862 watoa mimba kwa njia zisizo salama, 16 wapoteza maisha

Frank Leonard

WANAWAKE 862 walikimbilia katika hospitali ya Mtakatifu Francisco mjini Ifakara, mkoani Morogoro na kufanyiwa tiba za dharula baada ya kutoa mimba kwa njia zisizo salama.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Anjelo Nyamtema alisema; huduma hiyo ilitolewa kwa nyakati tofauti mwaka 2011 na 2012.

Nyamtema alisema  kati yao, 16 walifariki kwasababu walifika hospitalini hapo wakiwa wamepoteza damu nyingi pamoja na baadhi yao kuoza mfumo wa uzazi.

Alisema umri wa wanawake hao ulikuwa kati ya miaka 15 na 49; walifanyiwa upasuaji na kusafishwa kizazi kwa gharama ya kati ya Sh 20,000 na Sh 50,000 kulingana na ukubwa wa tatizo.

“Kwa upande chanya, wanawake hawa wanahitaji huduma ili waepuke vifo. Lakini kwa upande hasi inaonesha ongezeko la wajawazito wanaotoa mimba kwa njia zisizo salama,” anasema.

Katika kuwahudumia wanawake wa aina hiyo, muuguzi wa wodi ya uzazi hospitalini hapo, Prisca Asenga alisema kama wanavyohudumia wagonjwa wengine, kazi yao ni kunusuru maisha ya mwanamke aliyejaribu kutoa mimba kwa mtu asiye na ujuzi kwa njia zisizostahili na zenye hatari .

Utafiti uliofanywa na shirika la Afya duniani (WHO) mwaka 2010 unaonyesha kuwa kiwango cha utoaji mimba duniani kimebakia kuwa asilimia 28 kwa kila wanawake 1,000.

Hata hivyo WHO inasema uwiano wa mimba zinazotolewa bila utaalamu zimepanda kutoka asilimia 44 mwaka 1995 hadi 49 mwaka 2008.

Mwaka 2009 wanasayansi wa masuala ya afya wa Chuo Kikuu cha Copenhagen Denmark walifanya utafiti wa utoaji mimba nchini; utafiti huo ulihusisha wanawake 278 wa vijijini na 473 wa mijini waliokiri kutoa mimba kwasababu walizipata bila kutarajia.

Matokeo ya utafiti huo yalionesha kwamba asilimia 62 ya wale wa vijijini na asilimia 63 wa mjini walikiri kutumia njia zisizo salama kutoa mimba.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, utoaji mimba huo ulifanywa na watu wasio na ujuzi kwa asilimia 46 ya wanawake wa vijijini na asilimia 60 kwa wanawake wa mjini.

Utafiti unaonesha kwamba dawa za mitishamba zimeendelea kutumiwa kama njia kuu ya utoaji mimba kwa siri; asilimia 42 vijijini na asilimia 54 mijini.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *