Watumishi wa afya 200 kupatiwa mafunzo ya utoaji dawa ya usingizi kuokoa maisha wajawazito

Jamii Africa

Kufuatia upungufu wa wataalamu wa dawa za usingizi (anaesthesia), serikali itatoa mafunzo ya dawa za usingizi kwa watumishi wa afya 200 katika vituo vya afya vya upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito.

Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miezi 6 baada ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kutangaza kuanza kutoa shahada ya dawa ya usingizi (Bsc. Anaesthesia Nursing).

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano serikalini cha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa sambamba na uboreshaji wa huduma ya upasuaji wa dharura kwa wajawazito ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto ambao hufariki kwa kosa huduma muhimu za uzazi kwenye vituo vya afya.

“Mkakati wa kuhakikisha huduma za afya kwa akina mama wajawazito zinakuwa salama na uhakika kwa kuandaa rasilimali watu, miundombinu ya majengo na vifaa vitakavyowezesha huduma hizi ikiwemo upasuaji wa dharura kwa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, vifo 556 vitokanavyo na uzazi kwa kila viumbe hai 100,000 huripotiwa kila mwaka katika maeneo mbalimbali nchini. Maana yake ni kwamba watoto na wajawazito hufariki hasa wakati wa mama akijifungua.

Aidha, serikali itaboresha vituo vya afya 288 vya serikali vilivyopo nchini ili kuviwezesha kutoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa wajawazito ambapo waaguzi katika vituo hivyo watapatiwa mafunzo ya dawa za usingizi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga.

Utekelezaji wa mafunzo hayo ni matokeo ya ushirikiano wa Wizara ya Afya na Mfuko wa Pamoja wa Afya ambapo zaidi ya sh1,079 bilioni zimepatikana kufakisha mafunzo hayo ya dawa ya usingizi kwa wauguzi na matabibu waliopo kwenye vtuo vya afya nchini.

“Fedha hizo zitasomesha watumishi wapatao 200, kati ya watumishi hao 100 watapata mafunzo yao katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na MOI, watumishi 50 watafanya mafunzo katika hospitali ya KCMC, na 50 watafanya mafunzo hayo kwenye hospitali ya Bugando,” imefafanua taarifa ya wizara.

Lengo la serikali ni kuhakikisha ifikapo 2019 na kabla ya 2020 vituo vyote vya afya vinavyomilikiwa na serikali vinakuwa na watumishi maalum wa kutoa huduma ya dawa ya usingizi kwaajili ya wapasuaji wasiopungua wawili kwa kila kituo.

Mafunzo hayo ya mwaka mmoja ni mpito wakati serikali ikiendelea kukamilisha taratibu za kurasimisha utoaji wa shahada ya kwanza ya kutoa dawa ya usingizi katika Chuo cha MUHAS katka mwaka huu wa 2018/2019.

Hali halisi ya huduma ya dawa za usingizi nchini
Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kuna upungufu mkubwa wa madaktari wenye utaalamu wa kutoa dawa ya usingizi hasa wakati wa huduma ya upasuaji ambapo kwa sasa waliopo ni asilimia 1.2 tu ya mahitaji yote.

Ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya huduma hiyo wanahitajika madaktari 2000, lakini waliopo sasa ni madaktari 30 pekee.

Kufuatia changamoto hiyo Januari 31, mwaka huu wadau mbalimbali wa afya na elimu walikutana na kujadili namna ya kuondoa changamoto hiyo na kupendekeza mtaala utakaotumika kufundishia kozi ya Aesthesia kabla ya kuupeleka kwa Tume ya Vyuo Vikuu Nchini (TCU).

” Ni kweli kumekuwepo kwa changamoto hiyo ya watalaamu wa dawa hizo lakini sasa mpango huu ukikamilika maana yake tutaongeza idadi ya madaktari kamili maana hawa waliopo wengi ni wale ambao wamesoma kozi kwa mwaka mmoja au miwili.

” Mafunzo yakianza kutolewa hapa chuoni Muhimbili wataweza kuchukua wanafunzi 200, Bugando 50 na KCMC 50 jambo ambalo litaongeza idadi kubwa ya watalaamu ili kuweza kufikia lengo letu la kuwa na wataalamu 2000 nchi nzima,” alinukuliwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Mpoki Ulisubisya.

2 Comments
  • Inapendeza Sana Kama serikali na wizara ya Afya kufanya juhudi hizi za kuweza kutoa mafunzo hayo ili kuweza kuokoa maisha ya mama na mtoto hasa wakati wa kujifungua,
    swali langu ni kwamba wametoa majina ya watumishi hao wanaotakiwa kupata mafunzo hayo na vyuo husika ambazo zinatoa kozi hyo lakin hawajasema kuwa majina haya yaende chuo flan either bugando au kcmc, sasa mtu ataenda kuripoti chuo kip ili hali wametoa na tarehe ya kuripoti??

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *