Bila kuzingatia ukweli na ushahidi wa utafiti wa ndani, serikali haitatekeleza malengo ya milenia kufikia mwaka 2015

Gordon Kalulunga

AFYA inatafsiliwa kuwa ni ukamilifu wa binadamu kimwili, kiakili na kijamii na kutokuwepo kwa maradhi na tafsiri hiyo ipo katika sera ya afya ya taifa ya mwaka 2007.

Tunapozungumzia sera tunamaanisha kuwa ni tamko lenye kusudio la kufikia lengo au madhumuni maalum.

Nilipokuwa katika mkoa wa Mbeya wilaya ya Ileje, Chunya na Mbeya mjini na hatimaye mkoani Mara katika wilaya za Bunda, Butiama na Musoma nikifanya utafiti wa masuala ya afya ya uzazi, nimejionea mambo kadhaa yakiwemo mambo tisa ambayo nitayagusia leo.

Mambo hayo ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa watumishi wenye sifa kulingana na mahitaji ya wagonjwa katika zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Mengine ni miundombinu duni katika sehemu za kutolea huduma na umbali wa huduma hizo, vifaa tiba, upatikanaji wa damu salama, dawa, kauli, idadi ya watumishi, matatizo ya Kliniki, na usafiri.

Ajira.
Kwa upande wa ajira watumishi wengi wa idara ya afya wakipelekwa mkoani humo hasa wale ambao hawana asili ya mkoa wa Mara wanalazimika kuhama na wasichana wanalazimika ‘’kununua’’ vyeti vya ndoa na kuhama wakisema kuwa wameolewa.

Kutokana na hali hiyo Mganga mkuu wa wilaya ya Bunda Dr. Rainer Kapinga anasema kuwa wanapotaka kuajili watumishi katika wilaya hiyo wanatuma maombi na kuainisha sifa za watumishi wizarani kuwa wanaotakiwa ni lazima wawe na asili ya mkoa huo.

Anataja sababu kubwa ni kutokana na hulka za watu wa mkoa huo kuonekana kutojali watumishi kwa kuwatolea kauli ambazo haziwaridhishi baadhi ya watumishi wasio na asili ya mkoa huo na kuamua kuhama.

‘’Kwa mfano mgonjwa umemtundikia drip ya maji baada ya muda kidogo anakuambia kuwa njoo unitoe dudu lako hili’’ anasema Dr. Kapinga.

Makabila yanayoonekana kuweza kumudu mazingira mkoani humo ni kabila la wakulya na waikizu.

Miundombinu
Nilijionea uhaba mkubwa wa maji, tatizo la umeme ambapo kutokana na mfumo wa serikali kuamua kutumia Luku hospitali nyingi wanapata shida hasa wakati wa upasuaji(Oparation) huku wakihofia unit kuisha maana ukinunua umeme mwingi na hata makato wakati wa kununua tena yanakuwa makubwa zaidi na bajeti hazitoshi.

Mfano ni katika hospitali ya Manyamanyama ambako wataalam akiwemo muuguzi mkuu wa hospitali hiyo ambaye anasema kuwa ni vema serikali ikabadili mfumo huo ws Luku katika hospitali zinazotoa huduma za upasuaji.

Vyumba vya kulaza wagonjwa ni vidogo kwa mfano katika hospitali ya Butiama ambako chumba chenye dirisha moja kina vitanda kumi na hewa ni ndogo na wanawake wajawazito wanalazimika kutumia choo cha nje kilichopo umbali wa mita thelathini hali ambayo ni hatari na wanaweza kujifungulia chooni.

Katika zahanati ya Bunda zahanati hiyo chumba cha kuchomea sindano hakina dirisha hali ambayo inatakiwa miundombinu ya zahanati hiyo irekebishwe.

Pia katika kituo cha afya cha Ikizu familia mbili za watumishi hazina choo wala bafu kutokana na choo walichokuwa wakitumia kubomoka hivyo kulazimika kuchangia choo na wagonjwa wanaolazwa katika kituo hicho cha afya na kinatumika na wagonjwa wa nje.

Vifaa tiba.
Kuna uhaba mkubwa wa vifaa tiba katika hospitali na vituo vya afya katika mkoa wa Mbeya na Mara vikiwemo vya kusaidia wajawazito wakati wa kujifungua zikiwemo Suction Machine, Musk bag, sindano za kuchoma kwenye mapaja ili kumsaidia mama baada ya kujifungua ili kutoa kondo la nyuma, glovu na dawa zenyewe.

Kwa mfano katika hospitali ya Butiama mkoani Mara, madaktari wanalazimika kuwatoa kondo la nyuma akina mama baada ya kujifngua kwa njia za zamani kwa kuvaa glovu kwa kuunganisha kisha kuwaingiza mikono ukeni nah ii inaonesha ni jinsi gani hawajapata mafunzo ya kisasa ya kutumia sindano.

‘’Tunalazimika kufanya hivyo kuunganisha glovu ili kutoa kondo la nyuma la mama aliyejifungua kutokana na kutokuwa na glovu maalum ambazo ni ndefu zinazofaa kutumika na kutokuwa na sindano za kuwachoma kwenye mapaja ili kondo la nyuma litoke lenyewe’’ anasema kaimu Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Joseph Musagasa.

Damu salama.
Kuhus damu salama kuna tatizo kubwa linaloikabili nchi ambapo wagonjwa wengi wanahitaji damu salama lakini baadhi hawapati kutokana na kutokuwepo watu wa kujitolea damu.

Wengine wanapata damu kwa gharama kubwa kuanzia Sh.10,000 mpaka Sh. 25,000 kwa unit moja na baadhi ya wagonjwa wanakufa baada ya kukosa msaada wa damu.

Hivyo katika baadhi ya vituo vya afya na hospitali wanaamua kuokoa maisha ya wagonjwa hao kwa kuwatoa damu watu wanaokubali hasa ndugu wa wagonjwa na kuwaongezea wagonjwa bila uhakika wa vipimo vya VVU na UTI(Magonjwa ya zinaa) na ini.

Moja ya sababu za ukosefu wa damu kwa baadhi ya wanawake ni pamoja na ukosefu wa lishe bora ikiwemo samaki na matembele ambapo kwa watoto ni kutokana na homa kali na Malaria.

‘’Katika wilaya yetu ongezeko la upungufu wa damu kwa wajawazito ni kutokana na lishe duni ambapo kwa sasa samaki wanavuliwa na kupelekwa viwandani mkoani Mwanza hivyo wanawake wanakosa vyakula bora ikiwemo matembele’’ anasema mratibu wa afya ya mama na mtoto katika wilaya ya Bunda Daines Limo.

‘’Upungufu wa damu ni mkubwa kwa wagonjwa na wanaohitaji zaidi damu ni wajawazito, watoto na majeruhi wa ajali hivyo naiomba jamii ihamasike kutoa damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananchi wenzetu au ndugu zetu’’ anasema meneja wa benki ya damu salama kanda ya nyanda za juu kusini iliyopo mkoani Mbeya Dr. Baliyima Lelo.

Dr. Lelo anasema kuwa hakuna madhara ya kutoa damu kwasababu kuna wataalam wa kupima wingi wa damu na kujua watu wanaostahili kutoa damu ambapo kwa wale ambao damu yao ni chache hawatolewi damu, hivyo anatoa wito kwa wananchi kuona utoaji damu ni tendo la kizalendo.

Wanaokufa kwa wingi kutokana na ukosefu wa damu ni wajawazito na watoto chini ya miaka mitano ambao wanakabiliwa na upungufu huo kutokana na Maralia.

Dawa zinazohitajika kwa wajawazito.
Dawa zinazohitajika kwa wajawazito ni pamoja na dawa za Malaria, Pain Killer, dawa za kuharakisha kupona vidonda au maumivu (Antibiotic), Octacin, Sp na mseto lakini wajawazito wengi wamekuwa wakipewa dawa aina ya SP pekee huku katika baadhi ya maeneo wakinunua hata kadi za kliniki ingawa zimeandika kuwa haziuzwi.

Kauli mbaya kwa wagonjwa
Kumekuwa na mitazamo ya kimazoea na uhalisia wa ndani ambao kwa watumishi wa serikali wakifanya utafiti hawawezi kupata majibu lakini binafsi nilipata ushirikiano kwa baadhi ya wajawazito walioniamini katika wilaya ya Ileje na Chunya mkoani Mbeya, Bunda, Butiama na Musoma mkoani Mara.

Wajawazito hao wanasema kuwa baadhi wanataka kwenda kujifungulia katika sehemu za kutolea huduma za kisasa yaani zahanati, vituo vya afya na hospitali lakini hawapati ushirikiano kutoka kwa wauguzi badala yake wanapata matusi na kejeli kuwa wanapaswa kujifungua kwa nguvu zao bila msaada kwasababu wakati wanafanya tendo la ndoa wao hawakuwepo!nk.

Wajawazito wengi wanasema kuwa kutokana na kauli za wauguzi hao imefikia mahala kuona ni bora kujifungulia nyumbani ama kwa wakunga wa jadi kuliko kwenda sehemu ya kutolea huduma za kisasa na kwamba watalazimika kwenda hospitali kama watakuwa na matatizo makubwa katika ujauzito wao ingawa kliniki wanahudhuria kila tarehe wanayopangiwa.

Idadi ya watumishi na mafunzo kazini.
Idadi ya watumishi ni ndogo na baadhi hasa wale ambao wameajiliwa na mashirika ya dini yaani hospitali teule za wilaya badala ya halmshauri, wamekuwa wakilalamikia mfumo uliopo ambapo wale walioajiliwa na halmashauri wanapata mafunzo kazini ya mara kwa mara lakini wao hawapati.

Kwa mfano katika hospitali teule ya wilaya ya Bunda (DDH) mkoani Mara watumishI walioajiliwa na kanisa katika kitengo cha wazazi wanalazimika kutumia musk moja na glovu moja kuwasaidia wanawake kujifungua na hawajui zana za kisasa zilizobadilika kutokana na kutopata mafunzo kazini tofauti na wenzao walioajiliwa na halmashauri.

‘’Tunafanya kazi muda wote na miaka yote lakini hatupati mafunzo kazini tofauti na wenzetu walioajiliwa na halmashauri tunaomba serikali iliangalie jambo hili. Tunaomba serikali ituangalie’’ anasema Peter Sungwa ambaye ni muuguzi kiongozi katika wodi ya wazazi hospitali teule ya DDH Bunda.

Kliniki
Mahudhurio ya wajawazito wengi Kliniki ni ya kuridhisha sana ambapo ni asilimia 96 ya wajawazito wanahudhulia kliniki lakini wakati wa kujifungua ni asilimia 56 tu.

Wajawazito wengi wanasema kuwa wanapoenda kujifungulia katika vituo vya afya wanakumbana na gharama kubwa zikiwemo zile za kununua karatasi ya kulala wakati wa kujifugua, matusi na gharama za mwendo kutoka mahala wanakoishi mpaka kufikia huduma kuna umbali mrefu.

Kwa mfano katika hospitili ya Butiama kuna wanawake wanahitaji kujifungulia katika eneo la vituo vya afya lakini wanaishi umbali wa kilomita 100 na vituo hivyo na wanalazimika kujifungulia nyumbani au kwa wakunga wa jadi.

Usafiri.
Jiografia ya maeneo mengi katika mikoa ya Mbeya na Mara kufikia huduma za kisasa hasa kwa wajawazito siyo nzuri.

Kwa mfano katika wilaya mpya ya Butiama kuna wajawazito wanaishi kilomita 100 na hospitali ya wilaya ambayo ndiyo tegemeo lao katika kujifungua hasa wale wenye matatizo ambapo ambao hawana matatizo hulazimika kujifungulia nyumbani au kwa wakunga wa jadi.

Kuhusu ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa mwaka 2010 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu kuwa serikali ingenunua pikipiki za matairi matatu(Bajaji) ahadi hiyo imetekelezeka na baadhi ya vituo vya afya zipo bajaji hizo lakini hazifanyi kazi kutokana na dosari mbalimbali ikiwemo kutokata kona upande wa kushoto na muundo wake kuonekana kuwa wa udhalilishaji kwa wanawake.

Bajaji hizo 400 zilizosambazwa maeneo mengi nchini zinadaiwa kununuliwa kwa Shilingi Milioni 40 na kusambazwa katika vituo vya afya 134 lakini hakuna mahala zinapofanya kazi ya kusaidia wajawazito na maeneo mengine wamefungua kitanda na kuamua kutumia pikipiki kwa ajili ya kazi za kubebea dawa na vifaa vya hospitali.

Hali hiyo inajidhihilisha kuwa nchi aina wataalam wa utafiti bali mambo mengi utafiti unafanywa nje ya nchi hatimaye utafiti wao unatekelezwa Tanzania bila kuangalia mazingira na miundombinu ya nchi yetu hatimaye kuonekana kuwa fedha nyingi zinatumika bila faida.

Kutokana na ukweli, takwimu na ushahidi huo, kazi inabaki kwa serikali kuchukua hatua ili kutekeleza malengo ya milenia ambayo yanasema kuwa kufikia mwaka 2015 inatakiwa kuwe kumepungua kwa vifo vya mama na mtoto. Vinginevyo hatutafikia malengo hayo ya milenia hasa vijijini.

Mwandishi wa makala anapatikana kwa simu 0754 440749. Barua pepe; [email protected] WEB; www.kalulunga.com

2 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *