DOUGLAS Muhani, beki wa zamani aliyepata kuchezea klabu kadhaa za Tanzania pamoja timu ya taifa, Taifa Stars, anakumbuka siku ambayo yeye na wachezaji wenzake walipokesha makaburini wakiroga ili kupata ushindi.
Hii ilikuwa ni mechi ya Ligi ya Taifa Tanzania katika kituo cha Mwanza mwaka 1978, wakati akiichezea Sigara (sasa Moro United) na mechi hiyo ilikuwa inaikutanisha timu yake na Yanga.
“Tuliambiwa na mtaalamu wetu kutoka Tanga kwamba lazima tufanye ndumba kwa sababu mechi ingekuwa ngumu. Mganga wetu, ambaye tulikuwa naye tangu mwanzo wa mechi zetu, alituambia kwamba tungeshinda, lakini mwenzetu mmoja angedondoka uwanjani.
“Tuliamriwa kutomgusa wala kumsogelea, kwa sababu kufanya hivyo kungemaanisha kwamba angepoteza maisha,” anakumbuka. “Na kweli, kabla hatujafunga bao, mchezaji mwenzetu, John Mlebo, alianguka na kuzimia. Tulimtazama tu mpaka alipochukuliwa kwenye machela. Tulifunga bao, na wakati tulipodhani tumeshinda, Omar Hussein akaisawazishia Yanga zikiwa zimesalia dakika nane tu.”
Muhani anasema katika maisha yake ya uchezaji, akiwa amechezea klabu kadhaa kama Sigara, Coastal Union, Maji Maji na Bandari Mtwara, amekumbana na matukio mengi ya ushirikina kuelekea mechi za soka.
Anasema kuchanjwa chale kwenye vifundo vya miguu, kujifukiza ubani, kuoga maji yaliyowekwa talasimu pamoja na kuvalishwa hirizi ni mambo ya kawaida aliyokumbana nayo na ambayo anasema yanaendelea kufanyika kwa siri katika timu nyingi za soka, siyo Tanzania tu, bali Afrika kwa ujumla.
“Ni suala la saikolojia, unapokuwa mchezaji mambo hayo yanafanyika na hata kama huyapendi itabidi ufanye, kinyume chake unaweza kuonekana msaliti, na timu ikifungwa – hata kama ni kwa kiwango cha mchezo wenyewe – basi utabebeshwa lawama kwamba umevunja masharti,” anasema.
Hata hivyo, Muhani anasema ndumba pekee ambayo inaweza kuifanya timu kushinda ni maandalizi mazuri ukiwa na timu imara yenye wachezaji mahiri na wenye nia ya ushindi.
Anaongeza kwamba, timu nyingi za Kiafrika zinapoteza mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwalipa ‘wataalamu’ ili waroge zishinde, jambo ambalo halina uhalisia wowote, ingawa anabainisha kwamba kwenye mpira, uchawi unachukua asilimia mbili tu.
“Waganga wa jadi wanazichezea timu, wanakwenda kuroga katika timu ambazo ni imara wanazoamini zitashinda. Kama sivyo, mbona hawaendi kuanzisha timu mchangani na kuzipandisha daraja?” anahoji.
Vitendo vya ushirikina kwenye soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla vimekuwa vya kawaida, Simba na Yanga zikiwa zinatajwa kuongoza katika kuwa na waganga wengi nchini Tanzania.
Mechi baina yao hukumbwa na vituko vingi vya kishirikina na haikushangaza wakati mwaka 2004 timu hizo mbili zilipopigwa faini ya Dola 500 kila moja na Chama cha Soka Tanzania (FAT) baada ya wachezaji wao kufanya vitendo vya ushirikina ndani ya uwanja.
“Huu ni utamaduni tu, wakati mwingine matukio na vitendo hivyo vya ushirikina vinaongeza utamu wa mechi. Ni kama chumvi kwenye mchuzi,” anasema shabiki wa Yanga Juma Magoma.
