Kikwete kuteua Tume ya Katiba Kabla ya Krismasi?

Jamii Africa

Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuteua Tume ya kusimamia mchakato wa Katiba (Tume ya Katiba) ambayo itakusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba na hatimaye kuandika rasimu ya Katiba Mpya kabla rasimu hiyo haijapigiwa kura ya maoni na Watanzania wote. Rais Kikwete anatarajiwa kufanya hivyo baada ya kutia sahihi mswada wa Mapitio ya Katiba wa 2011 siku ya Jumanne kufuatia juhudi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo kushindwa kumshawishi asifanye hivyo ili kutoa muda wa kubadilisha mswada huo.

Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu – ambayo haikuambatanishwa na picha ya kusainiwa huko – Rais Kikwete amefanya hivyo ili kuweza kuanzisha mchakato wa kupata Katiba Mpya ya Tanzania. “Kutiwa saini kwa Muswada huo ili uwe Sheria ni hatua kubwa na muhimu katika safari ya kutungwa kwa Katiba mpya ya Tanzania kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya kwa wananchi Desemba 31, mwaka jana, 2010” imesema taarifa hiyo ya Ikulu iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu.

Katika kuonesha kuwa Ikulu imezingatia mazungumzo ya Rais Kikwete na chama kikuu cha upinzani CDM Ikulu imesema kuwa “Pamoja na kutiwa saini hiyo bado Serikali itaendelea kusikiliza maoni na mawazo ya wadau na wananchi mbalimbali kuhusu namna ya kuboresha sheria hiyo”. Vile vile taarifa hiyo imetoa wito kwa Watanzania wenye maoni mbalimbali juu ya sheria hiyo kuendelea kutoa maoni hayo na kuwa “serikali itasikiliza na kuchukua hatua zipasazo”.

Maoni ya baadhi ya wachunguzi wa mambo ya kisiasa nchini na Watanzania wengine sheria hiyo iliyopitishwa na Rais haina msingi wa Kikatiba kwani inapingana kabisa na Ibara ya 98 ya Katiba ya sasa ambayo hairuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya isipokuwa mchakato wa Kibunge wa kufanyia marekebisho Katiba ya sasa”. Kutokana na hilo baadhi ya watu wanaamini kuwa kuna uwezekano wa mabadiliko makubwa ya sheria hiyo kwenye kikao kijacho cha Bunge kwani ili mchakato wa Katiba Mpya uweze kuwa halali kunahitajika mabadiliko katika Katiba ya sasa kwanza.

“Katiba ya sasa imepuuzwa; hakuna mtu yeyote Tanzania mwenye madaraka ya kuamua kuandika Katiba Mpya wakati katiba ipo na ina mchakato wa kufanyiwa marekebisho mbalimbali chini ya Ibara ya 98” amesema mmoja wa wachambuzi hao – aliyekataa kutajwa jina lake- ambaye ni miongoni mwa wanaharakati wenye kupinga mchakato wa sheria ambao umependekezwa.

Hata hivyo vyanzo mbalimbali vilivyo karibu na Ikulu vimedokeza kuwa kwa vile Sheria imeshapitishwa na ni halali hakuna kinachomzuia Rais Kikwete kuanza kuunda tume ya Katiba kabla ya mkutano ujao wa Bunge. “Ukweli ni kuwa sheria ipo sasa hivi na Rais amepewa madaraka ya kuunda tume na tunatarajia kuwa yumkini kabla ya Krismasi au mara tu  kabla ya mwaka mpya, kutangaza tume ya Katiba Mpya kama zawadi ya kufungia mwaka” amesema afisa mmoja wa Ikulu aliyezungumza na FikraPevu na mwenye ujuzi wa jambo hilo.

Alipoulizwa kwanini Rais asisubiri kuunda tume hadi Bunge likutane na kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na CDM kwenye mkutano wao na Rais afisa huyo ambaye si msemaji wa Ikulu alisema kwamba “mchakato wa Katiba mpya ndio umeanza na kupitishwa Sheria ni jambo la kwanza; jambo linalofuatia ni kuunda tume na kuipatia hadidu rejea na kuanza mchakato rasmi kwa mujibu wa sheria hiyo na hivyo hakuna sababu nyingine ya kuchelewa” na kuongezea kuwa “kama taarifa ya Ikulu ilivyosemwa sheria inaweza kufanyiwa mabadiliko mbalimbali kama sheria nyingine zinazofanyiwa bila kuathiri sana kazi za Tume”.

Hata hivyo alipohojiwa kuwa itakuwaje kama mapendekezo ya sheria yatakayotolewa yanahitaji mabadiliko makubwa katika muundo wa tume na hata madaraka yake kuhojiwa afisa huyo alisema kwa kicheko kidogo “hakuna mabadiliko makubwa ya sheria yatakayofanyika, CCM ndio chenye serikali na CDM au chama kingine kitaweza kuleta maoni yao lakini mwisho wa siku CCM ndio itaamua ni maoni gani yanastahili kuingizwa kwenye sheria; Serikali haitakuwa tayari kuona mabadiliko makubwa yanafanyika na hivyo kupoteza maana ya tume yenyewe” alisema afisa huyo leo jioni.

Hata hivyo, kama kidokezo cha pembeni afisa huyo alisema kuwa endapo Rais Kikwete hatotangaza tume siyo kwa sababu hajui wajumbe wake bali atajaribu kuwapa CDM taswira ya kusikilizwa na hivyo anaweza kusubiri hadi kikao kijacho ambapo CDM wataweza kutoa mapendekezo yao lakini yatazimwa kwa kutumia taratibu za Bunge. “Ujue wakirudi Bungeni watapewa nafasi ya kuwashawishi wabunge wa CCM walioukubali ule mswada; sasa wakishindwa na kura ikiitishwa watakuwa wameshindwa kihalali na hawawezi kulalamika na hawawezi  kukimbia tena Bungeni” alisema.

Na. M. M. Mwanakijiji

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *