Iringa: Wakulima wa nyanya waanza kuzalisha mvinyo kukabiliana soko

Jamii Africa

WAKULIMA wa nyanya katika Kijiji cha Tanangozi wilayani Iringa, wameanza kuliongezea thamani zao hilo kwa kuzalisha mvinyo (wine) kama hatua ya kukabiliana na changamoto kubwa ya masoko inayowakosesha tija.

Akizungumza na FikraPevu, Peter Nzalawahe, ambaye ni Katibu wa Mradi wa Usindikizaji bidhaa zitokanazo na zao la nyanya, alisema mbali ya kusindika mvinyo, lakini pia wanatengeneza bidhaa nyingine kama Tomato Sauce, Chill Sauce, Tomato Paste na Jam.

Alifafanua kwamba, usindikaji una tija kubwa kwani tenga moja la nyanya mbivu linalouzwa kwa kati ya Shs. 10,000 hadi 20,000 ama wakati mwingine kushuka bei hadi Shs. 5,000 mahali pengine, linaweza kutoa chupa 120 hadi 144 za mvinyo zikisindikwa.

“Chupa moja ya mvinyo inauzwa Shs. 10,000, kwa hiyo kwa tenga moja unaweza kupata Shs. 1.2 milioni, na unaweza kuona namna ambavyo wakulima wanaweza kutengeneza faida na kujikwamua na umaskini ikiwa watasindika bidhaa zao,” alisema.

Nzalawahe alisema kwamba, hata wakulima wenzao wa Imalutwa katika Mji wa Ilula nao wameanza kutengeneza mvinyo.

Changamoto za vibali

“Soko letu la nyanya linaweza kuwa kubwa na kilimo kitatuletea tija ikiwa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda chetu kidogo zitapatiwa nembo na taasisi za viwango nchini,” Nzalawahe aliiambiaFikraPevu.

Alisema kwamba, kinachowakwamisha kuendelea na uzalishaji ni vibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na Mkemia Mkuu wa Serikali

“Kwa sasa tumesimama kidogo kwa sababu ya kukosa vibali, tumekwishapeleka maombi na tunasubiri taratibu, naamini tukipata tunaweza kuboresha kiwanda chetu kidogo na kikaleta tija kubwa,” alisema.

Akaongeza: “Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa alituita na kutuambia kwamba tunatakiwa kusitisha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa zetu zote mpaka hapo tutakapopata leseni za TBS na TFDA, taasisi ambazo kisheria ndizo zinazothibitisha ubora wa bidhaa na kama zinafaa kwa matumizi ya binadamu.

“Tumechangishana wenyewe na kununua kiwanja ambacho tunarajia kujenga kiwanda chetu. Tumeshapeleka sampuli za bidhaa zetu kwa taasisi hizo muhimu wakazichunguze, na kama zinafaa, ili tuweze kuruhusiwa tuendelee na uzalishaji. Tunaomba sana wadau watuunge mkono, kwani taaluma tuliyopata ni kupitia serikali yenyewe ambayo inalenga kutukwamua na umaskini.”

Mwenyekiti wa zamani wa Kijiji cha Tanangozi, Norbert Kikoti, ambaye ni Mwenyekiti wa Mradi huo, aliiambia FikraPevu kwamba, ikiwa taasisi hizo za serikali zitaweza kuharakisha uchunguzi wa bidhaa zao na kutoa mapendekezo ama kuruhusu ziendelee kuzalishwa, wanaamini watakuwa na uwezo wa kuzalisha kwa wingi bidhaa hizo na hivyo mkulima kunufaika zaidi.

“Tukiruhusiwa kuzalisha, mradi huu utatoa fursa ya ajira zaidi ya 200, mbali ya wanamradi ambao na wao wanaendelea kujishughulisha,” anasema Kikoti.

Kikoti aliongeza kwamba, kupatikana kwa hati za taasisi hizo kutatoa hamasa ya wananchi wengi kushiriki kilimo cha nyanya kwani uwepo wa kiwanda utawahakikishia soko la kudumu la mazao yao.

“Tunaomba pia wadau watusaidie mitambo mizuri zaidi ya kuzalisha biadhaa hizi kwa sababu tunaamini tuna uwezo mkubwa wa kujishughulisha kwa tija na kujiletea maendeleo wenyewe badala ya kusubiri ama kuilaumu serikali,” aliiambia FikraPevu.

Katika mahojiano na FikraPevu, Nzalawahe alisema, waliamua kuanzisha mradi huo baada ya kuona zao la nyanya linakosa soko la uhakika ambapo mara nyingi wakulima wanapata hasara kuliko faida.

“Wakati mwingine hata gharama hairudi, fikiria kuna wakati tenga tunauza hadi Shs. 3,000, ambazo haziwezi kutupatia tija yoyote, wengine wameamua kuachana na kilimo hiki ingawa kina faida kubwa,” alisema.

Aidha, alisema kwamba, wao wameendelea na uzalishaji baada ya kujiunga kwenye kikundi katika Mradi wa Umwagiliaji wa Matone kijijini hapo, ambapo baadaye walipatiwa mafunzo na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) kuhusu namna ya kusindika bidhaa katika hatua ya kuongeza thamani.

Kikundi chao chenye watu 25 kinajihusisha na usindikaji wa bidhaa mbalimbali zitokanazo na nyanya, ambazo zinapatikana kwa wingi karibu mwaka mzima kijijini hapo ambako kuna mradi maalum wa kilimo cha umwagiliaji wa matone unaowafanya wakulima wazalishe mwaka mzima.

Usindikaji wa bidhaa hizo, anasema Nzalawahe, unaleta tija kubwa kwa mkulima kuliko hata kuuza matenga ya nyanya mbivu katika soko ambalo limekuwa likipanda na kushuka kwa kasi.

Mwanzo wa mradi

Nzalawahe akionyesha chupa tupu ambazo zinasubiri kujazwa mvinyo.

FikraPevu inafahamu kwamba zao la nyanya linakabiliwa na changamoto kubwa ya masoko hali ambayo inawafanya wakulima kuendelea kuogelea kwenye wimbi la umaskini kutokana na kutopata faida licha ya kutumia gharama kubwa katika kilimo cha zao hilo.

Uhaba wa viwanda vya usindikaji mazao ya matunda ni chanzo cha kupotea kwa karibu asilimia 70 ya nyanya zinazozalishwa mkoani Iringa kutokana na kuharibika kabla ya kufika sokoni.

FikraPevu inafahamu kuwa, Iringa ina viwanda vitatu tu vya kusindika nyanya ambavyo pia uwezo wake ni mdogo ukilinganisha na kiasi cha nyanya kinachozalishwa.

Uchunguzi unaonyesha kwamba, karibu tani 107,190 za nyanya zinavunwa Iringa (ikiwa ni asilimia 70 ya nyanya zinazozalishwa nchini Tanzania), lakini ni asilimia tano tu ndizo zinasindikwa kwa sasa na zinazosalia zinasafirishwa zikiwa ghafi kwenye masoko ya ndani ya mkoa na nje ya nchi.

Karibu wakulima 35,000 mkoani humo wanalima hekta 6,109 za nyanya, zao ambalo ndilo kuu la biashara lakini linakabiliwa na changamoto ya kukosa masoko.

Nzalawahe alisema, wazo la kubuni mradi huo wa kusindika bidhaa za nyanya walilibuni baada ya kupewa mafunzo ya ujasiriamali na SIDO pamoja na wadau wengine wa ujasiriajamii mwaka 2012.

“Awali tulipewa mafunzo ya kilimo bora cha nyanya chenye tija kupitia Mradi wa MUVI (Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini), tukazalisha kwa wingi nyanya kuliko mahitaji. Soko likakosekana kutokana na uzalishaji kuwa mkubwa, hivyo tulipopata mafunzo ya kuanzisha miradi mingine, tukaona usindikaji ndio mradi utakaotufaa kwa sababu malighafi ipo kwa wingi hapa kijijini,” alieleza katika mahojiano maalum kijijini hapo.

Alisema, SIDO ndiyo iliyowapatia mtaji wa kwanza kwa kusimamia uzalishaji wa mvinyo wa kwanza mwezi Aprili 2012 na kuwafundisha kwa vitendo namna ya usindikaji wa bidhaa nyingine, ambapo waliweza pia kuzipeleka bidhaa zao katika Maonyesho ya Wakulima ya Nyanda za Juu Kusini (Nane Nane 2012) mjini Mbeya pamoja na kushiriki Maonyesho ya Viwanda Vidogo (SIDO).

“Tulifanya vizuri sana kwenye Nane Nane mjini Mbeya mwaka 2012 na hata Wine yetu ilipata nafasi ya kwanza kwa ubora, lakini tukashindwa kupewa tuzo kwa kuwa tu haijathibitishwa na TBS na TFDA. Hata katika maonyesho ya SIDO tulifanya vizuri pia, kikwazo ni hicho cha kutotambuliwa,” alisema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *