Daraja linalowawasumbua wakazi wa kata ya Subira (Songea) kwa miaka 30

Mariam Mkumbaru

Wakazi wa kata ya Subira katika Manispaa ya Songea  Mkoani Ruvuma,  wako katika hatari ya kusombwa na maji wakati wa kuvuka katika daraJa la kisiwani kitongoji cha Lihwena.

Daraja hilo lilijengwa miaka 30 iliyopita kwa kutumia miti ya muwazi miti ambayo inateleza wakati wa kuvuka na kusababisha wakazi wa kata hiyo kutumbukia ndani ya mto huo wakati wa kuvuka kwenda mashambani, zahanati, kuzika, shuleni na kwenye sherehe.

daraja-2JPG

"Hali ni mbaya sana kipindi cha mvua za masika watu wanatumbukia katika mtoni kwa sababu miti iliyojengewa inateleza sana, mwaka jana watoto wanne walipoteza maisha kwa kutumbukia  ndani ya mto na kusobwa na maji, pia wanaokwenda kuzika wanaangusha jeneza ndani ya mto mara kwa mara," alisema Joseph Komba

Komba alisema kuwa daraja hilo ndio kiunganishi kikubwa kwa wakazi wa kata ya Subira, kwa sababu upande wa pili kuna kanisa na zahanati na upande mwengine kuna makaburi, shule yaa msingi na mashamba ambayo wanalima mazao mbalimbali ya chakula na biashara kama mahindi, maharage na mpunga.

daraja-one

Aidha alisema kuwa kila baaa ya miezi minne wanabadilisha miti hiyo na kuweka miti mingine kwa sababu wakiacha hiyo hiyo daraja linakuwa katika hali mbaya sana na watu hawawezi kuvuka.

Kata ya Subira kwa sasa ina wakazi wpatao 8,700 na wote wanategemea huduma mbalimbali kwa kuvuka katika daraja hilo ambalo uvukaji wake wa hatari sana hasa kwa kipindi hiki cha mvua.

"Tunashindwa kuvuka kwenda kupata matibabu upande wa pili wa kitongoji kwa sababu ya kuhofia kutumbukia na hasa kipindi hiki cha mvua, hata watoto hawendi shuleni kwa kuhofia kutumbukia katika mto huo na kupoteza maisha," alisema Agata Ngonyani.

daraja-three

Tumeshatoa taalifa mara nyingi kwa diwani na uongozi wa wilaya lakini mpaka sasa hakuna mabadiliko juu ya suala hili la daraja katika kata hii ya Subira, hali bado ni mbaya mpaka sasa hata shughuli za kilimo zinasuasua kwa sababu watu wanaogopa kuvuka katika daraja hilo.

"Nina ujauzito wa miezi saba sasa lakini nimekwenda kupima mara moja tu tena kwa kuvushwa na jirani yangu kwa kunishika mkono ili nisitumbukie mtoni, kwa sababu naogopa kuvuka katika daraja hilo nisije nikatumbukia na kupoteza maisha mie na kiumbe kilichopo tumboni au kuvunjia kiuno," alisema Stella Ndunguru

Kwa upande wake mkurugenzi wa wilaya hiyo Beatrice Msomisi alisema kuwa, wanatambua kuwepo kwa tatizo la daraja hilo ambalo ndio kiungo kwa wakazi wa kata Subira na hata wageni wanaokwenda katika kata hiyo, kwa sasa anajipanga kwenda kutengeneza ili kurahisisha maendeleo kwa wakazi hao.

Aidha wakazi hao pia wako hatari kwa kupata magonjwa ya kuambukiza kama kuhara, matumbo na kipindupindu, kwa sababu maji wanayotumia katika matumizi ya kila siku sio safi na salama.

"Hakuna mabomba ya kusambaza maji safi na salama mpaka sasa tunatumia maji ya visima ambayo nayo sio salama na kipindi cha jua kali visima vinakauka na tunakwenda umbali mrefu sana kutafuta maji safi na salama kipindi ambapo visima hivyo vimekauka, wakati mvua nyingi visima vinajaa maji machafu" alisema Agnes.

Tatizo la ubovu wa daraja la kata ya Subira ni tatizo sugu lina miaka 30 mpaka sasa halijapatiwa ufumbuzi na wakazi wa kata hiyo wanazidi kupata shida ya kuvuka kupitia daraja hilo na wangine kupoteza maisha, hali hii mpaka lini? nani anawajibika kutengeneza daraja hili ambalo ni kiungo kikubwa kwa wakazi wapatao 8,700 katika shughuli za kilimo, mazishi, ibada, sherehe, shule na afya.

Maana bila ya kuwa na daraja madhubuti wakazi hawa hawawezi kufanya kazi za maendeleo kwa sababu wako katikati ya kata hiyo na daraja ndio linalowaunganisha kutoka upande mmoja kwenda upande mwengine, wahusika wasiwe na ahadi kama wanasiasa wanavyoomba kura kipindi cha kampeni wanatakiwa kufanyakazi kwa vitendo sio ahadi kwa miaka 30.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *