Ajira za watumishi wa afya Bunda zazingatia ukabila

Gordon Kalulunga

AFYA inatafsiliwa kuwa ni ukamilifu wa binadamu kimwili, kiakili na kijamii na kutokuwepo kwa maradhi na tafsiri hiyo ipo katika sera ya afya ya taifa ya mwaka 2007.

Tunapozungumzia sera tunamaanisha kuwa ni tamko lenye kusudio la kufikia lengo au madhumuni maalum.

Nilipokuwa katika mkoa wa Mbeya wilaya ya Ileje, Chunya na Mbeya mjini na hatimaye mkoani Mara katika wilaya za Bunda, Butiama na Musoma nikifanya utafiti wa masuala ya afya ya uzazi, nimejionea mambo kadhaa yakiwemo mambo tisa ambayo nitayagusia leo.

Mambo hayo ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa watumishi wenye sifa kulingana na mahitaji ya wagonjwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Mengine ni miundombinu duni katika sehemu za kutolea huduma na umbali wa huduma hizo, vifaa tiba, upatikanaji wa damu salama, dawa, kauli, idadi ya watumishi, matatizo ya Kliniki, na usafiri.

Kwa upande wa ajira watumishi wengi wa idara ya afya wakipelekwa mkoani humo hasa wale ambao hawana asili ya mkoa wa Mara wanalazimika kuhama na wasichana wanalazimika ‘’kununua’’ vyeti vya ndoa na kuhama wakisema kuwa wameolewa.

Kutokana na hali hiyo Mganga mkuu wa wilaya ya Bunda Dr. Rainer Kapinga anasema kuwa wanapotaka kuajili watumishi katika wilaya hiyo wanatuma maombi na kuainisha sifa za watumishi wizarani kuwa wanaotakiwa ni lazima wawe na asili ya mkoa huo.

Anataja sababu kubwa ni kutokana na hulka za watu wa mkoa huo kuonekana kutojali watumishi kwa kuwatolea kauli ambazo haziwaridhishi baadhi ya watumishi wasio na asili ya mkoa huo na kuamua kuhama.

‘’Kwa mfano mgonjwa umemtundikia drip ya maji baada ya muda kidogo anakuambia kuwa njoo unitoe dudu lako hili’’ anasema Dr. Kapinga.

Makabila yanayoonekana kuweza kumudu mazingira mkoani humo ni kabila la wakulya na waikizu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *