Wazazi wamtelekeza mtoto mlemavu wa miaka mitatu

Albano Midelo

MTOTO Anna Mapunda mwenye umri wa miaka mitatu  mkazi wa kijiji cha Mkako wilayani Mbinga mkoani Ruvuma anahitaji msaada wa matibabu katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam baada ya kuzaliwa na ulemavu sehemu ya haja kubwa.

Mtoto huyo anasumbuliwa na tatizo la kutokwa na sehemu ya haja kubwa nje kila anapokwenda kujisaidia na kwamba sehemu hiyo hukaa nje kwa hadi saa tatu kisha huanza kurudi yenyewe taratibu ambapo mtoto huyo hupata maumivu makali.anna na mlezi wakeMtoto Anna Mapunda (miaka mitatu) akiwa na mlezi wake wa sasa Veronika Milanzi ambaye ni katibu ya kanisa la TAG Ruhuwiko Songea

Kutokana na mtoto Anna kuzaliwa na tatizo hilo,baba yake mzazi anadaiwa alikuwa anampiga mtoto huyo kila  sehemu ya haja kubwa inapotoka nje wakati anajisaidia  hatimaye aliamua kumpa talaka mke wake na kwenda kuoa mwanamke mwingine ambapo mama mzazi wa Anna naye aliamua kwenda kuolewa  na mume mwingine katika mji wa Mbambabay mwambao mwa ziwa Nyasa.

Mtoto Anna akiwa na mama yake mzazi tatizo hilo liliendelea kumsumbua mtoto huyo ingawa alimpeleka katika zahanati ya kijiji pamoja na kwenda kwa waganga wa jadi kwa ajili ya kutafuta tiba za jadi ,hata hivyo tatizo liliendelea hali iliyosababisha mama huyo kumtelekeza mtoto wake baada ya kukata tamaa.

Mtoto Anna  mapema mwaka huu  alichukuliwa na shangazi yake ambaye anaishi mjini Songea na kwamba baba mzazi wa mtoto huyo alimwambia dada yake ambaye ni shangazi ya mtoto huyo kuwa amchukue ampeleke hata kwa wachuna ngozi yeye hamtaki kwa madai kuwa ameleta laana katika familia yake.

Shangazi ya mtoto huyo alimchukua mtoto huyo na kuanza kuhangaika ili kutatua tatizo hilo ndipo alimpeleka kwa rafiki  yake katibu ya Tanzania Assemblies Of God TAG kanisa la Ruhuwiko Songea Veronika Milanzi ambaye alikuwa akimpeleka katika kanisa hilo kwa ajili ya kumfanyia maombi kila siku.

“Nilimpompeleka siku ya kwanza kanisani kwa ajili ya kufanyiwa maombi mtoto huyu alikataa kurudi tena kwa shangazi yake tangu wakati huo  hadi sasa  ni karibu mwezi wanne mtoto huyu anaishi na mimi ,shangazi yake amekubali niendelea kuishi naye hadi sasa lakini tatizo lake la kutoka  haja kubwa bado linaendelea’’,alisema

Katibu huyo wa TAG licha ya kumfanyia mtoto maombi kila siku lakini pia alichangishana  fedha na baadhi ya waumini ili  kumpeleka mtoto katika hospitali ya misheni ya Peramiho ambako walimchunguza  na kudai kuwa angekuwa na tatizo la kutoka utumbo wa haja kubwa bila kurudi ndani wangemfanyia upasuaji na kumaliza tatizo hilo na kwamba kwa kuwa utumbo wa haja kubwa wa mtoto huyo unatoka nje anapokwenda haja na kisha unajirudi ndani pole pole hawana uwezo wa kumfanyia upasuaji.

Akizungumzia kitaalamu kuhusu tatizo hilo Dk Henry Mayala anasema magonjwa katika njia ya haja kubwa kitalaamu yanaitwa   bawasiri ambayo ni mojawapo ya tatizo ambalo mara nyingi linapotokea humfanya mtu kuwa na aibu kuelezea au kwenda hospitali ili kupata tiba sahihi.

Dk.Mayala anabainisha kuwa bawasiri au hemorrhoids husababishwa na kuvimba kwa mishipa ya damu aina ya vena katika eneo la mfereji wa haja kubwa na kwamba kuna aina mbili za bawasili ambazo ni bawasili ya nje na ndani

“Bawasili ya nje hutokea katika eneo la mwisho kabisa la mfereji wa haja kubwa, na huweza kuambatana na maumivu, pamoja na kuwashwa kwa ngozi katika eneo hilo. Mara nyingine mishipa hiyo ya damu (vena) hupasuka na damu huganda na kusababisha aina kitaalamu inaitwa Thrombosed hemorrhoid na bawasili ya ndani hutokea ndani ya mfereji wa haja kubwa. Na huwa haimbatani na maumivu na wengi huwa hawatambui kuwa wanatatizo hili’’,alisisitiza.

Kulingana na mtaalamu huyo bawasili  ya ndani  imegawanyika katika madaraja manne ambayo ni daraja la kwanza la ni  kutotoka katika mahali pake pa kawaida,daraja la pili  bawasiri kutoka wakati wa haja kubwa na kurudi yenyewe baada ya tukio hilo,daraja la tatua bawasiri kutoka wakati wa haja kubwa na mtu kuweza kuirudisha mwenyewe baada ya tukio hilo na daraja la nne Bawasiri kutoka wakati wa haja kubwa na vigumu mtu kuirudisha baada ya tukio hilo.

Amezitaja sababu zinazosababisha magonjwa ya haja kubwa kuwa ni pamoja na Tatizo sugu la kuharisha,Kupata kinyesi kigumu Ujauzito,Uzito kupita kiasi (obesity), Ngono ya njia ya haja kubwa (anal sex),Kwa ujumla mambo yanayo ongeza shiniko katika tumbo.• Umri mkubwa.

Milanzi ambaye anataka kumpeleka mtoto huyo katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam au hospitali nyingine ambazo zinaweza kutoa matibabu anatoa rai kwa watu wenye mapenzi mema kumsaidia mtoto huyo gharama za matibabu,usafiri na kujikimu  kwa kuwa yeye haina uwezo.

Iwapo umeguswa na ungependa kutoa ushauri au msaada wa wowote wa kufanikisha matibabu ya mtoto Anna Mapunda andika [email protected], simu+255 766463129

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *