Ukosefu wa takwimu zinazojitosheleza za meli, maeneo ya bahari zinakoendesha shughuli za uvuvi umekuwa kikwazo kwa serikali za nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania kukabiliana na uvuvi haramu usiozingatia sheria na mipaka ya kimataifa, utafiti mpya umeeleza.
Utafiiti uliotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Overseas Development ya nchini Uingereza unaeleza tatizo la uvuvi haramu kwenye bahari kuu ikiwemo bahari ya Hindi unachochewa zaidi na ukosefu wa miundombinu ya mawasiliano, ushirikiano na teknolojia ya kutunza takwimu za meli za uvuvi kwenye bahari kuu ikiwemo bahari ya Hindi ambayo inaunganisha mataifa mbalimbali duniani.
Tatizo ni kubwa kwa nchi za Afrika ambazo hazina teknolojia ya kisasa na taasisi imara za kusimamia uvuvi ambapo kila mwaka nchi za Afrika Magharibi zinapoteza Dola bilioni 2 za kimarekani huku nchi zinazotumia bahari ya Afrika Mashariki (Kenya, Tanzania, Mauritius, the Comoros, Mozambique, and the Seychelles ) zinapoteza zaidi dola milioni 200 kila mwaka.
Licha ya kila nchi kuwa na taratibu zake kupambana na uvuvi haramu, hazijafanikiwa kumaliza tatizo hilo na changamoto inayojitokeza kwenye ukusanyaji wa takwimu na matumizi ya vifaa vya kusimamia mwenendo wa meli katika eneo la bahari kuu.
Utafiti huo unaeleza kuwa ili kufuatilia eneo na safari, meli zinapaswa kuwa na kifaa cha mawasiliano kinachojulikana, ‘Vessel Management Systems (VMS)’. Hata hivyo meli nyingi hazina kifaa hiki hasa katika nchi zinazoendelea ambako teknolojia hiyo haipatikani au wasimamizi wa meli huzima ili kuepuka kufuatiliwa na mamlaka husika.
Licha ya kifaa cha VMS kuwa na uwezo wa kutambua eneo, umbali na mwelekeo wa meli lakini hakiwezi kutambua meli zinazoharibu mazalia ya samaki na viumbe wengine wa baharini.
Pia ukosefu wa takwimu za pamoja za dunia za meli za uvuvi ni changamoto nyingine. Vyombo vya baharini hubadilisha mara kwa mara bendera, umiliki na uendeshaji huku takwimu za umiliki zikiwa mikononi mwa mashirika ya kimataifa, mataifa yanayotoa usajili wa meli na bodi za leseni za uvuvi.
Kulingana na Shirika la Chakula Duniani (FAO) linaeleza kuwa kuna meli 75,000 hadi 779,000 kati ya milioni 4.6 zinazojihusisha na uvuvi haramu duniani kote.
Duniani kote suala la uvuvi haramu ni tatizo kubwa ambalo lina athari kwenye shughuli za kijamii, kiuchumi na mazingira. Kwa Afrika tatizo ni kubwa zaidi katika nchi za Afrika Magharibi ambapo sekta ya uvuvi inakabiliwa vikwazo vya kimataifa kutokana na kukithiri kwa uvuvi haramu. Kila mwaka nchi hizo hupoteza dola bilioni 2.3 za Marekani na kuathiri usalama wa chakula, uchumi wa watu wanaotegemea uvuvi kama shughuli ya kuwaingiza kipato.
Uvuvi haramu umechangia utekaji wa meli kwenye mwambao wa Somalia kati ya mwaka 2009 na 2012. Wavuvi haramu wanatumia njia mbalimbali kuhalalisha uhalifu wao ikiwemo kupeperusha bendera za nchi ambazo hawana usajili nazo, mikataba ya siri ya uvuvi. Mwaka 2017, taasisi ya Conservation Advocacy Oceana ilibaini meli 19 zilizokuwa zinapeperusha bendera ya Umoja wa Ulaya huku zikivua samaki kinyume na sheria kwa masaa 32,000 kwenye maji ya Afrika kwa miaka 3.
Taasisi ya Overseas Development inaeleza kuwa upatikanaji wa takwimu za uvuvi, kuwekwa wazi kwa uvuvi haramu, ushirikiano wa serikali za nchi mbalimbali zinaweza kuongeza uelewa na utashi wa kisiasa dhidi ya uvuvi haramu.
Kikosi Kazi cha FISH- iAfrica
Mafanikio ya kupambana na uvuvi haramu kwenye mwambao wa bahari ya Hindi unatokana na mtandao wa FISH-I Africa ambao unaziwezesha nchi washirika kubadilishana taarifa za kijasusi juu ya uvuvi. Mtandao huo ulianzishwa na shirika lisilo la kiserikali la Stop Illegal Fishing na unajumuisha nchi 8 zikiwemo Tanzania, Madagascar na Somalia.
FISH-i Africa inakusudia kuunda mtandao mpana wa Afrika utakaopambana na uvuvi haramu na uharamia kwenye bahari kuu zinazozunguka bara hilo.
Mwaka 2015 meli ATLANTIC WIND ilikamwata nchini Cape Verde, hata hivyo iliachiwa lakini iliendelea kukiuka masharti ya usajili wake. Mwaka jana, Mamlaka ya Usafiri wa Majini ya Zanzibar iliifutia usajili meli hiyo kwasababu ya kukithiri katika vitendo vya uharamia na uvuvi haramu.
Wiki iliyopita, Serikali nchini Ugiriki iliikamata meli yenye usajili wa Tanzania, eneo la Crete nchini humo ikiwa na shehena ya kutengeneza silaha za milipuko. Shehena hiyo ilichukuliwa nchini Uturuki, na ilikuwa ikipelekwa Misrata, Libya.
Hata hivyo, Serikali imechukua hatua ya kupitia usajili wa meli zote ambazo zinapeperusha bendera ya Tanzania kutokana na ongezeko la meli zinazojihusisha na uharifu wa kimataifa ikiwemo kusafirisha madawa ya kulevya, vilipuzi pamoja na uvuvi haramu.