“Kuna matukio mengi ya ushirikina, huwezi kuyahesabu. Watu hupewa ‘vitu’ wavibebe wakati timu zao zinapocheza, lakini ni lazima nao wawe wameganguliwa, maana imetokea mara kadhaa ‘vitu’ hivyo vimewadhuru baadhi ya watu. Simba na Yanga zina waganga wengi kila kona na inategemea ni nani aliye bora kwa mechi fulani, wakati mwingine mganga huyu anaweza kuisaidia timu pinzani ilimradi amepewa fedha ya kutosha. Huu ni utamaduni wetu, huwezi kuupuuza, ni utamaduni wa Mwafrika,” anaongeza Magoma.
Mkongwe wa soka wa Afrika, Abedi Ayew Pele wa Ghana aliwahi kukiri kwamba uchawi umetawala soka la Afrika. “Nimeshuhudia vitendo vya ushirikina mara nyingi kwa sababu ndani ya Black Stars walikuwa wanatuletea vitu vya kunawa, kunywa na kuogea,” nahodha huyo wa Ghana aliwahi kuliambia shirika la habari la GMS Press. “Ndani ya klabu ndiyo usiseme, kwa sababu vitendo hivyo ni vingi mno.”
Ni sehemu ya mchezo
Pamoja na kelele nyingi zinazopigwa, lakini wanaoamini na kujihusisha na vitendo vya ushirikina wanasema hiyo ni sehemu ya mchezo katika soka la Afrika.
Mganga wa jadi, Sharif Hussein Aboutwalib, anaamini kwamba anao uwezo wa kuzisaidia timu kushinda kutokana na timu nyingi kwenda kwake.
Sharif Hussein ambaye anaishi Bagamoyo, ameeleza bayana kwamba kwa miaka zaidi ya 20 sasa amekuwa akizipatia timu mbali mbali dawa ili zishinde, na sifa zake zimeenea mpaka Arabuni ambako mara kadhaa amekuwa akienda kufanya uganga wake.
“Wanakuja, wengi tu – kuanzia wachezaji, makocha na viongozi wa klabu – wakitaka niwatengenezee dawa ili wawe bora, na amini nakuambia, inasaidia,” anasema kwa kujiamini.
Anaongeza kwamba, tiba za jadi zinasaidia kuleta matokeo ya uwanjani, ingawa Wazungu wanapinga kama walivyoupinga utamaduni wa babu zetu na kuuita ni wa kijinga.
“Wazungu wao wanatumia dawa za kuongeza nguvu ili wawe na nguvu na kasi. Sisi Waafrika hatuna uwezo wa kupata dawa hizo za kuongeza nguvu, tunatumia jicho la tatu na nguvu za tiba za jadi ambazo hata waje na vipimo vya kisayansi hawawezi kugundua,” anaeleza.
Yapo matukio mengi kwenye mechi za soka barani Afrika. Mwaka 1975 kipa wa klabu ya Aigles Nkongsamba nchini Cameroon aliwahi kwenda kwenye mechi ya fainali akiwa na tai. Hiyo ilikuwa inawatisa wapinzani wao, Canon Yaounde, ambao waligoma na kutaka ndege huyo aondolewe.
Katika mechi moja iliyochezwa katika Mkoa wa Kasai, Mashariki mwa Congo DR Oktoba 28, 1998, radi iliua wachezaji wote 11 wa timu mwenyeji ya Bena-Tshadi na kuwajeruhi watu 30, lakini hakuna hata mchezaji mmoja wa timu ngeni ya Basanga aliyedhurika. Tukio hilo lilihusishwa na mganga mmoja maarufu nchini Congo aitwaye Tata Dongo Remi.
Januari 2008 gazeti la Daily News la Malawi liliripoti kwamba vitendo vya uchawi vilitawala mechi ya ligi baina ya Dwanga United na Moyale Barracks. Iliripotiwa kwamba mchezaji wa 11 wa Dwangwa, Winter Mpota, alikuwa nje ya uwanja na aliingia uwanjani baada ya wapinzani wao wote kuingia uwanjani.
