NYANI wanaoishi katika milima wa Balili, Bunda mkoani Mara, sasa wamefikia hatua ya kusaka vyakula vya wagonjwa wanaolazwa kwenye wodi za Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda. Hayo yalibainika wiki iliyopita, wakati Fikra Pevu lilipoamua kutembelea hospitalini hapo baada ya kupata taarifa kwamba wanyama aina ya nyani wameanza kuwa kero na wakati mwingine kusababisha hasara pamoja na hofu miongoni mwa wagonjwa katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda..
“ Mimi nilipigwa kofi na nyani; na kisha nikanyang’anywa mkate” alidai mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Rita Ikandalo ambaye alisema alikuwa hospitalini kwa siku kadhaa, kwa ajili ya kumuhudumia mgonjwa mmoja (jina linahifadhiwa)ambaye ni ndugu yake.
Ikandilo alisema kasheshe hilo lilitokea Desemba 16 mwaka huu, majira ya saa 3 asubuhi, baada ya kundi la nyani kuingia wodini.
“ … katika tukio hilo nyani alinipiga kofi na kufanikiwa kuchukua chakula. Hata hivyo alipasua chupa yangu ya chai” alidai mwanamke mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Wegesa Chacha(miaka 53).
Wegesa alisema wakati huo yeye alikuwa nje ya wodi akipumzika na kwamba baadaye nyani hao walitokomea mlimani.
Alisema hiyo ni mara ya kwamba kukumbwa na mkasa huo na hali hiyo imezua hofu miongoni mwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo.
“ Tukio hilo lipo; lakini usinitaje kwa sababu mimi siyo msemaji wa hospitali” alisema mmoja wa Wauguzi katika Hospitali hiyo.
Alisema mara kadhaa nyani huonekana kuzagaa ndani ya uzio wa hospitali ingawa hawajawahi kusikia kuwa wamesababisha madhara kwa wagonjwa.
Daktari Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Said Kalamba hakupatikana ofisini kwake. Ilidaiwa kuwa alikuwa nje ya ofisi kikazi.
Hata hivyo, kwa nyakati tofauti tangu juzi simu ya Kalamba ilikuwa ikiita pasipo kupokelewa.
Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda iko pembezoni mwa mlima Balili; ndani ya eneo la Mamlaka ya Mjimdogo wa Bunda.
Mwisho.