Usafiri wa treni Dar na maafa yanayonukia

Jamii Africa

NI majira ya saa 11:15 jioni wakati FikraPevu inapowasili katika stesheni kuu jijini Dar es Salaam ili kupata usafiri wa kuelekea Gongo la Mboto.

Hali iliyopo katika kituo hicho inatisha kutokana na umati mkubwa wa wasafiri huo wa garimoshi zinazofanya safari fupi katika Jiji la Dar es Salaam.

Umati huo unadhihirisha wazi kwamba usafiri wa garimoshi umekuwa mkombozi kwa walio wengi katika kuwafikisha maeneo ya katikati ya jiji hilo – wanafunzi kwa wafanyakazi, ambao siku za nyuma walikuwa wakichelewa kwenda shule na kazini kutokana na adha ya msongamano wa magari barabarani.

Kila abiria aliyeingia stesheni anayo tiketi yake, kwani watendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) huwakatia tiketi nje ya kituo huku wakiwagombea abiria, pengine kila mmoja akitaka kuonyesha makusanyo mengi ya mauzo.

Muda si mrefu honi ya garimoshi inasikika kuashiria kwamba linawasili stesheni na mara linatokea, kwa bahati nzuri ni lile la kuelekea Pugu na siyo la kuelekea Ubungo.

Bila ya kujali kuwa ajali zinaweza kutokea, utingo wa gari moshi hilo wanaacha milango wazi kabla garimoshi halijasimama.

Katika hali ya kushangaza, abiria wanaanza kudandia kwa kusukumana na kuning’inia kabla garimoshi halijasimama.

Wazee, watoto na abiria wengine wasio na uwezo wa kugombea wanaonekana wamesimama ama kusukumwa pembeni na ‘wenye nguvu’.

Kinachowashinda wengi ni kupita madirishani kama ilivyokuwa kwenye usafiri wa daladala miaka kadhaa iliyopita, pengine kutokana na madirisha ya treni kuwa juu zaidi.

kero treniAbiria wakigombea kuingia kwenye treni (Picha kwa hisani ya Kamanda wa Matukio Daima Blog)

“Jamani si watauana sasa! Hivi wakidondoka kwenye mataruma wakati treni halijasimama hali itakuwaje?” anahoji mmoja wa abiria ambaye ameamua kusimama pembeni kidogo kuwapisha wengine wagombee.

Abiria huyo anabainisha kwamba, kwa jinsi hali ilivyo sasa, hakuna tofauti na kile walichokikimbia kwenye daladala ambako walikuwa wakilazimika kupita madirishani ama kwenda kugeuza na magari kukwepa usumbufu, hivyo kulipa nauli mbili kwa safari moja.

“Inahitaji uwe na nguvu ili kupenya, vinginevyo unaweza usipate usafiri na kupata tena treni kwa wakati mwingine inaweza kuwa vigumu kwa vile usafiri hautabiriki, mara nyingine linafanya safari mbili na wakati mwingine linaweza lisirudi kupakia,” anasema abiria huyo ambaye hataki kutaja jina lake.

Wakati linaposimama, tayari mabehewa yote yamejaa huku wengine wakiendelea wakiendelea kugombea.

Ndani ya mabehewa yenyewe hali ni mbaya kutokana na msongamano mkubwa huku hewa nzito ndiyo ikitanda.

FikraPevu inafahamu kwamba, hali ya kudandia usafiri imezoeleka zaidi kwenye daladala hasa ziendazo pembeni mwa mji kama Mbagala, Gongo la Mboto na Mbezi, lakini hili la kudandia garimoshi kabla halijasimama linaonekana kuwa geni.

Hali ya sasa kwenye usafiri huo wa garimoshi imeonekana kuwa ya hatari kwa usalama wa abiria na inaelezwa kwamba inaweza kuleta maafa makubwa siku zijazo ikiwa hatua za makusudi hazitachukuliwa.

treni dar

“Kwanza hili la kudandia, ni hatari kubwa, unaweza kuteleza na kupoteza maisha, lakini msukumano unaotokea kwa abiria wenyewe ni hatari nyingine kwa sababu watu wengi wanaweza hata kuangukia kwenye reli na kukanyagwa,” anasema aliyejitambulisha kwa jina moja la Jonas.

Jonas anasema, tatizo jingine ni msongamano mkubwa kwenye mabehewa kiasi cha watu kukosa hewa nzuri, hali inayoweza kuwafanya abiria wakazimia au hata kupoteza maisha.

Treni ya kwenda Pugu kwa sasa inaelezwa kuwa na mabehewa 16 baada ya kuyapunguza kutoka 32 ya awali, ambapo uwezo wa behewa moja ni kubeba abiria 80 tu, ingawa kwa sasa, hasa nyakazi za asubuhi na jioni, behewa linaweza kubeba abiria hadi 200, jambo ambalo ni la hatari kiusalama.

“Tuko abiria wa kila aina, wapo wenye magonjwa ya kuambukiza kwa njia ya hewa jambo ambalo ni la hatari kwa usalama wa afya za wengine hasa kama hakuna nafasi ya kutosha, wengine wana presha au pumu na wanapobanwa wanaweza kukosa hewa na kupoteza maisha,” anasema.

FikraPevu imebaini kwamba, hali hiyo ya msongamano na kugombea usafiri wa treni inawanyima fursa watu wa makundi muhimu kama wazee, watoto na walemavu ambao hawawezi kupanda ngazi ndefu na zinazoteleza, achilia mbali kudandia.

Uchunguzi huo wa FikraPevu umebaini kutokuwepo kwa muda maalum wa garimoshi hilo kuanza safari ambapo wakati mwingine huchelewa hadi saa moja hasa safari za pili kwenda na kutoka mjini.

Ofisa Uhusiano wa TRL, Mapondela Mohamed, akifafanua kuhusu changamoto hizo aliiambia FikraPevu kwamba, haoni tatizo la abiria kudandia na kwamba TRL haina uwezo wa kuwazuia abiria wasidandie kwa kuwa ngazi za kupandia ziko nje.

“Ngazi za kupandia ziko nje, abiria wanadandia kabla garimoshi halijasimama ni kweli, lakini hata kama utafunga milango haitasaidia, tena ni bora milango iwe wazi ili wakidandia waingie kuliko kuifunga,” alisema Mohamed.

Kuhusiana na utaratibu wa kujali makundi yakiwemo ya walemavu, Mohamed alisema hakuna namna yoyote na akajibu kwa kifupi; “Mbona hata mtoa matangazo wa garimoshi ni mlemavu pia?”

Uamuzi wa serikali kupitia TRL kuanzisha usafiri wa garimoshi kwa safari za katikati ya Jiji la Dar es Salaam unaelezwa kwamba ulikuwa wa manufaa makubwa kutokana na kupunguza msongamano mkubwa wa daladala katika barabara za jiji hilo, ambao kwa miaka kadhaa siyo tu umeleta adha, bali umevuruga hata uchumi kutokana na watu kuchelewa kwenye shughuli mbalimbali.

Hata hivyo, changamoto zinazojitokeza sasa zinaonekana kuwa kikwazo kingine hasa kutokana na kuhatarisha usalama wa abiria, jambo ambalo serikali inapaswa kulishughulikia.

Uzinduzi wa usafiri wa njia ya reli jijini Dar es Salaam ulifanyika Septemba 10, 2012 na safari zilianza rasmi Oktoba 22, 2012 kwa treni la kutoka Ubungo hadi Stesheni.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *