Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuboresha maslahi ya wanahabari na kujenga taasisi imara zinazoendeshwa kwa weledi na taaluma ili kuongeza uhuru wa kujieleza na kupata taarifa.
Akizungumza katika Mdahalo wa pili wa Demokrasia Yetu uliondaliwa na Asasi ya Kiraia ya Twaweza, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Tanzania Media Foundation (TMF), Ernest Sungura amesema ili jitihada za kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari zifanikiwe nchini, wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kuboresha utendaji wa vyombo vyao kwa kubuni vyanzo vingine vya mapato na kuongeza weledi kwa waandishi na wahariri.
“Muundo wa uendeshaji wa vyombo vya habari lazima ubadilike ili kuwepo na uhuru wa uhariri. Lazima vyanzo vya mapato na teknolojia zibadilike ili kuendana na wakati”, amesema Sungura.
Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya habari wanabainisha kwamba vyombo vya habari vinabanwa, vinatishwa na baadhi ya wanahabari wanatiwa nguvuni kutokana na kazi wanayofanya.
Hali hiyo imetajwa kuwa ni mkakati wa watawala kuminya uhuru wa kujieleza na kupata taarifa ambapo magazeti ya Tanzania Daima, Raia Mwema, Mawio na MwanaHalisi yamefungiwa kwa tuhuma za uchochezi
Kulingana na Utafiti wa Twaweza (2016) unaeleza kuwa “Uhuru wa kujieleza umekuwa ukikabiliwa na vitisho vikali ambapo polisi wamekamata watu 358 kwa mwaka 2015 na watu 911 2016 kwa kosa la kutumia lugha mbaya”.
Sungura amesema vyombo vya habari vikiwa na mifumo imara ya mapato na kuwalinda waandishi wa habari dhidi ya rushwa vitachochea uhuru wa kujieleza na kuondoa dhana ya kukandamizwa.
Pia amewataka waandishi wa habari ambao wanakabiliwa na vikwazo vya kufanya kazi nchini kutumia njia mbadala ili kufikisha ujumbe kwa jamii.
“Wanahabari wa kukosa Uhuru wa kutoa habari watumie njia ya mtandao au watumie vyombo vya habari vya kimataifa; huu ndio ujasiri tunaoutaka katika sekta ya habari nchini”, amesema Sungura na kuongeza kuwa serikali inapaswa kuweka tafsiri sahihi juu ya sheria inazotumia kusimamia tasnia ya habari nchini ili wanahabari wafanye kazi zao kwa uhuru.
Ili kuhakikisha inasimamia maudhui na ukuaji wa tasnia ya habari nchini, sheria mbalimbali zimepitishwa ikiwemo; Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Huduma za Habari (2016) na Sheria ya Takwimu (2015). Lakini changamoto inajitokeza ni jinsi zinavyotekelezwa na wale waliowekwa kuzisimamia.
Kwa upande wake Wakili Jebra Kambole amesema sheria zilizopo ni nzuri kwasababu zinatoa haki ya kjieleza na kupata taarifa.
“Katiba imetoa uhuru wa kujieleza na pia imetoa uhuru zaidi wa kutafuta na kupata taarifa”, amesema Kambole na kuongeza kuwa, “Sio kila Sheria zinazotungwa na Bunge ni nzuri kuna sheria nyingi ni ‘unjust’. Wadau wa habari ni jukumu letu zile sheria mbovu tupambane nazo kwa njia zinazoruhusiwa kisheria ili tuweze kupata haki tunazozihitaji”
Ameeleza kuwa hali ya ubanaji wa uhuru wa kujieleza ikiendelea nchini, athari zake ni kukosa fursa za uwekezaji, sera, sheria na huduma nzuri za kijamii.
Naye Mwandishi wa Habari wa Kujitegemea, Pacal Mayalla amewataka wanahabari nchini kuendelea kutimiza majukumu yao kwa weledi na kutoa habari za kweli zinazolenga kutetea maslahi ya taifa.
“Kanuni ya kwanza ya Mwandishi mzuri wa habari ni kuandika ukweli na ukweli mtupu hata kama utakugharimu kiasi gani”, amesema Mayala na kuongeza kuwa ili ukweli usimame wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kuboresha mazingira ya kazi ya wanahabari ili kuwahakikishia usalama na weledi.
Mchangiaji mwingine katika Mdahalo huo, Vicent Kasali amesema ili mapambano ya wanahabari kudai uhuru yafanikiwe hawana budi kuungana na kuwa na sauti moja dhidi ya vitendo vyote vya dhuluma wanavyotendewa.