Kutoka Guta mpaka Nyabehu, Bunda…

Stella Mwaikusa

Mimi na waandishi wenzangu, tulitembelea  katika kijiji cha Guta,  Kinyambwiga na Nyabehu, vijiji  vinavyopatikana katika kata ya Guta wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Tulishuhudia mambo ya kufurahisha na mengine yalitupa maswali, lakini kwa ujumla tuliifurahia safari, kati ya mambo tuliyoyaona ni kuwakuta akina mama wakichunga kundi kubwa la ng’ombe na mbuzi kitu ambacho si cha kawaida sana katika jamii nyingi za kitanzania.

mama-akichunga

Kitu kingine tulichokishuhudia ni kuona mtoto wa kiume wa miaka minne akichunga kundi la ng’ombe wanaokadirwa kuwa hamsini mpaka sitini, na tulipojaribu kumuuliza anawezaje kulidhibiti kundi lile,  haikuwa rahisi kwetu kwani hatukuweza kuongea lugha ya kikurya ambayo ndiyo pekee anayoifahamu.

mtoto-akichunga

Lakini baada ya kuona mwandishi mwingine akishuka kwenye gari mtoto alikimbia na kuwaacha ngombe wakizagaa, hali ambayo ilitushangaza kwani hatukujua sababu iliyomkimbiza na tukaamua kuondoka.

Tukiwa tunaendelea na safari ya kuelekea kijiji cha Nyabehu kitongoji cha Nyantare, tulisimamisha gari ili kuwauliza wenyeji ambao walikuwa nje ya nyumba yao iliyozungushiwa wigo wa katani na miti ya miiba, hali ambayo haikuwa rahisi kwetu kuingia ndani ya wigo huo.

Dereva akajaribu kuita ili aweze kuzungumza nao, lakini ghafla wasichana wawili wanaokadiriwa kuwa na miaka 13-15 pamoja na mtoto wa kiume anayekadiriwa kuwa na miaka sita hivi, wote watatu wakakakimbilia ndani ya nyumba yao.

Tukaanza kujiuliza kwa nini hali ile ya watoto kukimbia inajirudia tena, lakini tukiwa katika hali ya kujiuliza, ghafla akajitokeza mama kutoka ndani na akasikiliza shida yetu, akutuelekeza, na tulipotaka kujua kwa nini watoto walikimbilia ndani ndipo tukapata kisa.

“Huku kwetu kuna vikundi vinavyofanya mauaji vinaitwa makirikiri ndiyo maana watoto wakiona gari linasimama maeneo ya huku kwetu wanahisi huenda ndio hao” anaeleza.

Tukaifahamu sababu ya kukimbia  kwa yule mtoto aliyekuwa akichunga, kwani hata tulipokuwa tunarudi tulijaribu kusimaisha gari ili kumsaidia mama aliyekuwa na mtoto akitokea kliniki huku jua likiwaka sana.

Kama ilivyokuwa kwa wale wengine, mama yule alikataa kabisa kupewa lifti, tukaamua kuondoka  maana tayari tulishaambiwa sababu., tembelea Bunda ni sehemu yenye vyakula vingi, kuna samaki, nyama za ng’ombe na mbuzi na maziwa kibao bila kusahau kichuri.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *