Inaelezwa kuwa watanzania wako hatarini kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo kansa kutokana na matumizi ya bidhaa bandia zinazozalishwa kwenye viwanda vya ndani na nje ya nchi.
Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI) lilifanya utafiti nchini mwaka 2015/2016 juu ya hali ya bidhaa bandia na kubaini kuwa asilimia 50 ya bidhaa zinazoingia nchini ikiwemo chakula, dawa pamoja vifaa vya ujenzi kutoka nje hazifai kwa matumizi ya binadamu kutokana na kukosa viwango vya ubora.
Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Mzumbe, Prof. Honest Ngowi ambaye alishiriki kwenye utafiti huo alisema waliwahoji watumiaji 250 wa bidhaa mbalimbali pamoja na watengenezaji 47 nchini na kukusanya takwimu mbalimbali ambapo walibaini Tanzania na Kenya ni nchi zinataabika zaidi na bidhaa bandia kutokana na Jiografia ya maeneo yao.
Bidhaa bandia huingia Tanzania kupitia bandari, viwanja vya ndege na mipakani hasa kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Tanga. Asilimia kubwa ya bidhaa hizo hazipitishi kwenye njia halali ambapo wahusika huzikwepa mamlaka zinazohakiki ubora wa bidhaa kabla hazijatumiwa.
“Idadi kubwa ya bidhaa bandia (asilimia 80) zinaingia Tanzania kupitia bandari ya Dar es Salaam na kwa kiasi fulani kupitia Tanga na Mbeya, huku mlango wa Zanzibar nao umefunguka kwa upana”, inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Bidhaa hizo zinazoingia nchini hutengenezwa nchini China na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). Pia zingine zinatengenezwa na viwanda vya ndani. “Kuna vitendo vya kutengeneza bidhaa bandia nchini kwenye sekta mbalimbali katika majiji na miji mikubwa ya Tanzania. Hizi bidhaa hujumuisha vileo, vinywaji, mbolea, mbegu na dawa za binadamu”.
Kati ya mwaka 2010 na 2016, Tume ya Huru ya Ushindani Tanzania (FCC) ilikamata makontena 1,151 yakiwa na bidhaa bandia na kuendesha dolia 138 katika maeneo mbalimbali nchini na kuwakamata washukiwa 1,711 wakiuza bidhaa bandia zenye thamani ya Trilioni 2.8.
FCC inaeleza kuwa maeneo ambayo yamekithiri kwa biadhaa hizo ni Dar es Salaam. Arusha, Mwanza na Mbeya. Kulingana na takwimu zao inakisiwa asilimia 10 ya bidhaa zote nchini ni bandia.
Tatizo la bidhaa bandia limeenea duniani kote ambapo linajukana kama ni uhalifu wa bidhaa kwasababu viwanda na kampuni zinawakosesha watumiaji taarifa muhimu za bidhaa wanazotengeneza na kuuza. Kulingana na Chama cha Wazalishaji bidhaa Marekani (United States’ Grocery Manufacturers Association) udangajifu wa chakula unaathiri asilimia 10 ya bidhaa za chakula zinazouzwa na kuigharimu sekta ya chakula kati ya Dola bilioni 10 na bilioni 15 kwa mwaka.
Ikizingatiwa kuwa bidhaa nyingi bandia zinazopatikana Afrika ni zile zinazotumiwa zaidi kukidhi mahitaji ya kila siku kama chakula, zina uwezekano mkubwa kuchangia ongezeko la viwango vya utapiamlo na kansa katika bara hilo.
Pale wazazi wenye kipato kidogo wanapoamini kuwa wanawanunulia watoto wao maziwa na ikatokea maziwa hayo hayana protini au virutubisho muhimu, athari kwa maendeleo ya watoto huwa ni kubwa zaidi.
Hakuna njia ya moja kwa moja ya kufahamu kwa kiasi gani udanganyifu unaotokea kwenye chakula unachangia udumavu, ambao unaathiri asilimia 34 ya watoto wa Afrika walio na umri chini ya miaka mitano na athari za muda mrefu za maumbile na akili.
Vipo visababishi mbalimbali vinavyochochea bidhaa bandia nchini Tanzania. Kwanza, ni kuongezeka kwa mfumo wa uzalishaji wa bidhaa ambapo una mlolongo mrefu wa usambazaji ambao unatofautiana kwa viwango cha udhibiti na kuibua changamoto ya wapi bidhaa imezalishwa.
Pia wazalishaji wa ndani wanakabiliwa na ushindani mkubwa hasa bei ndogo ya bidhaa toka nje, ambapo mara nyingi zinakuwa na ubora mdogo. Kwahiyo wanaweza kutumia njia zisizo sahihi kupunguza gharama za uzalishaji ili kukabiliana na washindani wao. Pia udhaifu wa mamlaka za kudhibiti viwango na ubora nayo huchangia kutokuwepo kwa mfumo thabiti wa ufuatiliaji ambapo hutengeneza mpenyo kwa bidhaa bandia kuingia sokoni.
Makamu Mwenyekiti wa CTI, Evarist Maembe amesema suala la bidhaa bandia bado ni tatizo kubwa na linahitaji nguvu ya pamoja kupambana na wahusika wa vitendo hivyo vya uhalifu wa bidhaa.
Nani anawajibika?
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Usalama wa Chakula, David Edwards amesema kuwa kila mmoja katika jamii ikiwemo viongozi wa serikali na wananchi wanawajibika kuhakikisha wanapata takwimu sahihi za uzalishaji ili kuzuia bidhaa bandia zinazoingia sokoni.
“Serikali ina uwezo wa kupata takwimu nyingi zinazotengenezwa na viwanda, kuzichambua ili kubaini fursa za kuwepo kwa udanganyifu. Upande wa pili, viwanda vya chakula wafuatilie na kuzingatia usalama na ubora wa chakula kwa mitandao yote ya usambazaji”, amesema Edwards.
Pia mamlaka za kusimamia viwango na ubora kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa bidhaa zote za ndani na zile zinazoingia nchini na kutoruhusu bidhaa hizo kumfikia mtumiaji. Sambamba na hilo elimu zaidi itolewe kwa wananchi ili wawe na maarifa ya msingi kubaini bidhaa bandia na kutoa taarifa kwa mamlaka za viwango.