Waziri Ummy Mwalimu awaagiza wataalamu wa afya kuzigeukia tiba asili

Jamii Africa

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewaagiza wataalamu wa wizara yake kuwekeza katika tafiti za tiba asili ili kuboresha utolewaji wa huduma hiyo katika maeneo ya vijijini.

Akizungumza katika kipindi cha ‘NjooTuongee’ kinachorushwa na runinga kwa ushirikiano wa taasisi ya Twaweza na JamiiForums amekiri kuwa serikali haijawekeza rasilimali za kutosha katika sekta ya tiba asili ambayo inatumiwa na watu wengi hasa waishio vijijini ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali za upatikanaji wa huduma za afya.

“Watanzania kwa asilimia 60 wale wanaoishi vijijini wanatumia tiba za asili”, amesema Waziri Ummy na kuwataka watendaji wa wizara yake kupokea changamoto hiyo ikizingatiwa kuwa tiba hiyo imekuwa ikitolewa isivyotakiwa na baadhi ya watu ambao hawana taaluma ya uuguzi.

“Tunasisitiza watu watoe tiba sahihi lakini kama Serikali hatujawekeza zaidi katika sekta hii na nimewapa changamoto hii wataalamu wa Wizara yangu”, amesema.

Amebainisha kuwa wanaendelea kufanya tafiti mbalimbali kwa shirikiana na watu wanaotoa tiba za asili na kutengeneza mazingira mazuri ya kutolea huduma hiyo ili iwafaidishe wananchi wanaopendelea huduma hiyo.

Changamoto iliyopo kwa baadhi ya watu wanaotoa huduma ya tiba asili ni kutozingatia taratibu za kitabibu ikiwemo vipimo na kiwango cha dawa ambacho mgonjwa anapaswa kupewa. Lakini bado watanzania wengi wameendelea kutumia tiba hizo ikiwa ni njia mojawapo ya kukabiliana na upungufu wa vituo vya afya na madaktari.

Hata hivyo, Waziri Ummy amekiri kuwepo kwa changamoto katika sekta ya afya ambazo zinahatarisha maisha ya watanzania ambao taifa linawategemea katika shughuli za uzalishaji mali na kuwa serikali inafanya jitihada mbalimbali kuboresha miundombinu ikiwemo upatikanaji wa vifaa tiba, dawa na uwepo wa madaktari na wauguzi wa kutosha kwenye vituo vya afya.

“Tunakubali ipo changamoto lakini tunajitahidi kutafuta suluhu. Nimejifunza kuwa Matibabu ni uchunguzi  lakini kama serikali tunaendelea na jitihada za kuboresha huduma za afya”, amesema waziri Ummy.

Katika mwaka wa fedha wa 2017.2018 serikali imetenga trilioni 2 ambazo zimeelekezwa katika sekta ya afya na kuiweka miongoni mwa sekta zinazopewa kipaombele  katika bajeti ya serikali.  

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu (kushoto) akiwa na watangazaji Maria Sarungi (katikati) na Mkurugenzi Mkuu wa Twaweza, Aidan Eyakuze (kulia) katika kipindi cha 'Njoo Tuongee' kinachorushwa na runinga ili kuongeza uwajibikaji na uwazi wa viongozi wa serikali

Ameeleza kuwa wizara yake inaendelea na mchakato wa kutengeneza mfumo mzuri ambao utafanikisha wananchi kutumia bima ya afya ili kuepuka gharama kubwa za matibabu ambazo hawawezi kuzimudu. Pia amewataka wahudumu katika vituo vya afya kutanguliza utu na kuwajali wagonjwa wanaoenda kutibiwa katika vituo vyao.

“Huo ni Mkakati wa kuwahamasisha Wananchi kutumia bima ya afya na hatakiwi mtu kunyimwa matibabu kwa kigezo cha fedha, matibabu kwanza Fedha baadaye”.

 

Changamoto katika sekta ya Afya

Changamoto kubwa sekta ya afya nchini ni uhaba na mgawanyo usio sawa wa madaktari katika amaeneo mbalimbali ya nchi. Kulingana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaeleza kuwa Tanzania ina upungufu wa watumishi wa afya 95,059 ambapo waliopo ni 89,842 ili kukidhi mahitaji yote wanahitajika watumishi 184,901. Upungufu huo ni zaidi ya nusu ya watumishi wa afya wanaohitajika nchini.

Akizungumza hivi karibuni katika ufunguzi wa hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mloganzila iliyopo mkoa wa Pwani, Rais John Magufuli alikiri kuwepo kwa mgawanyo usio sawa wa watumishi wa afya nchini.

“Mfano mwingine ni wa hapa hapa Dar es Salaam, hospitali ya Manispaa ya Temeke yenye kuhudumia wastani wa wajawazito  wanaojifungua 100 kwa siku ina madaktari bingwa wakina mama wawili. Lakini hospitali ya Taifa ya Muhimbili yenye kuhudumia wastani wa wakina mama wanaojifungua katika ya 40 na 50 kwa siku ina madaktari bingwa 40 ukiachilia mbali ya madaktari wanafunzi waliopo. Hii inadhihirisha kuwa hakuna mgawanyo mzuri wa madaktari wachache tulionao”, alinukuliwa rais na vyombo vya habari.

Utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza (2017) unabainisha kuwa changamoto nyingine iliyopo katika vituo vya afya vya serikali ni ukosefu wa dawa muhimu ambapo asilimia 70 ya wananchi walioenda kutibiwa walisema hawakukuta dawa kwenye maduka ya vituo hivyo.

 

Hizi ndizo changamoto zinazopaswa kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuwaepusha wananchi na tiba zisizo za uhakika ambazo hazijathibitishwa kisayansi.

Sera ya Afya ya mwaka 2007, inaielekeza serikali  kuinua hali ya afya ya wananchi wote na hasa wale walioko kwenye hatari zaidi, kwa kuweka mfumo wa huduma za Afya utakaokidhi mahitaji ya wananchi na kuongeza umri wa kuishi wa watanzania. Kutoa huduma muhimu za afya zenye uwiano wa kijiografia, viwango vya ubora unaokubalika, gharama nafuu na zilizo endelevu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *