Rais wa Tanzania, John Magufuli ameitaka Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi kuzirejesha serikalini shule za sekondari ambazo imeshindwa kuziendesha ili ziboreshwe na kutoa elimu bora kwa wanafunzi.
Ametoa agizo hilo leo kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Jumuiya ya Wazazi mjini Dodoma ambapo amesema ili kuipunguzia majukumu ya kuhudumia jamii, serikali iko tayari kuzichukua baadhi ya shule ili ziendelee kutoa huduma bora ya elimu kwa wanafunzi wa Tanzania.
“Uongozi utakaokuja na ninyi Jumuiya ya Wazazi kama mtaona inafaa kwa baadhi shule ambazo mmeshindwa kuziendesha na hasa katika shule hizi 54 mkaamua shule 10 au 20 kwamba zichukuliwe na serikali tutazichukua kwa ajili ya kufidia hayo madeni”, amesema rais Magufuli.
Ameibainisha kuwa mpango wa serikali kutoa elimu bure kwa shule zake umeleta changamoto kwa shule zinazomilikiwa na watu binafsi kukosa wanafunzi kwasababu wengi wanakimbilia kwenye shule za serikali ili kukwepa gharama za masomo.
“Ninafahamu bado kuna changamoto kubwa kwenye shule zetu kwasababu ya sera ya elimu ya sasa hivi tunatoa elimu bure. Kwa hiyo unapokuwa na shule nyingi za serikali zinazotoa elimu bure ni vigumu sana kupata wanafunzi watakaoenda kwenye shule ya kulipia”, amesema rais Magufuli.
Jumuiya hiyo ya CCM ambayo inamiliki miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii, pia imewekeza katika sekta ya elimu ambapo ina shule 54 za sekondari na Chuo kimoja cha Ufundi cha Kaole kilichopo mkoa wa Pwani ambacho kinatoa Astashahada ya Kilimo na Mifugo.
Mchakato wa kuzirejesha baadhi ya shule za jumuiya hiyo mikononi mwa serikali umeanza, ambapo shule ya sekondari ya Omumwani iliyoko mkoa wa Kagera imerejeshwa ili kuboresha huduma zake kwa kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
Shule hiyo iliwachukua wanafunzi wa shule mbalimbali mkoani humo ambazo ziliharibiwa na tetemeko la ardhi lililotokea Sepetemba 2016. Kwasababu ilikuwa ni shule ya kulipia serikali imeibadilisha umiliki wake kutoka kwa Jumuiya ya Wazazi kuifanya kuwa ya umma.
“Mwaka jana tulipoenda Kagera baada ya tetemeko nilitembelea shule ya Omumwani na nikaona huduma nzuri ilizokuwa inatoa kwa wanafunzi waliokuwa shule zao zimeanguka. Nikatoa maagizo mlikubali kupokea wanafunzi wa serikali na shule mbalimbali katika mji wa Bukoba na mkaanza kuwahudumia pale”,
“Baadaye nikawaomba kwamba shule sasa tuichukue iwe ya serikali, mlinikubalia tumeichukua, tukabaki namna ya kutafuta fedha za kulipa. Wiki iliyopita tumelipa hizo bilioni 1.7”, amesema rais Magufuli
Hata hivyo, ameitaka Jumuiya hiyo kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa ajili ya manufaa ya taasisi hiyo muhimu kwa chama tawala, “Jumuiya ya wazazi haitafutwa nikiwa mimi Mwenyekiti wenu. Ni muhimu kwa maendeleo ya chama lakini ni muhimu kwa ustawi wa taifa letu”.
Shule ya wazazi ya sekondari ya Meta iliyopo mkoani Mbeya
Jumuiya ya Wazazi
Jumuiya ya Wazazi CCM ni zao la Tanzania Parents Association (TAPA) iliyoanzishwa mwaka 1955 chini ya Chama cha Tanganyika National African Union (TANU) ambacho kilikuwa chama cha ukombozi wa Tanzania Bara.
Jumuiya hiyo ni moja ya nguzo tatu za CCM zikiwemo Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambazo wajumbe wake watahudhuria Mkutano Mkuu wa kumchagua Mwenyekiti wa Chama hicho ambaye atahudumu kwa miaka mitano kuanzia sasa.
Miradi ya CCM
Licha ya kumiliki shule na chuo, CCM inaendesha miradi mbalimbali vikiwemo viwanja vya mpira ukiwemo Uwanja wa CCM Kirumba (Mwanza), Samora (Iringa), Sokoine (Mbeya), Sheikh Amri Abed (Arusha), Majimaji (Songea) na Kaitaba (Kagera).
Inaelezwa kuwa enzi za chama kimoja, majengo na maeneo yote ya umma yalikuwa chini ya Serikali. Ujenzi na uendelezaji wa maeneo hayo ulifanywa na serikali kupitia kodi za wananchi, michango, fedha za wafadhili na wahisani mbalimbali. Lakini kumekuwa na mkanganyiko kwa umiliki wa baadhi ya mali za CCM ambazo zilipatikana kwenye mfumo wa chama kimoja.
Kwa nyakati tofauti wananchi wamekuwa wakitoa maoni yao, wengine wakitaka miradi hiyo ya viwanja na shule virudishwe serikalini kwasababu nchi imeingia kwenye mfumo wa vyama vingi na miradi hiyo ilianzishwa kwa fedha za wananchi.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni
Mwaka 2009 akiwa Bungeni, Waziri Kivuli wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ aliitaka serikali kuvirudisha viwanja vyote nchini vinavyomilikiwa na CCM ili vitoe huduma sawa kwa wananchi hata wasio na vyama.
“Viwanja hivi nilivyovitaja na vinginevyo vilijengwa na wananchi wote wakati wa utawala wa chama kimoja na hivyo CCM haipaswi kuvimiliki bali serikali ambayo ni ya wananchi wote inatakiwa ivimiliki”,
“Mbali na sababu hiyo, viwanja hivyo havihudumiwi kwa kiwango, tunaitaka serikali ivirejeshe mikononi mwake na kuanzisha mamlaka itakayovihudumia”.
Uamuzi kama huo wa kuzirudisha mali za chama mikononi mwa serikali, ulifanyika nchini Kenya wakati wa utawala wa rais Mwai Kibaki ambapo ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta uliokuwa mikono mwa chama cha ukombozi wa Kenya cha KANU ulirejeshwa chini ya usimamizi wa serikali.