SAMBARU: Kijiji kilichozungukwa na dhahabu kisichokuwa na ofisi

Kulwa Magwa

SERIKALI ya kijiji cha Sambaru, wilayani Ikungi, mkoa wa Singida, imekuwa ikifanyia shughuli zake sehemu yoyote, kutokana na kutokuwa na ofisi.

Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Bernad Nkhomee, anasema hawana ofisi ya kufanyia kazi, suala ambalo huwalazimu kuwasiliana na wananchi kwa njia mbalimbali ili wawatafute mahali wanapokuwa.

Bernad-Nkhomee

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Sambaru, Bernad Nkhomee

Nkhomee anasema, awali waliwahi kuwa na ofisi ambayo waliitumia kufanyia shughuli zao, lakini iliharibika na hata waliyopewa na msamaria mwema nayo imefungwa.

“Kwa sasa hatuna kabisa ofisi na mara nyingi ukinihitaji mimi au mwenyekiti lazima utumie simu au uende nyumbani kwake, “anasema mtendaji huyo wa kijiji.

Kutokana na kutokuwa na ofisi, Nkhomee, anasema nyaraka zinazohusiana na ofisi wamekuwa wakitunziwa na mwananchi anayemiliki nyumba katikati ya kijiji hicho, ili kuwarahisishia kutekeleza majukumu yao.   

Anasema, tayari wamewaeleza wananchi na baadhi ya wachimbaji madini – zikiwemo kampuni kubwa kuchangia ujenzi wa ofisi mpya wanayokusudia kuijenga.

“Hata hivyo mpaka sasa mwitikio umekuwa mdogo maana hakuna fedha zilizopatikana, ikishindikana tunakusudia kuchangisha kwa kuitisha mikutano ya hadhara na kuhamasisha michango ya papo kwa hapo, “anasema.

Kutokuwepo kwa ofisi ya kijiji huwalazimu wageni wanaofika sehemu hiyo kikazi, kuwasaka viongozi kwa kutumia wenyeji au kwenye maeneo maarufu yenye mikusanyiko ya watu.

Akizungumzia suala la wachimbaji na watafiti wa madini ya dhahabu katika kijiji hicho kuchangia shughuli za maendeleo, ukiwemo ujenzi wa ofisi ya kijiji, Mkuu wa wilaya ya Ikungi, Manju Msambya, anasema serikali haiwezi kuzilazimisha kampuni au watu wanaofanya utafiti wa madini, wachangie shughuli zozote kwa kuwa wengi wao hawajaanza uchimbaji.

“Vilevile hawa watu wanachofanya ni utafiti, lakini wakimaliza na kuanza kuchimba kuna kodi na tozo zingine wanazolipa serikalini ukiwemo mrahaba unaobakia wilayani, hivyo hatuwezi kuwashurutisha kwa njia yoyote, “anasema.

Alisema ujenzi wa ofisi, zahanati na miradi mingine ni masuala muhimu ambayo kipaumbele kinapaswa kufanywa na kijiji husika kwa ushirikiano na halmashauri ya wilaya.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *