Hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji ya mwaka 2017/2018 inaeleza kuwa asilimia 86 ya watu wanaoishi mijini na asilimia 72.58 ya vijijini katika Tanzania Bara wanapata maji safi na salama.
Ripoti hii inaonesha wazi kwamba idadi ya watu wanaopata maji ya uhakika na salama katika maeneo ya vijijini ni ya kiwango cha chini ikilinganishwa na ile ya wanaoishi maeneo ya mijini. Hata hivyo, hali halisi inaweza kuwa ni mbaya zaidi ukilinganisha na utendaji wa miundombinu ya maji kwamba inafanya kazi au la.
Takwimu zilizopo katika ripoti ya maendeleo ya sekta ya maji mwaka 2016, zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2010/11 na mwaka 2015/16, Serikali ilipanga kujenga jumla ya vituo vya maji 99,515 lakini ilishia kujenga vituo 42,718 pekee.
Vituo hivyo vilivyojengwa ni asilimia 43 tu ya malengo jambo ambalo linaloonyesha kuwa idadi kubwa ya wananchi waliotakiwa kupata huduma hiyo wameshindwa kupata kwa wakati.
Hali kama hiyo inatokana na matatizo mbalimbali yanayosababishwa na mambo tofauti yakiwemo masuala ya jiografia ya eneo husika, ubora wa maji, wingi wake na msimu ambao maji yanapatikana. Uhaba mkubwa wa miundombinu ya maji, matatizo ya utunzaji wa miundombinu, na kiwango kidogo cha ufahamu wa wakazi juu ya utumiaji wa maji salama pia yanachangia hali kama hiyo.
Kulingana na Utafiti wa taasisi ya Twaweza 2017 unaonyesha kuwa upatikanaji wa maji usio wa uhakika katika maeneo mengi ya vijijini ni matokeo ya umbali na uchache wa vyanzo maji ambapo wananchi hutembea umbali mrefu kuyafuata maji.
Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha usambazaji na umbali wa vyanzo vya maji kwa maeneo ya vijijini ni asilimia 39. Kwa muktadha huo asilimia 61 ya wakazi wa vijijini kutembea umbali mrefu kuyafuata maji.
Mathalani, Wilaya ya Magu ni miongoni maeneo nchini yanayokabiliwa na tatizo la maji kwa muda mrefu ambapo taarifa za Mkoa wa Mwanza zikionyesha ni 53% tu ya wakazi wa mkoa huo wanaopata maji safi lakini hali ni mbaya zaidi wilayani hiyo ambayo wakazi wake wanaishi maeneo ya vijijini.
Kuna mipango mingi ya kibajeti ambayo imekuwepo katika wilaya hiyo lakini haijatekelezwa kwa miaka mingi na kuzidi kuongeza ugumu wa maisha kutokana na kutopatikana kwa urahisi huduma muhimu ya maji.
Mnamo mwezi Machi 2016, Mbunge wa Magu, Bonaventure Kiswaga, alinukuliwa akikiri kuwa tatizo la maji wilayani humo bado ni kubwa, licha ya ahadi mbalimbali za kisiasa kutatua tatizo hilo.
"Dira ya 2025" ya Serikali ya Tanzania inalenga kufikisha kiwango cha upatikanaji wa maji kufikia asilimia 90 kwa maeneo ya vijijini. Lakini mipango na utashi wa kisiasa una nia ya dhati kufikia malengo hayo?
Serikali na mamlaka husika zinakumbushwa kuyatazama maeneo ya vijini ikiwemo Wilaya ya Magu na kutafuta suluhisho la kudumu juu ya tatizo la upatikanaji wa maji ikizingatiwa kuwa rasilimali ya maji ni muhimu kwa maendeleo ya mwanadamu.