ABIRIA 5 wamefariki dunia ambapo wengine 11 kujeruhiwa baadhi yao vibaya baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kugongana katika wilaya ya Magu Mkoani hapa.
Habari zilizolifikia FikiraPevu na kuthibitishwa na Kamanda wa apaolisi mkoani hapa zinadai kwamba ajali hiyo ilitokea jana ( Februali 29) katika eneo la barabara kuu la lami, Mwanza-Musoma.
Inadaiwa kwamba ajali hiyo ambayo ilihusisha basi na gari dogo la abiria ilitokea jana majira ya saa 2:45 katika kijiji cha Bulula Kata ya Nyanguge, Tarafa ya Kahangara.
” Mimi alikuwemo ndugu yangu katika moja ya magari yaliyogongana” kilidai chanzo cha habari kwa sharti la kutotajwa jina.
” Ni kweli kuna ajali imeuwa; chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa gari dogo aina ya Noah kugeuka ghafla akiwa katika mwendo kasi na kugongana na basi hilo” alithibitisha Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Liberatus Barlow .
Alisema gari hilo lenye namba za usajili T 716 BMV aina ya Noah Toyota,mali ya Mzamilu lilikuwa likitokea Magu mjini kuelekea jijini Mwanza ,ambapo liligeuka ghafla kuelekea Magu.
Alifafanua kuwa hali iliyosababisha gari hilo kugongana na basi hilo lenye namba za usajili T655 BDP mali ya kampuni ya Zakaria Wambura lililokuwa likiendeshwa na Bw. Aziz Hassan (4).
Alisema ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu watano papo hapo waliokuwa wakisafiri na gari aina ya Noah akiwemo dereva wake.
Alisema abiria 11 waliokuwa katika basi la Zakaria waliijeruhiwa katika ajali hiyo , 10 kati yao walikimbizwa katika hospitali ya wilaya ya Magu kwa matibabu.
Alieleza kuwa majeruhi mmoja kati ya hao 11 aliyetambuliwa kwa jina la Mbarouk Taka (52) mkazi wa Vingunguti Dar es salaam amevunjika mkono wake wa kulia .
Kamanda Barlow alisema majeruhi huyo alikimbiza katika hospitali ya Rufaa Bugando (BMC)Jijini Mwanza kwa ajili ya kupatiwa matibabu na kwamba ali yake ilikuwa mbaya.
“Leo majira ya asubuhi imetokea ajali mbaya ambayo imesababisha vifo vya watu watano, baada ya gari aina Noah kugongana uso kwa uso na basi la abiria mali ya kampuni ya Zakaria ambalo lilikuwa likielekea Sirari wilayani Tarime likitokea Jijini Mwanza,” alisema na kuongeza kuwa,
“Baada ya kufika katika kijiji cha Bulula, kulikuwa na gari dogo la abiria likitokea Magu, ambalo ghafla liligeuka kulekea Magu na kusababisha yagongane na hiyo ni baada ya dereva wa basi la Zakaria kujitahidi kulikwepa bila mafanikio”
Alisema marehemu wanne wametambuliwa ambao ni pamoja na dereva wa Noah,Deus John Kengele (42) mkazi wa Kiloleli Wilaya ya Ilelema jijini,mfanyabiashara,Peter Lubisha (45) .
Wengine aliwataja kuwz ni fundi umeme,Emmanule Kapesa (30) na mwinegine aliyetambuliwa kwa jina moja la Mwinyi mkazi wa Igoma wilaya ya Nyamagana jijini hapa.Marehemu mmoja bado hajatambuliwa.
Imeandaliwana na Juma Ng’oko, Mwanza