“Hakuna sehemu yenye UKIMWI katika dunia hii kama ilivyo hapa Chome.”
Ni maneno ya Anna Clement anayeona mienendo ya wakazi wa eneo hili isivyokuwa mizuri, na kwa hali hiyo, maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI yatakuwa juu.
Ameongeza ndugu mwandishi utaona leo huyu katembea na huyu na kesho na yule wakati unajua huyu anaugua ugonjwa huu wa ukimwi.
Mkazi mwingine wa Chome, Cleopa Mshighati anasema heshima hakuna kabisa watu wanafanya umalaya nje nje sio kama zamani huwezi kuona hali hii.
Ameongeza kitu cha kwanza huku kijijini kwetu ugonjwa wa ukimwi unakwenda kwa kasi, kwasababu kabila la kipare tunaona ugonjwa huu ni siri, hatuwezi kuelezana wazi wazi kuwa mwenzetu huyu ana maambukizi ya ugonjwa huu.
Mshighati alisema umaskini ndio unaosababisha watu kupata ugonjwa huu na akitolea mfano kwa vijana wa shule za sekondari alisema hawanywi chai ama chakula nyumbani na kukosa mahitaji mengine kama mafuta,nguo na kujikuta wanatumbukia katika mtego wa mapenzi na hatimaye kuweza kuambukizwa kwa kuwa si rahisi kushauri matumizi ya kinga.
“Kwa mtazamo wangu naona suala la ugonjwa huu, lingekuwa wazi kwa kila mtu aliyeathirika, ikijulikana kuwa fulani anao ingesaidia kuokoa kizazi kijacho.”aliongeza Mshighati.
Mshighati alisema usipokupata ugonjwa huu hautaona umuhimu wake wa kujikinga,lakini ukikuingia hubaki kuwa majuto.
Bwana mazingira msaidizi utawala, Kitwana Mungi alisema sababu ya kuonekana kuna maambukizi kwa kata ya Chome ni kwamba mwaka 2008-2010 wahamiaji kama 3000,waliokuja kuchimba dhahabu isiyo rasmi walivamia msitu wa Chome(Shengena),na kwa hali hiyo maambukizi yanaweza yakawa yaliongezeka.
Hata hivyo ameongeza kuwa elimu juu ya maambukizi ya VVU inatolewa lakini kuitekeleza ni suala la mtu binafsi kuamua.
Kaimu mkurugenzi wa wilaya ya Same, James Nshare amesema maambukizi ya wilaya ya same yamepungua tunakaribia kufikia asilimia mbili,na kunauhamasishaji unaendelea,Hedaru ndio inaongoza lakini nayo inapungua kwa kuwa uhamasishaji unafanyika katika nyumba za kulala wageni na kwa wananchi.
“Kwa upande wa Chome wananchi hawakuwahi kuona mgonjwa wa ukimwi na baada ya mwingiliano wa watu waliovamia msitu kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania ikatokea hivyo na kuweza kusema panaongoza”alisema Nshare.
Mkuu wa wilaya ya Same mh.Herman Kapufi amesema si kweli kwamba Kata ya Chome inaongoza kwa kuwa na maambukizi mengi katika wilaya hii.
“Risala niliyosomewa katika maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani mwaka jana(2012), kutoka ofisi ya mganga mkuu wa wilaya inaonyesha kupungua ,kwa sasa ni 2.8% tu.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mganga mkuu wa wilaya ya Same, Dr. Aubrew Mushi alisema tunafanya kliniki ya kuwahamasisha wananchi kwa kutumia madaktari waliopo katika mpango wa VTC katika kuzuiya maambukizi ya VVU kwa wilaya nzima.
Akizungumzia hali ya maambukizi kiwilaya, mganga mkuu huyo amesema yamepungua kutoka asilimia 5 ya hapo awali hadi kufikia 2.8% mwaka 2012.
Hata hivyo amesema kinachokwamisha jitihada za uhamasishaji wakati mwingine ni rasilimali fedha ili kuweza kuwafikia watu wote kwa wakati.
Kwa mujibu wa Dr. Eligi Musile wa kitengo kinachojihusisha na kupambana na ugonjwa wa ukimwi,katika hospital ya mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi alisema maambukizi ya kimkoa yamepungua kutoka 7% mwaka 2003 hadi kufikia 1.9 mwaka 2008.
“Takwimu hizo zilipatikana baada ya kufanyika utafiti wa kwanza mwaka 2003-4,na wa pili 2007-8” aliongeza Dr. Musile.
Akizungumzia sababu za kushuka kwa namba ya watu walioathirika ni uwelewa kuongezeka,elimu ya masuala ya ukimwi iko kwa kiasi kikubwa,kuna NGO’s nyingi zinazoendesha mapambano ya ugonjwa huu pamoja na viongozi wa siasa na mashirika ya dini kuhusika katika mapambano.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania TACAIDS kuhusu hali ya maambukizi Tanzania kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2007-2008 kiwango cha maambukizi kitaifa kilishuka kutoka asilimia 7.7 ya mwaka 2003-2004 mpaka 5.1.
Mikoa 5 inayoongoza kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2007/2008 ikiwa ni Iringa 15.1%, Dar-es salaam 9.3%, Mbeya 9.2%, Mara 7.7% na Shinyanga 7.4% huku mkoa unaoongoza kwa maambukizi mpya hivi sasa ni Mara ambao umeongeza 3.5% kutoka 4.2% za mwaka 2003/2004 na kufikia 7.7% za mwaka 200/2008.