TANESCO kuendelea kupinga tuzo ya DOWANS mahakamani?

Jamii Africa

LICHA ya kuwa hukumu iliyotolea na Mahakama Kuu katika kukamilisha kusikiliza upinzani dhidi ya kusajiliwa tuzo ya DOWANS ambayo ilitolewa na mahakama ya kimataifa ya biashara (ICC) ilikuwa wazi na isiyo na kipingamizi kuhusu vipengele vya sheria, wanaharakati nchini bado hawajakata tamaa.

Wanaendelea kuisukuma TANESCO iendelee kudai mahakamani kuwa tuzo hiyo isisajiliwe, wakianzia kilichoonekana katika taarifa ya Kamati ya Bunge ikiongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe mapema mwaka 2008. Wanadhani kwa vile ile ilikuwa Kamati ya Bunge, ilichokiona kina nguvu ya sheria, na kupitisha uamuzi mahakamani unaokinzana na
hisia ya msingi ya kilichoonekana na Kamati, kuwa mkataba wa Richmond/DOWANS ulikuwa batili, ni sawa na kuvunja sheria – hivyo kutambua uamuzi wa ICC ambao unajikita katika mkataba wa awali wa Richmond inakuwa kosa.

Kimsingi wanachotaka wanaharakati na wanachofuatilia mawakili wa TANESCO katika kupeleka madai ya kutengua maamuzi ya Mahakama Kuu katika Mahakama ya Rufani ni kusema kuwa kwa vile Bunge linatunga sheria, na chini azimio la Bunge la Januari 2008 mkataba huo ulikuwa baitli, ni wazi kuwa tuzo ya Dowans ambayo msingi wake ni mkataba huo itakuwa batili.

Wanachotaka, na baadhi wana uhakika kabisa na madai hayo, ni kuwa usajili wa tuzo ya ICC haufanyiki kwa sheria za ICC ila za Tanzania, hivyo pale ambapo ni wazi mtiririko wa ‘kutunga sheria’ kwa suala hilo, yaani jinsi suala hilo lilivyosikilizwa na kuamuliwa bungeni, haiwezekani mahakama ya hapa nchini ikasajili hukumu hiyo kwa msingi wa mkataba wenyewe, na iwe inatumia sheria ya Tanzania katika kuuangalia, au kuutafsiri, mkataba wenyewe.

Hii ni sawa na kutaka Mahakama ya Rufani ibatilishe mkataba na usiwe na nguvu kisheria, ambayo katika hali halisi ni kutaka kampuni ya DOWANS itumie zaidi ya dola milioni 120 kuingia gharama za kuleta mitambo nchini, kuiweka na kuzalisha umeme kwa miaka iliyokaribia kufikia miwili (siku 90 tu zilibaki) lakini kazi yote hiyo isiwe na thamani yoyote kisheria kwani msingi wake ulikuwa batili. Na wanaharakati wa Tanesco wanataka kuamini kuwa mtu anaweza akapokea mitambo ya gharama hiyo, akapokea na umeme wa gharama hiyo, akawa anadaiwa dola milioni 24 (shilingi bilioni 32 kwa thamani ya shilingi ya wakati huo) halafu akavunja mkataba kivyake – na atoke mahakamani anacheka kwani hakufanya kosa lolote kwani Bunge lilisema mkataba huo ni batili. Ni kile Mwalimu Nyerere alichosema ni kesi ya nguruwe kupelekewa ngiri, kuwa atashinda hata iweje!

Ambacho wanaharakati wanashindwa kuelewa ni kuwa Tanzania ni sehemu ya mfumo wa biashara duniani ambako sheria na kanuni za kutafsiri sharia zinatakiwa zifanane, na kwa msingi huo kinachoangaliwa katika tafsiri ya sheria ya suala hilo ni Commonwealth (common law) commercial law, yaani mtiririko wa maamuzi ya mivutano ya kibiashara Uingereza na India.

Kwa maana hiyo wanaharakati wanajidanganya wenyewe wanapotaka mahakama ya Rufani iangalie suala hilo katika mtiririko wa Kitanzania, tena wa kujali tu hisia za Bunge kuhusu suala hilo, na siyo mapana na marefu ya suala lenyewe –kuwa kuleta mitambo nchini kunahitaji mkataba, kwani Dowans haikuwa na uwezo wa kuingiza na kuwekeza, ifunge mashine za
kufua umeme ianze kuzalisha na kuuza umeme kivyake; inabidi shughuli hiyo ifanywe na Tanesco.

Kwa maana hiyo mkataba na Tanesco usingekwepeka, na kama mitambo hiyo ilifika ikatumika, kulikuwa na msingi wa shughuli hiyo, yaani mkataba, ambao ulikuwa unaridhisha kwa Dowans hivyo wakaridhia kugharamia kuleta mitambo na kuanza kutumika, ikitazamiwa chini ya mkataba huo kuwa ingetumika kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuhitaji mkataba mwingine, au kuondolewa mashine, au kununuliwa na yeyote ‘huku Tanesco ikiwa na haki ya kwa kwanza kukataa,’ kama ilivyo kawaida, kwani ndiye mlengwa wa kwanza wa mitambo hiyo kuletwa, na muathirika wa kwanza kama ingeuzwa bila wao kupewa nafasi kuinunua.

Makala haya yameandikwa na Erick Kabendera wa FikraPevu

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *