Sababu za wanawake kuishi muda mrefu kuliko wanaume

Jamii Africa

Daniel Samson

Kila binadamu aliyezaliwa huongezeka kimo kuanzia akiwa mtoto, kijana na hatua ya mwisho ni uzee na kifo. Kifo hakina kanuni  na kinaweza kumpata mtu yoyote wakati wowote.

Matarajio ya watu wengi ni kuishi  mpaka uzeeni lakini umri wa kuishi hutofautiana  toka nchi moja hadi nyingine kulingana na mazingira yanayowazunguka watu wa taifa husika.

Umri wa kuishi pia hutofautiana kati ya wanaume na wanawake, ambapo wanawake katika maeneo mbalimbali wanaishi miaka mingi kuliko wanaume.  Nchi ya Sweden ambayo inaaminika kuwa na huduma bora za kijamii, umri wa kuishi kwa wanawake ni  miaka 83.5 na wanaume 79.5. 

Utafiti uliofanywa na Chuo cha Imperial cha London (2017) na Shirika la Afya Duniani uliangazia umri wa kuishi katika mataifa 35 yaliyostawi kiviwanda na ulibaini kwamba wanawake nchini Korea Kusini watakuwa wa kwanza duniani kuwa na umri wa kuishi wa zaidi ya miaka 90.

Utafiti huo unaeleza kuwa watu watakuwa wakishi miaka mingi kuliko sasa kufikia mwaka 2030 na pengo kati ya wanaume na wanawake litaanza kufutika katika mataifa mengi.

Kwa Tanzania, idadi kubwa ya wanawake wanaishi hadi miaka 63 na wanaume miaka 61, ambapo umri huo wa kuishi umeongezeka kutoka miaka 57 kwa wanawake na 54 kwa wanaume kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi, 2012. Tofauti inayojitokeza ni kuwa wanawake wanaishi muda mrefu kwa zaidi ya asilimia 2 kuliko wanaume.

Licha ya wanawake kuishi muda mrefu lakini inatajwa katika tafiti mbalimbali kuwa wanawake wa Afrika hufariki zaidi wakiwa katika umri wa miaka 15 na 34 kutokana na matatizo ya uzazi na huduma duni za afya.

Zimekuwepo hisia kuwa kazi ngumu kwa wanaume ndizo zinawamaliza mapema.  Lakini hoja hii haina nguvu kwa wakati huu kwasababu wanaume na wanawake wote wanajihusisha katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali toka migodini, mashambani hadi katika biashara.

Unywaji wa pombe, kuvuta sigara na kula chakula kupita kiasi imetajwa kama sababu nyingine ya wanaume kufa mapema. Watetezi wa sababu hii wanasema matumizi ya pombe na sigara huathiri baadhi ya viungo vya mwili.

Wanatoa mfano wa wanaume kutoka nchi ya Urusi ambao hufariki miaka 13 mapema kuliko wanawake kwa sababu wengi wao wamekithiri kwenye unywaji wa pombe na uvutaji wa sigara.

Kutokuwa na ajira kwa mwanaume kunaweza kumsababishia afe mapema. Kulingana na riport ya Mtandao wa Afya ya Wanaume (MHF) inasema 20% ya wanaume wasio na ajira wana uwezekano wa kufa mapema kuliko wanaume walio na kazi. “Wote tunafamu kuwa wagonjwa wengi hawafanyi kazi” anasema Martin Tod,  Mkurugenzi Mtendaji wa MHF.  “Ripoti yetu inaonyesha kuwa mwanaume  ambaye hajaajiriwa anakuwa mgonjwa”

Watafiti mbalimbali wanakubaliana na sababu ya kibaolojia na mabadiliko ya watu kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

“ Ni kweli mitindo ya maisha inachangia lakini haichukuliwi kama jambo ambalo limejikita katika  maumbile ya mwanadamu” anasema Tom Kirkwood,  mwanafunzi wa Chuo Cha Newcastle nchini Uingereza.

 

Vinasaba Vilivyo katika mwiili wa mwanadamu (DNA) vinatofautiana katika kufanya kazi na kuweza kuhimili mabadiliko ya kimazingira. Inatajwa kuwa mwanamke ana DNA ambayo ina kromosumu  X na Y na mwanaume ana X ambayo ikichoka hana nyingine ya kumsaidia ikilinganishwa na mwanamke mwenye mbili ambapo moja ikichoka nyingine huendelea kuhimili  mabadiliko ya kiafya kwa muda mrefu.

Mtaalamu wa maabara nchini Ujerumani, Dk James Vaupel anadai kuwa vinasaba huchangia kasi ya kuzeeka kwa asilimia tatu pekee na sehemu kubwa ya visababishi vya kuzeeka haraka hutokana na mtindo wa maisha usiofaa pamoja na lishe duni.

Magonjwa ya moyo yanachangia pia kwasababu ya msongo wa mawazo ambao wanaume wanakutana nao katika majukumu ya kila siku na kuwapunguzia umri wa kuishi. Wanawake hawako katika hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo kutokana na mfumo wao wa damu ambao kila mwezi hupata hedhi na kuwasaidia kusafisha damu.

Upatikanaji wa huduma za afya, pesa na mabadiliko ya kiuchumi katika familia nayo huchangia wanaume kufa mapema.

 

Hali ilivyo Afrika Mashariki

Umri wa kuishi kwa wananchi wa Tanzania hautofautiani sana na wananchi wa nchi nyingine za Afrika Mashariki. Kwa Burundi wanawake huishi hadi miaka 62 na wanaume miaka 58,  huku Kenya miaka 65 kwa wanawake na wanaume (62).

Kwa upande wa Uganda, wanawake (56), wanaume (54) na Rwanda inakaribiana na Kenya ambapo wanaume huishi kwa wastani wa miaka 58 na wanawake (61).

Licha ya umri wa kuishi kati ya mwanamke na mwanaume kutotofautiana sana kwa wananchi wa Afrika Mashariki, bado kuna watu wanaishi hadi miaka 80 na wakiwa na nguvu wanafika miaka 100.

 

Mambo ya kuzingatia ili kuishi muda mrefu

Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa wakazi wa maeneo mbalimbali wanaoishi maisha marefu zaidi duniani kama vile Japani, Italia na Marekani, pamoja na mambo mengine, wanajiepusha na matumizi ya vileo, tumbaku na kupunguza ulaji wa nyama nyekundu.

Nyama yenye shida kubwa ni ile yenye mafuta mengi, nyama choma iliyoungua na ile iliyosindikwa. Nyama ya namna hii huchangia kutokea kwa magonjwa ya moyo, kiharusi, kisukari na saratani ya utumbo. Hii inasababisha uzalishaji wa kemikali zinazodhuru afya.

Pia kuvuta hewa safi ya kutosha na kupata mapumziko ya kutosha baada ya kazi ngumu kila siku. mazoezi na kula chakula asilia cha mimea kama vile mbogamboga na matunda kwa wingi.

Vyakula vya asili vineelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa matokeo ya watu kuishi miaka mingi kuliko wale ambao hawazingatii utaratibu huo.

Wataalamu wa masuala ya afya ya jamii wanaongeza kusema kuwa, uhusiano bora na mtazamo chanya katika maisha huongeza urefu wa maisha kwa miaka saba na nusu.
 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *