Tarime: CHADEMA yavuna zaidi ya wanachama 3,500 wakiwemo viongozi wa CCM

Jamii Africa

OPARESHENI maalumu ya ‘Vua gamba vaa Gwanda’ inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imeitikisa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, baada ya zaidi ya wanachama 3,500 wakiwemo viongozi wa CCM kujiunga na CHADEMA wilayani hapa.

Mbali na idadi hiyo ya watu kujiunga na CHADEMA, pia wananchi wengi wamegombania kadi za chama hicho kama njugu, ikiwa ni lengo la kutaka kujiunga na harakati za vuguvugu la kutaka kuleta mabadiliko ya kisiasa hapa nchini kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2014, na hatimaye uchaguzi mkuu mwaka 2015.

heche-tarime

 

kadi-ccm

Picha ya kwanza: Mwenyekiti wa Bavicha taifa, John Heche akiwa amezungukwa na umati mkubwa a wakazi wa Sirari wakinunua kadi za Chadema kwenye mkutano wa hadhara. Picha ya pili, Heche akipokea kadi za CCM kutoka kwa mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Sirari Tarime, Masha Vincent baada ya kutangaza kuhamia Chadema. (Picha zote na Sitta Tumma)

Wanachama hao wakiwemo viongozi wa CCM wamejiunga na CHADEMA wakati wa mkutano wa hadhara wa chama hicho, uliofanyika mjini Sirari kisha kuhutubiwa na mwenyekiti wa Baraza la Vijana taifa wa chama hicho (BAVICHA), John Heche.

Miongoni mwa viongozi wa CCM waliorudisha kadi kisha kukabidhiwa kadi za CHADEMA mkutanoni hapo, ni pamoja na mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Sirari, Masha Vincent ambapo mke wake pia Veronika Masha alirudisha kadi ya CCM kisha kujiunga na CHADEMA.

Akizungumza kwa niaba ya wanachama wengine wapya waliojiunga na chama hicho kikuu cha upinzani nchini mara baada ya kukabidhiwa kadi za Chadema, Masha alisema wamechukuwa uamuzi huo baada ya kuchoshwa na kile alichodai majungu, fitina na uhasama unaofanywa na baadhi ya viongozi wa CCM wilayani hapa.

Alisema, enzi za CCM zinaonekana kuelekea kuisha, hivyo kujiunga kwao na CHADEMA ni kuongeza vuguvugu la mabadiliko, na kuwaomba vijana kufanya maamuzi ya dhati katika kuleta mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi.

“Mimi nimeamua kuondoka rasmi CCM. Maana yupo kiongozi mmoja hapa Sirari alikuwa anatusakama baada ya kumpinga mambo yake. Sasa tupo kwenye chama makini na chenye mtazamo mpana katika maendeleo ya nchi hii”, alisema Masha kisha kushangiliwa na umati mkubwa wa watu.

Awali, mwenyekiti wa Bavicha taifa, John Heche aliwaomba Watanzania kutumia kura zao vizuri uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 pamoja na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika nchini mwaka 2015 kwa kuipigia kura CHADEMA ili ishike dola na kuleta mabadiliko ya kweli katika maendeleo ya wananchi.

Alisema, CHADEMA imedhamiria kuleta ukombozi mpya kwa wananchi wa taifa hili, na kwamba iwapo Watanzania wataiwezesha kuingia madarakani mwaka 2015, itahakikisha serikali yake inatumia vizuri rasilimali za nchi kwa faida ya Watanzania wenyewe na si wawekezaji.

Aidha, akiwa katika mkutano wa hadhara kule Muriba Tarime jana, Heche alilaani vikali mauji ya vijana yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya askari polisi katika mgodi wa dhahabu wa Nyamongo uliopo wilayani hapa, na kusema upo uwezekano wa kuishtaki serikali ya Tanzania katika mahakama ya Kimataifa ya makosa ya uhalifu (ICC), kuhusiana na mauaji hayo.

Alisema, CHADEMA haiwezi kuendelea kuona Watanzania wanauawa kama wanyama katika wilaya hiyo, hivyo ikibidi ipo siku serikali italazimika kwenda kujibu mashtaka kwenye mahakama hiyo ya ICC kuhusiana na unyama inaowafanyia wananchi wake kwa kuruhusu jeshi lake la polisi kutumia mtutu kuwaua raia mgodini hapo.

“Hatuwezi kukubali vijana wetu, Watanzania wenzetu, wakurya wenzetu waendelee kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika mgodi wa Nyamongo. Ipo siku serikali ikibidi itashtakiwa ICC kutokana na mauaji ya wananchi wetu”, alisema mwenyekiti huyo wa Bavicha taifa, Heche.

Alisema, mgodi wa Nyamongo kama ungelitumiwa vizuri na Serikali ya CCM ingelisaidia kupeleka maendeleo ya elimu, barabara, maji safi na salama ya kunywa, hospitali pamoja na mawasiliano, lakini kwa sasa madini hayo yanatumika kuwanufaisha raia wa nje ya nchi.

Hata hivyo, aliituhumu Serikali ya CCM kupitia kwa Rais Jakaya Kikwete kwamba utawala huo umekuwa ombaomba namba moja kwa misaada huko Ulaya, na kusema wakati mwingine Rais Kikwete huwa anapishana na ndege za wazungu zikiwa zimebeba madini, huku kiongozi huyo naye akitoka Ulaya kuomba vyandarua, jambo ambalo litaenda kudhibitiwa na CHADEMA itakapoingia Ikulu 2015.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma -FikraPevu, Tarime.

3 Comments
  • nchi yetu itajengwa na vijana wote bila kujali elimu,dini na chochote kile iwapo viongozi watawajali vijana na si katika familia zao,hii inatokana na vijana kukosa kazi na viongozi kuwapa ndugu zao ambao hawana elimu kama vijana wakulima waliosoma kwa shida,naiunga mkono chadema asilimia 100

  • Watanzania wa leo sio wa jana wala juzi,tumechoshwa na uongo wa watawala wasio viongozi wa Magamba wanao jijali wenyewe na familia zao huku asilimia kubwa ya Watanzania wakiishi kwa shida na hata kufariki mapema kutokana na ugumu wa maisha.

    Naishangaa serikali ya magamba kufanya ardhi mali ya serikali hiyo wakati ardhi ni mali ya umma yaani wananchi wote.Madini,misitu na vyote ni mali yetu sote,iweje watawala wa magamba wagawe ardhi kwa wanaowaita wao wawekezaji ambao hawana tija kwa jamii.haya mambo ndio yanayowafanya Watanzania tuifagilie CHADEMA ili kikamate DOLA mwaka 2015.

    Big up Tundu,Slaa,Lema,Mnyika,Mdee,Nassari,Mbowe Hakuna Kulala mpaka kieleweke!

  • Songambele CHADEMA, mimi nawapigia kampeni ya nyumba kwa nyumba, tiieni bidii ya kuingia vijijini.

    PEOPLES!!!!!!!! POWEEEERR!!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *