Udongo ni rasilimali muhimu inayotumiwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo ambacho kinategemewa na watanzania kuendesha uchumi wa taifa. Lakini uharibifu wa mazingira umechangia kushuka kwa thamani ya ardhi na kuathiri kilimo cha mazao, mifugo na uvuvi.
Kutokana na mabadiliko yanayojitokeza kwenye udongo, wananchi wameshauriwa kulima mazao yanayoendana na aina ya udongo uliopo katika eneo husika. Tanzania ni moja lakini udongo hutofautiana kutoka eneo moja hadi lingine ambapo mazao yanayolimwa hutofautiana katika eneo husika ili kuhakikisha uwiano mzuri wa mazao yanayolimwa nchini.
Ripoti ya Takwimu za Mazingira ilitolewa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS-2015) inaeleza kuwa sehemu kubwa ya Tanzania Bara ina udongo wa kitropiki ambao una virutubisho vichache na madini ya nitrogen na phosphorus.
“Japokuwa Tanzania ina aina nyingi za udongo, lakini unaofaa kwa kilimo unapatikana katika maeneo machache kama Arusha, Kilimanjaro, Morogoro na Mbeya”, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ambapo kupungua kwa thamani ya ardhi ya kilimo ni matokeo ya uharibifu wa mazingira.
Kutokana na tofauti hizo za udongo wakulima wanashauriwa kulima mazao yanayoendana na aina ya udongo unaopatikana eneo husika ili kujihakikishia usalama wa chakula.
Aina za Udongo zinazopatikana nchini
- Udongo wa kichanga
Ukanda wa Pwani ambao unajumuisha mikoa ya Dar es salaam na Pwani, sehemu kubwa ya udongo wake ni ya kichanga. Udongo wa kichanga huundwa kutokana na kuvunjika vunjika na kumomonyoka kwa miamba kama vile mawe ya chokaa, matale, mawe meupe ya kung’aa na mwambatope.
Udongo huu hauhifadhi maji ambapo maji kupenya kwa urahisi huzuia matatizo ya kuoza mizizi. Udongo wa kichanga huruhusu maji kupitiliza zaidi ya kiasi kinachohitajika, ambayo husababisha mimea kukosa maji wakati wa kiangazi.
Kutokana na sifa za udongo huo wakulima wanashauriwa kulima mazao yanayohimili ukame kama mihogo, kunde, uwele ambayo huwa mkombozi wakati wa njaa.
- Udongo wa Mchangatope
Mchangatope ni udongo wenye chenga ndogo zaidi kuliko udongo wa mchanga hivyo ni laini unapoushika. Udongo huu ukimwagiwa maji, unateleza kama sabuni. Na unapatikana zaidi katika Nyanda za Juu za Kati mwa nchi.
Huundwa na madini kama vile mawe angavu ambayo yana madini aina ya kwatzi na punje ndogo ndogo za mabaki ya viumbe hai. Ni chengachenga kama udongo wa mchana lakini unahodhi virutubisho vingi zaidi na unyevu. Udongo huu una uwezo mdogo wa kuhifadhi maji.
- Udongo tifutifu
Udongo tifutifu hutengenezwa na uwiano mzuri wa mchanga, mchangatope, mfi nyanzi na mabaki ya viumbe hai. Huchukuliwa kama udongo unaofaa zaidi katika ardhi inayolimika. Udongo tifutifu una rangi nyeusi na unafanana na kushika unga mikononi.
Umbile lake ni mchanga mchanga na huhodhi maji kirahisi sana, hata hivyo upenyezaji wake wa maji ni mzuri. Kuna aina nyingi za udongo tifutifu kuanzia wenye rutuba hadi ulio na tope zito na tabaka nene la juu. Hata hivyo kati ya aina zote hizi tofauti za udongo, udongo tifutifu ndio unaofaa zaidi kwa kilimo.
Kwa Tanzania udongo huu hupatikama zaidi Nyanda za Juu Kusini na Kaskini mwa nchi hasa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma.
- Udongo mfinyanzi
Udongo mfinyanzi huundwa na chembe chembe ndogo sana ambazo zina sehemu ndogo sana ya kupitisha hewa. Udongo mfi nyanzi huundwa baada ya miaka mingi ya miamba kumomonyoka na athari za hali ya hali ya hewa.
Mara nyingi vidimbwi hutokea kwenye udongo mfi nyanzi na udongo hugandamizwa kwa urahisi. Kutokana na uwezo wake mdogo wa kupenyeza maji, hatari ya maji kutuama na ardhi kuwa ngumu, sio rahisi kufanya kazi na udongo mfi nyanzi. Udongo huu hupatikana zaidi Ukanda wa Kaskazini Magharibi na Nyanda za Magharibi Kigoma na maeneo ya mkoa wa Mwanza. Aina za udongo zilizotajwa hapo ni miongoni mwa aina nyingi za udongo zinazopatikana nchini.
Hata hivyo, mazao yanayolimwa katika maeneo mbalimbali ya nchi ni mahindi, mhogo, maharage, mpunga na ndizi. Mahindi ni zao la chakula katika maeneo mengi lakini mhogo na viazi vitamu vinatumiwa zaidi katika maeneo yenye ukame.
Mzao ya biashara hujumuisha Kahawa, tumbaku na pamba, chai, mkonge na korosho ambayo husafirishwa nje ya nchi. Kutokana na aina za udongo katika maeneo tofauti, wakulima wanashauriwa kulima kilimo kinachoendana na mabadiliko ya ardhi ili kujihakikishia usalama wa chakula.