“Tenda kama mwenye mali” Ni moja ya ujumbe uliotundikwa katika viambaza vya mgodi wa madini ya dhahabu wa Tulawaka uliopo wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick.
Kisa na maana cha ujumbe huo wanakijua wenye mali ambapo katika maneno ya mwisho unasema daima jiboreshe, na toa mafanikio. Wao ndio wenye mali, hata ugumu wa kuwafikia unathibitisha.
Mgeni wa aina yangu sio rahisi kuaminika,kiu ya kuona uchimbaji na uzalishaji wa dhahabu iliishia kwenye vifusi vyeusi vya mchanga kwenye mashimo makubwa chini ya ardhi vikipakiwa katika magari makubwa.
Barabara chini ya ardhi inayaelekeza magari kuingia katika mashimo na kupotelea katika mahandaki yakibeba mchanga nilioelezwa ni madini yanapelekwa hatua za uzalishaji baada ya kupasua miamba chini ya ardhi.
PICHANI: Mojawapo ya mashimo makubwa katika mgodi wa Tulawaka linalozalisha madini ya dhahabu
Kwamba baada ya saa tatu sikuiona dhahabu, madini ya thamani yenye rangi ya manjano mbivu. Rasilimali iliyozungukwa na wananchi masikini ambayo ni kipimo cha thamani ya sarafu na utajiri wa Watanzania.
Tabaka kati ya wageni na wazawa linachangia harufu ya ubaguzi katika migodi ya madini. Katika mgodi wa dhahabu wa Tulawaka wafanyakazi wanatofautiana kwa kila hali kuanzia huduma hadi malipo.
Kilio kinawakilishwa na Alex Ndallo Katibu wa Chama cha Kutetea na Kulinda Haki za Wafanyakazi wa Sekta ya Madini (TAMICO) kuwa hawana mahusiano mazuri na mwajiri baada ya kupuuzia madai ya kuongezewa malipo huku wageni wakipendelewa.
Anasema zipo kazi zinazofanywa na wageni wanazoweza kuzifanya na kushangazwa posho kukatwa kodi tofauti na sekta ya umma.Tofauti ya huduma za chakula kwa wafanyakazi nayo ni habari nyingine.
Chakula kinatolewa kulingana na wafanyakazi wa tabaka mbili ambao wametengewa maeneo. Wafanyakazi wageni wanaodaiwa ni wataalamu chakula chao ni maalumu tofauti na kundi kubwa la wafanyakazi.
Kwa mujibu wa Katibu huyo inatafsiriwa kama ubaguzi ambapo Kaimu Meneja wa mgodi huo raia wa Ghana Eric Acheampang anasema haoni shida ya utaratibu huo kwani unalenga kuwawezesha wageni kula mapishi ya nchi walizotoka.
Anatetea utaratibu unaoweka mipaka na hawaoni sababu ya wenyeji kunusa mapishi ya kigeni achilia mbali kuyaonja. Udhaifu huu unatumiwa na wawekezaji kwa kuagiza hata nyanya kutoka nje ya nchi hata kama zinapatikana maili moja nje ya mgodi.
Ili kuzima sauti za wafanyakazi, uongozi wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi ambao pia unamilikiwa na Barrick umeanzisha chama cha Buzwagi Workers’ Forum kama mbadala wa TAMICO.
Katibu wa TAMICO mgodini hapo Jonston Mbando anasema hiyo ni mbinu ya kuwadhoofisha ili wasiendelee kudai masrahi bora ya kazi na huduma stahili.
Juhudi za kupinga udhalilishaji zimeishia kufukuzwa kazi akiwa na wengine arobaini ambao wamefungua kesi namba 515/2011 mahakama ya wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.
Kesi hiyo ipo mikononi mwa hakimu Filex Nyalada ambaye katika shauri hilo la jinai amebebeshwa jukumu la kuonyesha kama sheria inashinda haki au vinginevyo.
Kama kiongozi wa tawi Octoba,8,2011 alitoa tangazo la kuhudhuria semina kwa wafanyakazi kwa kufuata taratibu zote ili kuwaelimisha wanachama kuhusu haki zao.
Analaani lugha ya kibaguzi iliyotolewa na Mike Darren raia wa Marekani eti ‘Small dogs to be chassed by big dogs to go to work’. Kwamba mbwa-koko hana la kujitetea mbele ya jibwa!.
PICHANI: Usafirishaji wa vifusi vya mchanga kutoka chini ya ardhi
Kauli ya mzungu huyo ndiyo kiini cha kesi iliyofunguliwa katika mahakama ya wilaya ya Kahama. Ulinzi mkali katika mgodi wa Buzwagi unamzuia yeyote kumfikia raia wa kigeni asijibu tuhuma za udhalimu huu.
Wafanyakazi wa mgodi wa Tulawaka kama walivyo wenzao wa Buzwagi ni sawa na kisa cha shamba la wanyama cha mwandishi wa vitabu George Orwell ambapo baada ya kujikomboa na udhalimu wa binadamu wanyama waliishi kwa usawa.
Baada ya uhuru uongozi wa wanyama uliendesha vitendo vya udhalimu na ubadhilifu wa rasilimali. Kundi la wanyonge lilibaini kuwa wanyama wote walikuwa sawa ingawa baadhi walikuwa bora zaidi.
Kwa hali ilivyokuwa kundi la wanyama wanyonge lilitakiwa kutafakari upya ili kujitetea na kulinda heshima na uhuru wao ambao waliupata kwa gharama ya damu ya ndugu zao na sasa ulikuwa unalinufaisha kundi dogo.
Haya ndiyo mazingira ya kazi yanayowakabiri wafanyakazi wazawa wanaopinga unyonyaji unaofanywa na wawekezaji kuanzia mgodi wa Tulawaka,Nyamongo na kwingineko.
Sura za wananchi wa kijiji cha Mkunkwa ambao kimsingi ni wamiliki wa mgodi wa Tulawaka kwani upo katika eneo lao zimeficha visasi na hofu ya kutoridhishwa na uwekezaji wa mradi mkubwa kama huo katika eneo lao.
Mwenyekiti wa kijiji Leonard John anasema hakuna lolote kubwa ambalo wananchi wanajivunia kwa kuwepo mgodi huo. Anadai pamoja na uongozi wa mgodi kutoa ahadi za kuchangia shughuli za maendeleo hakuna linalotekelezwa.
Kilio cha wananchi ni kwamba wawekezaji hawataki hata kuimarisha barabara kwa hofu kuwa waporaji wa madini wataongezeka. Wanalalama kuwa vipaumbele vyao vimepuuzwa ambavyo ni huduma bora za afya, maji na barabara.
Mwenyekiti wa kijiji hicho anasema wagonjwa husafirishwa kwa machela umbali wa kilometa 18 hadi Runzewe katika wilaya jirani ya Bukombe ili kusaka matibabu kwani hakuna magari kutokana na ukosefu wa barabara.
Upuuziaji wa vipaumbele vya wananchi unajidhihirisha katika kijiji jirani cha Mavota ambapo Mwenyekiti wake Paschal Joachim anasema uongozi wa mgodi umeendelea kuwapiga chenga kwa miaka kadhaa wasitimize ahadi ya kujenga visima vitatu vya maji.
Kaimu Meneja wa mgodi Eric Acheampang anasema wanashirikiana na jamii kuchangia miradi ya maendeleo na kuwa kila mwaka hutoa dola laki mbili za Kimarekani kwa ajili ya shughuli hizo wakiwemo wananchi wa vijiji jirani.
Kama hivi ndivyo nani hukabidhiwa fedha hizo ilhali vijiji jirani havina huduma muhimu. Mkuu wa wilaya ya Biharamulo Ernest Kahindi anakiri kutolewa kwa fedha hizo kila mwaka na kuwa hata hivyo huzitoa kwa kusuasua baada ya ufuatiliaji wa mara kwa mara.
Kwamba fedha za mgawo uliopita ambao ulilenga pia kutimiza ahadi kwa wananchi wa kijiji cha Mavota, uongozi wa wilaya uliona ni busara zote zielekezwe katika ujenzi wa shule ishirini miongoni mwake shule kumi za msingi.
Hii ndiyo Biharamulo ambayo Taasisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) kwa mwaka 2009 inaionyesha kuwa imezama katika tope la umasikini kwa mwananchi kuwa na wastani wa pato la shilingi 420,000 kwa mwaka sawa na shilingi 1,167 kwa siku.
Wastani wa pato kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kwa mwaka ni shilingi 483,158 sawa na shilingi 1,342 kwa siku huku wastani wa pato kitaifa kwa mwaka zikiwa ni shilingi 693,470 sawa na shilingi 1,926 kwa siku.
Nchi inayojali utawala bora wananchi wanashirikishwa na wao kujiandalia mipango ya utekelezaji kulingana na vipaumbele na wala sio kufuata utashi wa viongozi wanaojipa jukumu la kufikiri badala yao.
Uwazi na uwajibikaji ni masuala ya msingi katika utawala bora na kilichofanyika ni ubabe wa viongozi wa wilaya ya Biharamulo kukandamiza matakwa ya wananchi wa kijiji cha Mavota na vinginevyo.
Hawakuhusishwa na badala yake viongozi kujichukulia uamuzi wa kufikiria mahitaji badala yao. Matumizi ya fedha hizo hayawezi kuaminika kwani yamevitenga vijiji vilivyochakaa kutokana na vumbi la mgodini.
Matokeo ya kutowahusisha wananchi leo tunashuhudia majengo yaliyotelekezwa porini katika wilaya ya Missenyi eti ni masoko kwa ajili ya wananchi. Hii ni miradi ya viongozi ambayo hualarishwa ofisini kwa kutumia mgongo wa wananchi.
Mikataba ya madini baina ya serikali na wawekezaji imekuwa chanzo cha malalamiko mengi ya wananchi kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa kuruhusu vitendo vya unyanyasaji na uporaji wa rasilimali bila taifa kunufaika.
Hata hivyo Waziri wa Nishati na Madini Wiliamu Ngeleja akiongea na Fikra Pevu anasema kuwa sheria ya madini iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni inalenga kulinufaisha taifa wakiwemo wananchi wanaozunguka maeneo ya migodi.
Kwa mujibu wa Ngeleja Serikali iko tayari kuwatimua wawekezaji wakorofi na kuwa sasa suala la kununua bidhaa na huduma kutoka kwetu sio jambo la hiari tena.
Anakiri kuwa kuna malalamiko mengi katika sekta hiyo na kushangaa wafanyakazi kutengwa kwa mafungu wakati wa kupatiwa huduma mbalimbali na uongozi wa migodi.
Kwamba serikali iko tayari kuwalinda wafanyakazi wanaotoa malalamiko ya unyanyasaji dhidi ya migodi na kuwa katika baadhi ya maeneo yapo malalamiko ya ufujaji wa fedha zinazotolewa na migodi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.
Imeandikwa na Phinias Bashaya mwandishi wa Fikra Pevu – Kagera