia Mdahalo wa Kongamano la Demokrasia uliondaliwa na Taasisi ya Twaweza, jijini Dar es Salaam jana.

Hata hivyo, Zitto ameitaka  Ofisi ya CAG na PPRA kuchunguza fedha zilizotumika kujenga uwanja wa ndege wa Chato, ambao haujafuata taratibu za kisheria na haukupitishwa na bunge, ili wananchi wapate taarifa za uhakika na kuondoa mjadala ambao haujapatiwa majibu ya uhakika kutoka serikalini

Ikumbukwe kuwa katika kikao cha tisa cha Bunge, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche aliibua sakata la ujenzi wa uwanja huo lakini majibu ya uhakika hayakutolewa. Uwanja huo ambao unadhaniwa kugharimu zaidi za bilioni 39 unajengwa katika mji wa Chato  anakotoka Rais John Magufuli.

“Si vibaya kujenga viwanja vya ndege na Chato ni Tanzania kama sehemu nyingine yoyote ya Tanzania na hatuwezi kutopenda wenzetu kupata maendeleo lakini jambo la muhimu ni namna gani ule mradi unatekelezwa haukuwa kwenye mipango ya bajeti, hapakuwa na zabuni ya wazi”, amesema Zitto na kuongeza kuwa,

“Kampuni ambayo imepewa kufanya ile kazi haijawahi kujenga kiwanja chochote cha ndege, katika mazingira kama haya uwazi ungeweza kusaidia kwa sababu PPRA ambayo ni mamlaka ya manunuzi ya umma ingeweza kufanya uchunguzi na kuweza kutueleza uhalisia wa jambo hili. Kwasababu ni fedha nyingi zinatumika pale, zaidi ya bilioni 39”.

Haki ya Kupata Taarifa

Mkurugenzi wa JamiiForums, Maxence Melo amesema  wananchi wana haki ya kupata taarifa za mwenendo wa shughuli za serikali yao ambayo wameiweka madarakani. Ili kuhakikisha haki hiyo inatekelezwa kikamilifu inapaswa kutengeneza mfumo imara utakaoweka utaratibu mzuri wa kupokea na kutoa taarifa muhimu za serikali.

“Hakuna mfumo mzuri wa kutoa na kupata taarifa serikalini. Viongozi wa serikali wawe wabunifu walete mfumo utakaosaidia kupatikana kwa taarifa zenye manufaa kwa wananchi”, amesema Melo kuwa ili mfumo huo ufanye kazi ni lazima uhuru wa kutoa maoni na kujieleza uheshimiwe.

Naye Deogratius Bwire, kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), amesema mabadiliko ya kisheria na sera ni muhimu katika kuongeza uwazi na uwajibikaji katika jamii ambapo amesema serikali inapaswa kuzifanyia marekebisho baadhi ya sheria kama Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Kupata Habari na Sheria ya Takwimu ambazo zinaminya uhuru wa wananchi kupata taarifa.

Hata hivyo, wananchi wametakiwa kuamka na kuhamasika kutafuta taarifa katika mamlaka husika ili ziwasaidie kufanya maamuzi sahihi katika shughuli za kujiletea maendeleo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Twaweza, Aidan Eyakuze amesema tafiti zao zinaonyesha ni idadi ndogo ya wananchi ambao wanatafuta taarifa lakini wanakutana na vikwazo mbalimbali ambavyo vimewekwa na viongozi. Amewetaka kutumia haki yao ya kupata taarifa kusimama na kudai uwazi na uwajibikaji katika shughuli zote jamii.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *