Haki ya Faragha ni miongoni mwa haki za msingi ambazo zinatambulika kimataifa ambayo hulinda uhuru na taarifa muhimu za mwananchi mmoja mmoja zisifahamike kwa watu au umma. Msingi wa haki ya faragha ni kuhakikisha kila binadamu haingiliwi kwa mambo anayoyatenda isipokuwa tu akivunja sheria za nchi.
Haki hiyo inagusa kila sekta ambapo katika huduma za afya, taarifa za mgonjwa ni siri hazitolewi hadharani mpaka mgonjwa mwenyewe aridhie. Taarifa za watumiaji wa simu za mkononi na mitandao ya kijamii ni siri kati ya mtumiaji na mtoa huduma.
Ripoti ya Waangalizi wa Haki za Binadamu (Human Rights Watch) iliyotolewa Januari 2018 imeainisha baadhi ya matukio yaliyotokea nchini Tanzania mwaka 2017 ambayo yanaweza kutafsiriwa kuwa ni kuingiliwa na kuvunjwa kwa haki ya faragha hasa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wanakosoa mwenendo usiofaa wa baadhi ya viongozi wa serikali.
Pia mitandao ya kijamii inatumika kuibua vitendo vya ufisadi na rushwa kwenye sekta mbalimbali nchini, lakini ulinzi wa watu wanaotoa taarifa hizo muhimu kwa jamii uko mashakani kwasababu wanakabiliwa na vitisho, kuvamiwa na kupigwa na watu wasiojulikana.
Sehemu ya ripoti hiyo imeelezea tukio la Polisi wa Tanzania kumkamata Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa JamiiForums, Maxence Melo mwaka 2016 kwasababu alikataa kutoa taarifa za baadhi ya watumiaji wa mtandao wa JamiiForums ili zisaidie kwenye upepelezi wa kesi.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa, “Mamlaka zimekuwa zikiwakamata bila sababu za msingi au wakati mwingine kuwatisha na kuwasumbua wanaharakati wa haki na baadhi ya wanachama maarufu wa vyama vya upinzani ambao walikuwa wakikosoa serikali au Rais.
Desemba 13, 2016, polisi walimkamata Bwana Maxence Melo, mtetezi maarufu wa haki za binadamu na mmiliki wa mtandao wa kijamii JamiiForums, ambao ni tovuti binafsi ya kuibua maovu na kutoa taarifa pamoja na Bwana Mike William, ambae ni mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Jamii Media, ambayo ndiyo inayohodhi tovuti hiyo.
Tovuti hiyo huchapisha makala na mijadala inayoweka hadharani vitendo vya rushwa katika sekta ya umma na kukosoa vitendo vya serikali. Polisi walifanya msako katika ofisi za JamiiForums na nyumbani kwa Melo ambapo inaripotiwa kuwa walichukua nakala kadhaa za nyaraka.
Disemba 16, 2016, Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam ilifungua mashtaka dhidi ya Melo, chini ya sheria tata ya Makosa ya Mtandao (CyberCrime Act of 2015), mashtaka yakiwa ni pamoja na kukwamisha upelelezi kwa kukataa kutoa majina ya wachangiaji wa JamiiForums wasiotaka majina yao kujulikana, na “kuendesha tovuti ambayo haijasajiliwa Tanzania.” Kesi yao ilianza kusikilizwa mwezi Agosti 2017 na inaendelea mpaka wakati taarifa hii inaandikwa”.
Mpaka sasa JamiiForums inakabiliwa na kesi tatu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambapo kesi mbili zinagusa moja kwa moja haki ya faragha na uhuru wa kutoa maoni.
Miongoni mwa kesi hizo ni Kesi namba 457 inayoikabili JamiiForums, kuhusu kampuni ya CUSNA Investment na Oceanic Link ambayo ilidaiwa kufoji nyaraka bandarini, kukwepa kodi na kuwatesa wafanyakazi wazalendo na kupendelea wageni toka nje ya nchi.
Katika kesi hiyo, Polisi walitaka JamiiForums iwapatie taarifa za mwanzisha mada na mchangiaji mmoja ili waweze kuwakamata na kuwahoji kutokana na ukiukwaji wa taratibu, JamiiForums inadaiwa ilikataa kutoa taarifa binafsi za mwanachama wake kwa kuamini kuwa chanzo hicho cha taarifa kilikuwa na nia njema hivyo kutaka kwanza iwepo Hati ya Mahakama inayoridhia kukamatwa kwa mhusika na kuelezwa kosa lake.
Kesi ya pili ni 456 ambayo inawakabili JamiiForums ni washtakiwa na kampuni ya Oilcom ambayo inadaiwa kukwepa kodi na kuchakachua mafuta bandarini. Oilcom ilidai kuwa taarifa hizo sio za kweli na zinalenga kuchafua jina la kampuni hiyo.
Mwaka huo huo wa 2016, Polisi iliwakamata Wakurugenzi wa JamiiForums akiwemo Maxence Melo ili wasaidie kupatikana kwa taaarifa za mtumiaji wa mtandao wa JamiiForums, Furheer JF Expert Member kujieleza juu ya taarifa aliyoweka kwenye mtandao huo dhidi ya Oilcom. Kesi zote mbili zinaendelea kusikilizwa kabla ya kutolewa uamuzi wa mwisho.
Tangu mwaka 2013 baada ya kutolewa kwa taarifa muhimu za Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kulikofanywa na mfanyakazi wa shirika hilo, Edward Snowden kwa nchi ya Urusi, haki ya faragha imeendelea kuibua mjadala wa kimataifa juu ya umuhimu wa kulinda haki hiyo.
Mwaka 2017 kampuni ya Apple inayotengeneza simu za Iphone ilikataa kutoa taarifa za mteja wake ambaye alituhumiwa na CIA kuhusika na vitendo vya kigaidi. Hata CIA walipotafuta kibali cha mahakama kupatiwa taarifa hizo, kampuni hiyo ilikataa kwasababu ya kuheshimu na kulinda faragha ya wateja wake.
Hata hivyo, swali linabaki kuwa haki ya faragha itaendelea kuwepo katika kipindi hiki ambacho teknolojia ya kufuatilia na kuzifikia taarifa za watu imeongezeka?