Chanjo zasaidia kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano nchini

Frank Leonard

VIWANGO vya chanjo nchini, vimeendelea kupanda toka asilimia 50 miaka ya sitini hadi zaidi ya 90 mwaka 2011.

Afisa Mafunzo wa Mpango wa Taifa wa Chanjo toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Zebina Msumi amesema mafanikio hayo yamewezesha vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja kupungua kutoka 99 hadi 51 sawa na asilimia 49.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi (mwenye tai) akizindua kampeni ya chanjo ya kuhara na nimonia Iringa
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa Amani Mwamwindi (mwenye tai) akizindua kampeni ya chanjo ya kuhara na nimonia Iringa

Kwa upande wa vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano alisema, vimepungua kwa asilimia 45 kutoka 147 mwaka 1999 hadi 81 mwaka 2011, kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa hai.

Mafanikio hayo ni juhudi ya serikali kwa kushirikiana na wadau wake ya kufikia lengo namba tano na nne la malengo ya milenia la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2015.

Aliyataja magonjwa yanayokingwa kupitia mpango wa chanjo kuwa ni pamoja na polio, kifua kikuu, pepopunda, dondakoo, kifaduro, homa ya ini, homa ya uti wa mgongo, surua, nimonia na kuhara.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zilizotolewa mwaka 2010 zinaonesha kwamba kwasasa nimonia ndiyo inayoua watoto wengi zaidi walio chini ya umri wa miaka mitano kuliko magonjwa mengine yoyote.

Kwa mujibu wa takwimu hizo inakadiriwa zaidi ya watoto 800,000 duniani kote wenye umri chini ya miaka mitano hufa kwa nimonia kila mwaka.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na mtoto kupumua kwa shida, kukohoa, homa, kushindwa kula au kunyonya; nyingine ni homa ya uti wa mgongo, ugonjwa wa pua na masikio.

Mratibu wa Chanjo Mkoani Iringa, Dk Naftari Mwalongo alisema ugonjwa huo husababishwa na vimelea vya aina nyingi vikiwemo vya streptococcuos pneumoniae.

Alisema magonjwa yanayosababishwa na vimelea hivyo huenea kwa njia ya hewa wakati mtu mwenye maambukizi anapopiga chafya au kukohoa.

Yanaweza kuambukizwa pia kwa njia ya kugusa sehemu zenye vimelea vya maradhi kama vile nguo, leso na vikombe.

Alizitaja chanjo zinazokinga magonjwa ya nimonia kuwa ni PCV 7, PCV 10 na PCV 13 zinazojulikana kama ‘pneumococcal conjugate’.

Kwa mujibu Dk Mwalongo ugonjwa huo unaweza kutibiwa kwa kutumia viuasumu (antibiotic) kulingana na mwongozo wa uwiano wa matibabu kwa watoto (IMCI).

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *