WANANCHI wa Jimbo la Ilemela jijini Mwanza, wamelalamikia manyanyaso wanayopewa na askari polisi wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, na kumuomba mbunge wao, Highness Samson Kiwia (CHADEMA), kufikisha kilio chao hicho kwa Mkuu wa polisi nchini (IGP), Said Ali Mwema.
Wamesema, wamekuwa wakionewa na kunyanyaswa na askari polisi kwa kupigwa bila makosa yoyote, na kwamba wanafanyiwa unyama huo kama wakimbizi ndani ya nchi yao, jambo ambalo walimuomba mbunge wao kulishughulikia tatizo hilo ili wakae kwa amani na utulivu, badala ya polisi kuharibu amani iliyopo.
Malalamiko hayo yalitolewa jana wakati mbunge Highness alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kayenze Kata ya Bugogwa, ambapo alielezwa kwamba, manyanyaso na mateso hayo wamekuwa wakiyapata kutoka kwa baadhi ya askari polisi wa Kituo cha Sangabuye.
Wananchi hao walisema, kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipata mateso hayo bila sababu zozote kutoka kwa askari polisi hao wa kituo kidogo cha Kayenze, na kwamba ni vema mbunge wao akawashughulikia askari hao ikiwa ni pamoja na kufikisha kilio chao hicho kwa IGP Mwema.
Mmoja wa waathirika wa mateso hayo, aliyejitambulisha kwa jina la Diana Epafa, alidai mkutanoni hapo kwamba, hivi karibuni alivamiwa njiani na askari mmoja wa kituo hicho cha Sangabuye kisha kumshambulia kwa makofi bila sababu.
“Mheshimiwa mbunge, tumekuwa watumwa wa polisi wa Kayenze. Tunapigwa ovyo…mfano ni mimi Diana Epafa nilivamiwa na askari polisi njiani saa moja jioni akaanza kunipiga bila kosa.
“Baada ya kupigwa, nilikimbilia kituo cha polisi lakini sikumkuta OCS, na nikaelekezwa kwamba OCS yupo kwenye baa. Nilipomfuata huko baani na yeye alinitishia kunipiga, ikabidi niondoke. Hivi polisi wapo kwa ajili ya kutulinda sisi na mali zetu au wapo kwa ajili ya kutupiga?. Mheshimiwa Mbunge tusaidie”.
Hata hivyo, wananchi wengine walilalamikia kitendo cha jeshi la polisi wilayani Ilemela cha kukamata ovyo na kuwabambikia kesi za unyang’anyi na uvuvi haramu, na kwamba hufanyiwa hivyo pale mtu anapoombwa rushwa ya fedha akakataa kutoa.
Badaa ya kupokea malalamiko hayo, mbunge huyo wa Ilemela alimtaka Mkuu wa kituo kidogo cha polisi Kayenze (OCS), Stafu Sajenti Julius Egwaga, kujibu tuhuma hizo, alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa Diana Epafa, na kusema hakuwahi kuyashughulikia tangu ayapate mwaka jana.
“Ni kweli siku moja usiku Diana Epafa alikuja kuripoti kwangu tukio la kupigwa na askari, lakini hajarudi tena kufuatilia malalamiko hayo tangu mwaka jana.
“Anasema alikuja akanikosa kituoni akanifuata baani, hivi kweli mheshimiwa mbunge, mimi kama binadamu ni kosa kunywa angalau bia moja?”, alisema OCS huyo wa kituo kidogo cha polisi Kayenze.
Kwa upande wake, mbunge Highness aliwaonya askari polisi kuacha mara moja hulka ya kuwanyanyasa na kuwabambikia kesi wananchi wasio na makosa, na kwamba vitendo hivyo hatavivumilia hata kidogo, badala yake atalazimika kufuata taratibu nyingine ili kukomesha kabisa manyanyaso hayo.
Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma – Mwanza