Kwanini kukaa muda mrefu kunasababisha kuganda kwa damu kuliko ukiwa umelala?

Jamii Africa

Unaweza kuwa umegundua kuwa ukikaa sehemu moja bila kubadilisha mkao hata kwa saa moja, miguu yako itaanza kupatwa na hali isiyo ya kawaida. Wengine wanaweza kuhisi mshtuko fulani wa kutekenywa, maumivu au ganzi, lakini wengine wanafikia hatua ya kutoweza kusogeza miguu kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Na wengine wanapooza miguuni kwa muda mfupi.

Dalili hizi hujidhihirisha kwa mtu ikiwa atakaa sehemu moja muda mrefu kwa muda usiopungua saa moja.

Kwa upande mwingine, tunapolala huwa tunajinyoosha miguu yetu kwenye kitanda kwa saa 6 hadi 7. Lakini hatuhisi hali yoyote ya kutuumiza au dalili kama tulizoziona wakati tumekaa.

Kukaa kwa muda mrefu kunaweza kusababisha hali isiyo ya kawaida na wakati mwingine damu kuganda (boold clots) ndani ya mwili. Lakini ukiwa umelala huwezi kuhisi hali hiyo ikitokea kwenye mwili. Kwanini iko hivyo?

 Jinsi damu inavyozunguka

Kama tunavyofahamu, moyo ni kiungo au ogani muhimu inayohusika na mzunguko wa damu mwilini. Damu inaanza safari yake kwenye moyo; baada ya kutoka kwenye moyo, damu inaingia kwenye mshipa mkubwa (aota) na kusambazwa sehemu zingine za mwili kupitia mishipa midogo midogo (arteries).

Baada ya damu kuingia kwenye mishipa midogo midogo, hurudishwa tena kwenye mapafu na moyo kwa kupitia mfumo wa mishipa ya vena (venous system).

Mishipa ya vena ina matundu madogo ambayo yanasaidia damu kutorudi nyuma wakati ikisafiri kuelekea kwenye moyo. Kwa msingi huo inapambana na nguvu ya mvutano ambayo inazuia damu isisambae au kusafiri kutoka kwenye miguu hadi kwenye moyo.

Wakati mtu amekaa sehemu moja kwa muda mrefu, damu haiwezi kusafiri haraka kama inavyotakiwa. Hali hiyo huchochea mgando kwenye mwili ambapo matokeo yake ni kuganda kwa damu.

 

Ukiwa umelala…

Ukiwa umelala kitandani, kwa kiasi fulani miguu yako inakuwa imenyooka ukilinganisha na unapokuwa umekaa, na ni rahisi kuisogeza. Kwasababu hii, damu haitalazimika kufanya kazi kubwa ya kushindana na nguvu ya mvutano ili kufika kwenye mapafu na moyo. Matokeo yake damu inasafiri kwa urahisi.

Wakati umelala kwa kiasi kikubwa viungo vya mwili vinakuwa vimetulia, na hali hiyo haiwezi kusababisha tatizo la mzunguko wa damu kwasababu mwili umenyooka na damu hailazimika kusafiri kwenda juu.

Hata hivyo, haimanishi kuwa ukilala unakuwa salama dhidi ya kuganda kwa damu. Hata ukijilaza, mvutano bado una umuhimu katika mzunguko wa damu. Ukijilaza, nguvu ya mvutano inainuliwa kidogo na kupunguza tatizo la kuganda kwa damu kwa saa 8 hadi 15.

Kwa msingi huo, ukijilaza kitandani  bila kugeuka geuka kwa saa 20 au zaidi, unaweza kupata matatizo. Ndio maana madaktari wanakuwa makini hasa kwa wagonjwa wanaolala muda mrefu, jambo wanalolifanya ni kuwageuza mara kwa mara ili kuhakikisha damu haigandi na kuudhuru mwili.

 

Ukiwa umekaa…

Ukiwa umekaa sehemu moja hasa wakati unasafiri kwenye treni, basi au ndege kwa muda mrefu inasababisha shughuli za misuli ya mwili kupungua.

Kwa mkao huo, miguu pia haisogei na muda mwingi hukaa kwenye mwelekeo mmoja. Wakati huohuo damu inakosa nguvu ya kupambana na nguvu ya mvutano. Kutokana na mchakato fulani wa kibailojia, mzunguko wa damu kwenda juu  unapungua. Hali hii kwa kiasi kikubwa inasababisha kuganda kwa damu kwenye mwili na matokeo yake mtu hujisikia kupata ganzi au namna fulani ya kupooza.

Damu iliyoganda ikisafiri kwenye mishipa na kufika kwenye mapafu, inaweza kuleta madhara mbalimbali ikiwemo matatizo ya mfumo wa upumuaji (Pulmonary Embolism).

Ndio maana inashauriwa kusimama na kutembea mara kwa mara wakati ukiwa safarini hasa kwenye safari ndefu au ukiwa kwenye shughuli zinazokufanya ukae muda mrefu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *