Vita ya kibiashara kati ya China na Marekani  yachukua sura mpya. China kuongeza ushuru wa bidhaa

Fadhili Mpunji

Siku chache baada ya Marekani kutangaza kuwa itatoza ushuru wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 60, serikali ya China imejibu kwa kutoa masharti mapya kwa bidhaa zinazotoka Marekani kuingia nchini humo.

Serikali ya China imejibu kwa kutoa orodha ya bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 50 zinazoagizwa kutoka Marekani ambazo zitaongezewa ushuru, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na uamuzi wa Serikali ya Marekani.

Serikali ya Marekani inadai kuchukua hatua ya kutoza ushuru bidhaa kutoka China, ili kurekebisha urari wa biashara kati yake na China, ambao umekuwa unainufaisha zaidi China kuliko Marekani. Licha ya kuwa Marekani ina haki ya kuchukua hatua kama hiyo kwa mujibu wa sheria zake, hatua hiyo ni kinyume na utaratibu na kanuni za Shirika la biashara Duniani  (WTO).

Wakati Marekani ilipotangaza uamuzi wake, China ilisema kuwa kama nchi hiyo ikitekeleza azma yake, haitakaa kimya. Wizara ya Fedha ya China imeandika kwenye tovuti yake kuwa, idara ya Ushuru wa Forodha ya China imeamua kuweka ushuru zaidi wa asilimia 25 kwa bidhaa 106 zilizo chini ya vifungu 14.

                            Soya kutoka Marekani itatozwa ushuru ingia China

 

Baadhi ya bidhaa zitakazotozwa ushuru ni pamoja na bidhaa za kilimo yakiwemo maharage ya soya, magari na bidhaa mbalimbali za kemikali. Thamani ya jumla ya ushuru utakaotozwa kwa bidhaa za kutoka Marekani utafikia dola bilioni 50.

Naibu Waziri wa Biashara wa China, Wang Shoucheng amesema hatua ya Marekani kuongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa za China umekiuka wajibu wa kimataifa, lakini China itatumia Sheria zake kujibu maamuzi hayo ya Marekani kwa njia mbalimbali.

Hata hivyo, habari zimeanza kujulikana kuhusu malalamiko ya baadhi ya wakulima wa China kuhusu baadhi ya vitendo vya Marekani kwamba vinaathiri soko la kimataifa la mazao yao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Fedha wa China, Zhu Guangyao amesema China imeweka Soya kutoka Marekani katika orodha hiyo kutokana na matakwa ya wakulima wa China.

“China inaagiza asilimia 60 ya Soya ya Marekani inayouzwa nje. Wakulima wa China waliishtaki Marekani kutoa ruzuku kwa wakulima wake wa Soya, kitendo hicho kiliathiri maslahi ya wakulima wa China. Lakini hadi sasa orodha ya China haijatekelezwa, sasa ni wakati wa kufanya mazungumzo.” Amesema Guangyao.

Kumekuwa na mtazamo kuwa, hatua hiyo ya Marekani huenda inailenga China kwa makusudi, kwa kuwa baadhi ya bidhaa za China zilizoongezewa ushuru zinaweza kununuliwa kutoka nchi nyingine bila ushuru huo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *