Mbunge wa Monduli Bw. Edward Lowassa amesema kuwa kauli mbalimbali zinazotolewa na wanasiasa kupitia vyombo vya habari zikimhusisha yeye na mpango wa kuihujumu serikali ya Rais Kikwete au Chama cha Mapinduzi ni za kinjozi, hazina ukweli, na haelewi lengo lake hasa ni nini. Akizungumza na waandishi wa habari jimboni kwake Monduli leo Bw. Lowassa amesema kuwa “watu wanaopenyeza taarifa hizi katika vyombo vya habari wanafanya hivyo kwa malengo ya kufikiria ya kujisafishia njia za kisiasa”
Bw. Lowassa alikuwa na kauli rasmi iliyoandikwa kwenye kurasa tano aliyokuwa ameianda na kuisoma mbele ya waandishi wa habari. Alikanusha vikali madai kuwa ana mpango wowote wa kumhujumu Rais Kikwete au Chama cha Mapinduzi ambacho yeye ni mbunge wake. “Ni jambo lisiloingia akilini kunihuisha na kile kinachoitwa mikakati ya kumhujumu rais au chama ambacho mimi ni kada wake wa muda mrefu, mbunge anayetokana na chama hicho hicho na mtu ninayeiongoza Kamati nyeti ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na zaidi ya yote kiongozi wa ngazi mbalimbali za kisiasa na kiserikali nilizowahi kushikilia” alisema Bw. Lowassa kwa msititizo.
Aliendelea na kusema kuwa licha ya kwamba hajawahi kufikiria kuibua “mabaya ya Rais Kikwete” hayo yanayoiwa “mabaya” yeye hayajui. “Mbali ya ya ukweli kwamba huo ni uongo wa wazi, silka yangu kama mwanasiasa na mtu mwenye dhamana kubwa kwa watu wa Monduli kwa taifa languhaiwezi kamwe kunituma nianze kupanga mikakati ya kumhujumu kiongozi wetu mkuu au chama ambacho kimenielea na mimi mwenyewe nikakitumikia kwa uadilifu na kwa juhudi kubwa pengine kuliko hao wazushi” alisema Bw Lowassa.
Akifafanua asili ya madai hayo dhidi yake Bw. Lowassa amesema kuwa “tangu serikali ya Awamu ya Nne iingie madarakani kuna kundi la watu limekuwa likifanya juhudi kubwa kunigombanisha na Rais wakitumia kila aina yoja za kupikwa”. Akifafanua kuhusu kundi hilo Lowassa amesema kuwa “ndilo ambalo mwaka juzi lilipenyeza ndani ya chama chetu na katika jamii hoja kwamba nilikuwa nimejipanga kugombea Urais kwa tiketi ya chama chetu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana likidai kuwa nilikuwa na malengo ya kumpinga Rais Kikwete ambaye alikuwa ndio kwanza anaelekea kukamilisha ngwe yake ya kwanza madarakani”.
Lowassa aliendelea kurudia kauli aliyoitoa huko nyuma kuw yeye na Rais Kikwete hawakukutana na kuanza urafiki wao wakiwa barabarani akimaanisha kuwa urafiki wake ni wa kina sana. Katika mazungumzo yake hayo na vyombo vya habari Lowassa aliviasa vyombo hivyo kuandika habari kwa weledi na siyo kutumia muda mwingi kuandika habari za watu na kuvitishia kuwa ameamua sasa kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya vyombo hivyo na waandishi wa habari. “Nimeamua kuanza kuchukua hatua mbalimbali za kisiasa na kisheria ambazo naamini zitatoa majibu sahihi dhidi ya wale wote walio nyuma ya ajenda hizi chafu kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawia ndani ya chama changu na kwa jamii nzima ya Watanzania ambao kwa muda mrefu wamelishwa mambo mengi ya kizushi wakati mwingine ya hatari dhidi yake” alisema Bw. Lowassa huku akisikilizwa kwa makini.
Hata hivyo kinyume na matarajio ya baadhi ya waandishi katika taarifa yake rasmi Bw. Lowassa hakuzungumzia kabisa mojawapo ya hoja ambazo zimekuwa zikimuandama tangu alipojiuzulu Uwaziri Mkuu mwezi Februari mwaka 2008 kufuatia kuhusishwa kwa ofisi yake na mchakato mbovu ulioingiza nchini kampuni ya Richmond kutoka Marekani ambayo ilikuja kugundulika baadaye kuwa haikuwa na uwezo wala uhalali wa kuingia mkataba wa nishati nchini. Lowassa akiwa Waziri Mkuu ndiye aliyesimamia Timu ya Majadiliano ya Serikali ambayo mojawapo ya matokeo yake ni kuipatia Richmond Mkataba licha ya kampuni hiyo kushindwa vigezo mbalimbali.
