Musoma wagoma kuuza mafuta, vituo vyafungwa, lita moja yauzwa sh. 10,000/-

Jamii Africa

MJI wa Musoma mkoani Mara, umekumbwa na ukosefu wa nishati ya mafuta, hasa aina ya Petroli na mafuta ya taa, na kwamba hali hiyo imelazimika kufungwa kwa vituo kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo muhimu.

Bei ya mafuta kwa sasa mjini hapo yanauzwa kati ya sh.7,000 hadi sh. 10,000 kwa lita moja, ambapo imemlazimu mbunge wa jimbo la Musoma mjini, Vincent Nyerere (CHADEMA), kufanya ziara ya ghafla na kujionea hali halisi ya ukosefu wa bidhaa hiyo ya mafuta.

Kero ya upatikanaji wa nishati mafuta ya Petroli Tanzania mwaka 2011 (Picha toka maktaba)

Habari kutoka Musoma zinaeleza kwamba, baadhi ya viongozi waliohojiwa na mbunge katika ziara yake hiyo ya ghafla, walisema kuwa mafuta yamewaishia tangu siku ya Jumatano, na wengine siku ya alhamisi na kudai kuwa bidhaa hiyo itapatikiana kuanzia Jumanne mwaka ujao wa 2012 kutokana na ukosefu katika maghala wanayochukulia.

Meneja wa kituo cha kampuni ya White, Said Fundikira alisema kuwa wao huagiza mafuta jijini Mwanza katika kituo cha GAPCO, na kudai kuwa wamewaasiliana kwa njia ya simu na kuambiwa kuwa anaweza kupata mafuta siku ya jumanne au jumatano wiki ijayo.

“Najitahidi tuone tunanusuru upungufu huu lakini jitihada zinagonga mwamba. Maana tumeshaambiwa hadi mwakani na hakuna jinsi tunasubiria hadi watakapotuletea na akiba yetu imeisha jana (juzi),”alisema Fundikira.

Naye mkurugenzi wa kituo cha Kiraba Kampani, Shamsa Kiraba aliiomba EWURA kujipanga na kujidhatiti ili kuona hali haiwi mbaya nchini kutokana na ukosefu huo wa mafuta, ambao unaendelea sehemu mbalimbali nchini na kusababisha kushuka kwa uchumi wa nchi na maisha kupanda.

“EWURA ijipange vizuri na kuona ni jinsi gani wanaweza kutatua tatizo hilo kubwa la uhaba wa mafuta nchini lakini ingiwa kuna tuhuma nyingi zinaelekezwa kwetu sisi wauzaji. Lakini nasema katika kituo chetu sisi hata kama bei wa bidhaa tumenunua kwa bei ya juu na siku ya pili bei inashuka hatujali tunauza kwa bei hiyo mpya elekezi na sio kuficha mafuta,” alisema Kiraba.

Kwa mujibu wa habari hizo, pia ziara hiyo ya mbunge ilifika hadi kwa baadhi ya watumiaji wakubwa wa bidhaa hiyo waendesha pikipiki maarufu bodaboda katika kituo cha Nyasho ambapo hawakusita kueleza hasira zao na kupaza sauti kwa wauzaji wa mafuta mjini hapo kilichosababisha pikipiki kubakia tatu badala ya 27.

Mmoja wa dereva wa bodaboda, Bakari Bega alisema kuwa wanapata usumbufu mkubwa kutoka kwa wauzaji hao kwani wanatumia mwanya huo wa upungufu wa mafuta kuuza kwa bei ya juu hasa kuwapa kuwapa walanguzi na kuuza kwa bei ya juu.

“Hapa kwanza kazi hakuna hata pesa imeshakosekana kwetu pamoja na  hilo tunaomba serikali ya Manispaa ya Musoma ikakague baadhi ya vituo vya mafuta watakuta kuna mafuta yapo ila ndio hivyo wanataka kupata faida kubwa kwani jioni wanafungua kwa wizi na kuuza bei ya s. 3,000 kwa lita,”alisema Bega.

Madereva hao walimwambia mbunge Nyerere kwamba: “Kituo cha Petrolux kinauza mafuta kinyemela, twende mheshimiwa ukaone”.

Mbunge wa Musoma mjini, Nyerere aliifahamisha FikraPevu leo kwa njia ya simu kwamba, wameagiza wataalamu kuvikagua vituo vyote vya mafuta mjini humo, na kwamba kituo kitakachokutwa na mafuta kitafungiwa kwa mujibu wa sheria.

“Tayari wataalamu wameshaanza zoezi la kukagua mafuta kwa kila kituo hapa Musoma. Kama tutakuta mafuta yapo na wamesema yameisha, hatua kali zitachukuliwa pamoja na kufungiwa vituo vyao”, alionya mbunge huyo kijana.

Habari hii imeandikwa na Sitta Tumma, Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *