Serikali kwa kushirikiana na taasisi binafsi katika Wilaya ya Tunduru inaendelea na uchimbaji wa visima virefu vya maji katika vijiji 23 ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Wilaya hiyo.
Mhandisi wa Maji Wilaya ya Tunduru, Emanuel Mfyoyi kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya wilaya hiyo, anaeleza kuwa wakazi wengi wanategemea maji ya visima kutokana na maji ya bomba yanayozalishwa, kusambazwa na Mamlaka ya Maji Mjini Tunduru (TUWASA)kutokidhi mahitaji yote ya wakazi.
Anaeleza kuwa kwa kushirikiana na shirika la All Mother and Children Count (AMCC) chini ya Kanisa Anglikana Dayosisi ya Tunduru-Masasi wanatekeleza mradi wa uchimbaji wa visima virefu katika vijiji 23 vilivyomo katika wilaya hiyo ili kupunguza hadha ya wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji.
Mradi huo ambao umepewa jina la Children Health Improvement Program (CHIP) una lenga zaidi kuwafikia wanawake na watoto ambao mahitaji ya maji ni makubwa kuliko makundi mengine katika jamii.
Licha ya Tunduru kuwa karibu na Ziwa Nyasa ambalo hutumika kwa matumizi mbalimbali ya kibinadamu, lakini Wilaya hiyo haifaidiki na chanzo hicho ambacho hakijawekewa mikakati endelevu kuzalisha maji ya bomba ambayo yangemaliza kabisa tatizo la maji katika Mkoa wa Ruvuma.
Kulingana na Ripoti ya Shirika la Watoto Duniani (UNICEF) ya mwaka 2017 juu Upatikanaji wa Maji safi inaeleza kuwa kati ya mwaka 2000 na 2015, idadi ya watu duniani waliokuwa wanatumia maji ya bomba imeongezeka kutoka bilioni 3.5 hadi bilioni 4.7. Watu wasiotumia maji ya bomba waliongezeka kutoka bilioni 1.7 hadi bilioni 2.1 duniani kote. Na watu 2 kati ya 5 maeneo ya vijijini na 4 kati ya 5 wanatumia maji ya bomba.
Hata hivyo, Wilaya ya Tunduru ina kazi kubwa ya kuinua hali ya upatikanaji wa maji ikizingatiwa kuwa visima ndio tegemeo kubwa la wakazi huku maji ya bomba yakipatikana katika maeneo machache.
Tanki la kuhifadhia maji lilipo kata ya Namasakata Wilaya ya Tunduru
Upatikanaji wa Maji
Wilaya ya Tunduru ina wakazi wapatao 298,279 lakini maji ya bomba yanayozalishwa na Mamlaka ya Maji Mjini Tunduru (TUWASA) yanawafikia wakazi 175,250 tu ambao ni asilimia 58.8. Asilimia iliyobaki hawapati maji ya uhakika kutokana na uwekezaji mdogo usioendana na ongezeko la idadi ya watu.
Mahitaji ya halisi ya maji kwa mtu mmoja mmoja ni lita 60 kwa siku, ambayo hayapatikani yote na huwalazimu baadhi ya wakazi kutembea umbali wa nusu kilometa kuyafuata maji katika vijiji vya jirani vyenye vyanzo vya maji.
Vyanzo vikuu vya maji ni chemichemi zilizo katika milima ya Wilaya hiyo na zinapatikana katika maeneo ya Mlingoti, Mkwanda, Namalowe, Nalwale, Lituguru, Njenga na Nande. Chanzo kingine cha maji ni visima virefu na vifupi vinavyomilikiwa na Halmashauri na taasisi binafsi kama shule na makanisa.
Ili kukabiliana na uhaba wa maji Wilaya hiyo inaendelea na miradi ya uendeshaji wa visima vinavyochimbwa chini ya ardhi ili kuhakikisha huduma ya maji inawafikiwa wakazi wengi zaidi ili kukuza uchumi wa wilaya hiyo.
Halmashauri inamiliki jumla ya visima 849 lakini vinavyofanya kazi ni 574 na visivyofanya kazi ni 275 idadi hiyo ni karibu robo ya visima vyote ambavyo viko hai. Visima vinavyomilikiwa na watu binafsi ni 1,037 na vyote vinafanya kazi. Sababu kubwa ya visima hivyo kutofanya kazi ni uchakavu na uharibu wa mazingira ambao unazuia matumizi endelevu.
Kata za Nakapanya, Ngapa na Mindu zinatajwa kuwa na shida kubwa ya maji ambapo mikakati mbalimbali ya kuzifikia zinaendelea ikizingatiwa kuwa kata hizo zinakabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara ambayo inazifanya zisifikiwe kwa urahisi.
Mafundi wakiendelea na uchimbaji wa kisima cha maji
Mafanikio yaliyopatikana
Sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia imekamilisha miradi 4 ya usambazaji wa maji ya bomba katika kata za Nandembo, Nalasi, Lukumbule na Mbesa ambapo wananchi wanapata maji ya uhakika.
Halmashauri katika mwaka wa fedha 2016/2017 imefanya ukarabati wa visima katika shule za sekondari za Ligunga, Masonya, Mtutula, Nakapanya, Marunba na Mchoteka. Pia inaendelea na uchimbaji wa kisima kirefu katika vijiji cha Msinjili, Mbungulaji na Rahaleo.
Kulingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s) ambayo yanalenga hadi kufikia 2030 kuongeza matumizi ya maji ya uhakika katika sekta zote na usambazaji wa maji safi kutatua tatizo la upatikanaji wa maji ili kupunguza idadi ya watu ambao wanataabika kutokana na uhaba wa maji.
Hata hivyo, kufikia malengo hayo nchi wahisani zimetakiwa kuongeza uwekezaji katika miradi ya maji na utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuhakikisha watu wanapata maji safi, salama na yenye uhakika.