Licha kukataa kabisa kuzungumzia sakata la Richmond akidai kuwa muda wa kulizungumzia hilo haujafika Bw. Lowassa alikataa vile vile kuzungumzia “mtoto” wa Richmond yaani kampuni ya Dowans ambayo ilirithishwa mkataba wa kufua umeme ambao Richmond iilingia na Tanesco kinyume cha sheria na mkataba huo kuonekana kuwa ni halali. Katika wakati wa maswali na majibu Bw. Lowassa alisema kuwa hakuwa kwenye mkutano huo kuzungumzia masuala hayo kwani wakati wake haujafika. Alipoulizwa endapo labda amepigwa mkwara kutozungumzia Richmond/Dowans Bw. Lowassa alijibu kwa mkato kuwa “nafikiri haya yanawatosha kwa leo”.
Akizungumzia hali ya kisiasa ndani ya CCM Bw. Lowassa amesema kuwa misuko suko inayoendelea ndani ya chama ni hali ya kawaida na kuwa nayo itapita tu. Alielezea kuwa hali ya taifa iko katika utete wa aina yake hasa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili wananchi. “Taifa linakabiliwa na changamoto nyingi kama zile za utawala bora, kuporomoka kwa thamani ya shilingi kila kukicha, mdodoro wa uchumi, tatizo kubwa la ajira kwa vijana, kushuka kwa kiwango cha elimu na ugumu wa maisha kwa ujumla” alisema Bw. Lowassa wakati wa kuhitimisha taarifa yake rasmi kwa namna kama ya kuishtaki au kuishtumu serikali ya chama chake kwani yote aliyoyasema yametoka chini ya uongozi wa CCM.
Bw. Lowassa ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na mbunge wa muda mrefu hakuzungumzia baadhi ya matatizo ambayo yanawakabili wananchi wengi na taifa kwa ujumla hasa matukio ya uvunjaji wa amani huko Igunga ambacho chama chake kilishinda katika mazingira ambayo yameacha kovu kwa wananchi wa Igunga hasa baada ya madai ya watu kadhaa kuuawa katika mazingira ya kisiasa. Bw. Lowassa hakuzungumzia kama Kamati yake ilikuwa ina mpango wowote wa kutembelea huko Igunga na kufuatilia kilichotokea au matukio mengine ya ulinzi na usalama ambayo yamekuwa yakitokea katika mazingira ya kisiasa kuanzia Januari 5, 2011 huko Arusha.
Pamoja na kuanisha hali inavyoendelea nchini Bw. Lowassa ambaye ni Mbunge mwenye uzoefu wa muda mrefu hakuzungumzia mipango yoyote ya kutumia bunge kubadili kanuni au sheri ambazo zinaonekana kuwa ni sehemu ya tatizo katika utendaji kazi wa serikali au utawala bora au kuhakikisha kuwa mfumo wa uchumi na usalama unafanya kazi ipasavyo.
Mazungumzo ya Lowassa na waandishi wa habari yamekuja siku chache tu baada ya aliyekuwa Spika wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Bw. Samwel Sitta kuzungumza katika kipindi cha 45 Minutes cha ITV ambapo aligusia kwa kina sakata la Richmond na Dowans na kudai kuwa kulipa kampuni hiyo ya Dowans ni wizi wa wazi na ataendelea kupinga. Msimamo wa Lowassa kuhusu kuilipa kampuni ya Dowans haujawahi kuanishwa wazi. Mwenyekiti aliyeongoza Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata hilo la mkataba wa Richmond Dr. Harrison Mwakyembe (mwenye kipaza sauti) hajapatikana kuzungumzia maendeleo ya kisiasa kuhusiana na suala hilo kwani siku chache zilizopita alikimbizwa nchini India ambako anapatiwa matibabu ya ugonjwa wa ngozi na hali yake ikiripotiwa kutengamaa siku kwa siku.
Bw. Lowassa ni mmoja wa wabunge watatu ndani ya CCM ambao wamekuwa wakitajwa tajwa na vyombo vya habari kuhusiana na kasfha mbalimbali na migogoro ndani ya CCM. Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Igunga Bw. Rostam Aziz wa kwanza juu- (ambaye alijiuzulu nafasi zote za uongodi ndani ya CCM na kuamua kuachana na kile alichokiita ‘siasa uchwara’) na Bw. Andrew Chenge ambaye ni mbunge wa Bariadi Mashariki. Bw. Chenge ndiye aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wakati mikataba mbalimbali tata inaingiwa na alidaiwa kunufaika binafsi na baadhi ya mikataba hiyo hasa baada ya kutajwa katika uchunguzi wa SFO ya Uingereza.
Imeandikwa na M. M. Mwanakijiji
Ni jambo la kusikitisha mno kuona Lowassa anakuja na hoja za vitisho kwa hao anaosema wanamfafata na waache kuandika mambo yake,nilitegemea angeiita waandishi wa habari kwa kusomna alama za nyakati kwa kuelezea matatizo yanayo lisibu taifa kwa haraka hasa swala la malipo kwa Dowans,nanilitegemea atakuja na majibu ya kashfa zake mojamoja mfano ile ya tarehe 15/7/2007 kuandika barua kushinikiza kiwanda cha General Tire kupewa haraka Billion 10 bila masharti na wenzake Mramba na Zakia Meghji walikubali,Barua Na.PM/P/1/567/40 kwa lengo kulinda ajira na kiwanda kisifilisike,ajabu pesa zilichakachuliwa hazikufika zote.
Hapo inaonesha jinsi inavyowezekana Lowassa akihisika mnafiki kwa kusimama na kusema serikali ikabili tatizo la ajira na yeye akijifanya kutetea ajira wakati anatumia mgongo huo huo kuchuma au kuona wanaochuma bila kuwalipua,huo si uzalendo,kama Lowassa kashindwa ongelea Richmond na Dowans na Generaltire wakati huu ndiyo wakati wake nikutaka kujiosha kwa mgongo wa chupa.
Mbona Mzalendo Samweli Sitta aligusia swala la Dowans ilikutoa nguvu kwa wanaharakati, yeye hataki kuonesha msimamo wake juu ya wizi alafu anajifanya hapendi wizi na c mwizi,swala la ukosefu wa ajira na elimu mbovu ya makaratasi si laleo nawala hakuwahi kulishupalia kabla akiwa waziri mkuu ,leo anashupalia kuwafungulia mashtaka wanao msema ni kichekesho, analeta mambo ya kina Slvatory ya kusema Raisi hajaongwa suti na watafikiria kuwachukulia hatua waliosema hayo,badala ya kuchukua hatua ndiyo useme kama kweli wewe ni msafi’Tabia ya Kkwete na Lowassa ni tabia zinazoshabihiana,kweli rafiki wa nyoka ni nyoka na ndege wanao fanana huruka pamoja.
Kwa nini tuwe na siasa za kuviziana? Serikali iko serious na lipi? Ndio maana watu wakaacha kushughulika na maendeleo badala yake wakaenda kwa Babu wa Loliondo kutafuta uponyaji huku wakiwaacha madaktari wetu wataalam bila kazi. DECI nayo hivyo hivyo, ikawatapeli watanzania kama alivyofanya BABU.
Ninaungana na Lowasa kuwa watu wanaomchafua ni wanasiasa wanaotumia jina lake wenyewe. Mbona kazi zake alizozifanya zinaononekana. Ni kweli wamuache, ni mchapakazi tena ni makini.SOMA KITABU CHANGU ”KIKOMBE CHA BABU” NA ”ANGUKO KUU TANZANIA”.
KAMA LOWASA NI FISADI. JE,WATANZANIA MMEFANYA NINI NA MITAMBO YA RICHMOND/DOWANS BAADA YA KUJIVUA GAMBA NA KUWA SYMBION POWER OF MAREKANI?
NADHANI MMEELEWA MAANA YANGU. UFISADI MWINGINE NI WA VIONGOZI WETU WAKUU, TUSIMWANGALIE LOWASA KAMA ADUI WA MAENDELEO.
Lowassa anayohaki ya kueleza hisia zake kama anaona hajatendewa haki na mtu yeyote. Kama anahatia na kama ni fisadi kama baadhi yetu tunavyoropoka kwa kufuata mkumbo, kwa nini asipelekwe mahakamani? Kama serikali haijafanya hivyo; hata nyie mnaopayuka payuka ili muonekane mmeshindwa nini kwenda mahakamani? Tumeshagundua ujanja wenu na hao bwana zenu wanaowatuma, hamtaki apelekwe mahakamani maana huko ataonekana hana hatia. Badala yake mnataka muendelee na wimbo usio na chorus Lowassa fisadi, alikuibia mkeo? Pigeni mayowe na hao wanaotaka wapewe urais wa majaribio. Mungu mkubwa na kama Lowassa kaandsikiwa urais, 2015, hakuna wa kumzuia tusubiri tuone.