“Kwa kutilia shaka vitendo vya timu mwenyeji, Moyale pia ikaiga mtindo huo wakati wa kipindi cha pili wakati walipomtaka kiungo wao Charles Kamanga abakie nje ya uwanja, wakimsubiri Mpota wa Dwangwa aingie kwanza. Kwa mshangao wa wengi, Mpota hakuingia uwanjani na Kamanga wa Moyale naye hakuingia, na kumlazimu mwamuzi A. Maseko kuendelea na mechi huku kila timu ikiwa na wachezaji 10. Na hiyo yote ilikuwa kwa sababu ya juju,” liliandika gazeti hilo.
Kupiga marufuku
Uamuzi wa FAT kuzipiga faini Simba na Yanga mwaka 2004 kwa vitendo vya kishirikina ni hatua mojawapo ya kukomesha vitendo hivyo katika soka la Afrika, hasa kutokana na ukweli kwamba klabu zinatumia fedha nyingi kuwalipa waganga wa jadi badala ya kufanya maandalizi ya kitaalamu.
Katibu Mkuu wa iliyokuwa Kamati ya Muda ya FAT, Mwina Kaduguda, alipata kusema kwamba, fedha nyingi zinatumika kuwalipa waganga ambao hawana msaada wowote badala ya kuboresha maslahi ya wachezaji ili wajitume.
“FAT iliwahi kumlipa mganga aliyesafiri na timu ya taifa kwenda Nairobi katika mechi ya awali ya Kombe la Dunia dhidi ya Kenya,” aliwahi kukaririwa na BBC Sport akisema. “Walitumia posho za wachezaji kumlipa mganga na wachezaji hawakupata chochote. Hatimaye taifa Stars ilifungwa mabao 3-0. Hii haikutokana na kuzidiwa uchawi na Wakenya, bali wachezaji walikosa morali kwa sababu ya kunyimwa posho zao.”
Katibu wa zamani wa Simba, Kassim Dewji, pamoja na mafanikio aliyoiletea timu hiyo ya kutwaa vikombe nane ikiwa ni pamoja na kuiwezesha kuivua ubingwa wa Afrika Zamalek na kutinga kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, lakini alilazimika kujiuzulu mwaka 2004 baada ya kushindwa kuafikiana na wazee wa klabu waliokuwa wanashinikiza kila mara waganga walipwe fedha.
Dewji aliwahi kusema kwamba, viongozi wengi wa klabu wanashiriki vitendo vya ushirikina kwa sababu ya kuhofia kufukuzwa na wanachama, na kwamba kuna vikundi vya watu vinavyonufaika kutokana na mamilioni ya fedha yanayotengwa kwa madai ya kuwalipa waganga hao wawezeshe timu ishinde.
“Naamini katika maandalizi, kocha bora na wachezaji bora. Lakini ndani ya klabu kuna watu ambao wao wanajinufaisha na fedha hizi za ‘wataalamu’. Klabu inatenga mpaka Dola 5,000 kumlipa mtaalamu ambaye mchango wake hauonekani uwanjani. Ni kazi kubwa,” alipata kukaririwa akisema.
Kwa upande wake, mwandishi mkongwe wa michezo nchini na Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA), Amir Mhando, anasema ingawa vitendo hivyo vipo na vinafanyika kwa siri, lakini havina msaada wowote katika maendeleo ya soka.
“Ni vyema wanaojihusisha na vitendo hivyo wakaachana navyo kwa sababu vinaua kiwango cha mchezo kwa mchezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla. Ni kupoteza fedha na muda,” anasema.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kama ilivyo kwa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) na lile la ulimwengu (FIFA) yanapiga marufuku vitendo visivyo vya kiungwana michezoni na kwamba yeyote anayebainika kujihusisha na vitendo hivyo anaadhibiwa, ikiwa ni pamoja na kufungiwa maisha kujihusisha na soka, kama wanavyopiga marufuku vitendo vya rushwa.
Pengine hatua za namna hii zinaweza zikaliokoa soka la Tanzania na Afrika kwa ujumla na viongozi wa timu wakajikita zaidi katika kusajili wachezaji wazuri, makocha bora na kuziandaa timu kwa makini ili zishindane na kuleta matokeo mazuri uwanjani.