Wanakijiji wagomea kushiriki miradi ya kijiji wakidai taarifa ya fedha

Jamii Africa

WAKAZI  wa kijiji cha  Machochwe  katika  Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara  wamegoma kushiriki  shughuli  zozote za maendeleo , hadi  hapo  watakaposomewa mapato na matumizi  ya fedha za kijiji chao.

Habari za uhakika  kutoka  ndani ya kata hiyo  zimeliambia  gazeti hili kwa njia ya simu juzi kwamba  wananchi  hao wanamtuhumu   Ofisa Mtendaji wa Kijiji  hicho,  Peter  Hagare, kuwa  hajawahi kuwasomea  mapato na matumizi  kwa  zaidi  ya miaka mitano sasa.

Imeelezwa kwamba Hagare  ambaye  pia ni Kaimu  Ofisa Mtendaji wa Kata ya Machochwe  hataki  kuitisha  mikutano   ya hadhara.

Kwa  mujibu wa habari, mgomo huo ulianza mwanzoni  mwa mwezi huu baada ya makubaliano  yaliyofikiwa   na  wananchi  kupitia  mikutano  mbalimbali  waliyoifanya  kwa kuwashirikisha  wenyeviti wa vitongoji.

Habari  hizo ambazo pia zimethibitishwa na Diwani wa kata hiyo, Chacha Samwel(Chadema), zinadai   kuwa mgomo huo  ni miongoni mwa  hatua chache  ambazo tayari  zimeshachukuliwa na wananchi hao ili  waweze kusomewa mapato na matumizi.

“ Kilichotukasirisha zaidi  ni kitendo cha  Ofisa Mtendaji  huyu  ‘kutafuna’ shilingi 100,000  ambazo alizichukua   kwa lengo la  ufunguzi wa  akaunti ya kijiji  cha  Machochwe, badala yake  hakufanya hivyo; na hivyo  inadhihirisha kwamba  hana mapenzi mema  na maendeleo  ya wananchi”  anasema Chacha  John, kutoka kijiji cha Machochwe.

Anasema Ofisa Mtendaji huyo kila anapoulizwa juu  ya suala hilo, hutoa  visingizo mbalimbali  kwa  lengo la  kukwepa  kukutana na  wanakijiji.

Anaendelea kwa kusema;  “ Hatua  nyingine  ambayo tumeichukua  ni pamoja na kuifunga  ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji  cha Machochwe ili mwajiri wake( Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti) pamoja na Mkuu  wa Wilaya  wafike kwa  ajili ya kusikiliza  kilio chetu”

Imeelezwa kwamba siku nne baada ya wanakijiji kufunga ofisi hiyo, ilifunguliwa  na uongozi wa Wilaya ya Serengeti kwa msaada wa polisi.

“ Matokeo yake ni kwamba  Mkuu  wa Wilaya ya Serengeti, Edward

Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Dk. Kebwe Stephen

Ole  Lenga,  aliyekuwa  amefuatana na  polisi  alifika  kijijini Februali 6  na kuamuru ofisi hiyo ifunguliwe  bila  hata  kusikiliza  malalamiko yetu. Hata  hivyo, bado  tunaendelea  na mgomo wa kutoshiriki  shughuli za maendeleo  hadi  ‘kieleweke”  alisema  mwanakijiji huyo.

Diwani  wa kata hiyo alithibitisha  kuhusu  kuwepo kwa  mgomo huo  na kuongeza kuwa  Afisa  Mtendaji  huyo  amekuwa  kikwazo kikubwa   katika  shughuli mbalimbali za maendeleo.

“  Wakati mwingine   huitisha vikao  vya WDC (vikao  vya Maendeleo  ndani ya Kata) pasipo hata  kunishirikisha” anasisitiza  diwani huyo, Chacha  Samwel  (Chadema).

Chacha anasema  kwamba  zaidi  ya  kugoma kushiriki katika shughuli za maendeleo, wakazi  zaidi ya 200  wa kijiji cha Machochwe  wanashinikiza Ofisa Mtendaji huyo  ahamishwe.

Diwani huyo anasema wanakijiji wanaamini kwamba ofisa huyo  hukingiwa  kifua  na Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri pamoja na Mkuu  wa Wilaya.

Ofisa Mtendaji huyo amethibitisha kuwapo kwa mgomo huo, lakini amemlaumu Diwani Chacha kuwa ndiye anayewachochea wananchi kwa kile alichokieleza kwamba ni kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
“ Ni kweli  kwamba  wanakijiji   wamegoma kushiriki  shughuli za maendeleo; eti waataka nihamishwe  kwa madai  ambayo ata hayana msingi wowote,” anasema Ofisa Mtendaji huyo na kuongeza; “… Hata hivyo, mimi sijakataa  kuhamishwa iwapo  mwajiri wangu  ataridhia.”

Mkurugenzi  Mtendaji wa halmashauri hiyo hakupatikana kwa njia  ya simu ili weze kuzungumzia suala hilo; simu yake haikuwa hewani wakati Mkuu wa Wilaya, Ole Lenga alielekeza suala hilo kwa Mkurugenzi Mtendaji.

“ Suala hilo lipo, lakini  linashughulikiwa na  DED (Mkurugenzi Mtendaji  wa Halmashauri); muulize  atakuambia kinachoendelea  ni nini,” anasema Mkuu  wa wilaya hiyo, Ole Lenga.

Taarifa hii imeandaliwa na  Juma Ng’oko,  aliyekuwa  Serengeti

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *