Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jnsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewaagiza madaktari katika hospitali na vituo vya afya kuwafanyia uchunguzi wa ugonjwa wa kifua kikuu wanafunzi kabla ya kuanza masomo.
Wanafunzi wanaotakiwa kupimwa maambukizi ya ugonjwa huo ambao kitaalamu unajulikana kama Tuberculosis (TB) ni wale ambao wanaandikishwa kusoma katika shule za bweni nchini.
Katika tamko la kuadhimisha Siku ya Kifua Kikuu Duniani, Waziri Ummy amesema ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo ni muhimu watumishi wa afya kuwapima TB wanafunzi wote kabla hawajaanza shule ili kuwakinga wanafunzi wengine ambao hawana maambukizi ya ugonjwa huo.
“Nawaagiza waganga wafawidhi wote wa Hospitali na vituo vya huduma kuhakikisha watoto wote wanaoanza shule za bweni wanafanyiwa uchunguzi wa TB kikamilifu kabla ya kuanza masomo”.
Ameongeza kuwa serikali tayari imezindua dawa mpya za TB za watoto ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO). Dawa hizo mpya ni mseto ulioboreshwa ambapo zimewasili nchini kwa ajili ya matumizi ili kuokoa maisha ya watoto ambao taifa linawajiika kuwalinda na hatari yoyote inayotishia ustawi wa maisha yao.
“Serikali imezindua dawa mpya za TB za watoto ili kuhakikisha inakidhi matakwa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), dawa hizo mpya ni za watoto za mseto (RHZ/RH) ulioboreshwa, tayari zimeshawasili nchini na tumeanza kuzisambaza kwenda mikoani na Halmashauri zote”.
Hata hivyo, serikali inaendelea na utekelezaji wa kampeni ya uhamasishaji na upimaji wa TB kwa wananchi wote hasa wale wanaopatikana kwenye maeneo ya migodi na miji ambako kuna msongamano mkubwa wa watu.
“Serikali na wadau mbalimbali tunaendelea na utekelezaji wa kampeni za uhamasishaji na upimaji wa TB kwa wananchi katika maeneo ya migodi, makazi duni kwenye miji mikubwa, magereza na shule”, amebainisha waziri huyo.
Kwa mujibu wa WHO, mwaka jana pekee kulikuwa na wagonjwa milioni 10.4 ambapo mwaka 2016 watu milioni 1.8 walifariki kutokana na maradhi hayo. Licha ya juhudi za kimataifa kupambana na ugonjwa huo bado TB imebaki kuwa kisababishi kikubwa cha vifo vya watu duniani ambapo kila siku wanafariki watu 4,500.
Takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha wagonjwa wa TB wanaogundulika katika vituo vya kutolea huduma hapa nchini ni asilimia 40 tu na idadi kubwa iliyobaki hugundulika wakati hali ikiwa mbaya. Ugonjwa huo husambaa zaidi kwa njia ya hewa na kila mgonjwa 1 anaweza kuwaambukiza watu zaidi ya 20 kwa mwaka.
Kila mwaka nchini Tanzania, wagonjwa 60,000 hugundulika na TB ambapo wanaofariki kwa maradhi hayo ni 28,000.
Dalili, tiba na kinga ya TB
Dalili za kifua kikuu ni pamoja na kukohoa zaidi ya wiki mbili, kupata homa za mara kwa mara, kutokwa jasho hasa nyakati za usiku, kupungua uzito na kukohoa makohozi yaliyochanganyika na damu.
Njia za kujikinga na ugonjwa huo ni pamoja na kupima na kupata matibabu, kuepuka misongamano ya watu, kuishi katika nyumba yenye hewa ya kutosha, kuziba mdomo wakati wa kukohoa au kupiga chafya, kuepuka shughuli zenye vumbi nyingi kama viwandani na migodini na kufungua madirisha ili kuruhusu hewa ya kutosha kuingia ndani ya nyumba.
Kifua kikuu kinatibika na endapo mtu atagundulika kaambikizwa ugonjwa huo, huduma zake ni bure kuanzia kupima mpaka kupata matibabu.
Machi 24 ya kila mwaka dunia huadhimisha siku ya Kifua Kikuu Duniani ili kutafakari hatua zilizofikiwa kupambana na maambukizi ya ugonjwa huo na kutengeneza mikakati ya kuwalinda wananchi dhidi ya maradhi hayo ambayo huenezwa zaidi kwa njia ya hewa.