Serikali yatakiwa kutimiza wajibu wake wajawazito wapate huduma bure

Frank Leonard

UONGOZI wa Hospitali Teule ya Ilembula, wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe umeiomba serikali kutekeleza vifungu vyote vya makubaliano ya uendeshaji wa pamoja wa hospitali hiyo ili huduma kwa makundi maalumu wakiwemo wajawazito na watoto chini ya miaka mitano zitolewe bure.

Katibu wa hospitali hiyo mali ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kusini, Silvester Udope alisema “Vinginevyo wateja wote wa hospitali hii bila kujali maelekezo ya Sera ya Afya ya mwaka 2007 watalazimika kuendelea kuchangia huduma.”

Katibu wa hospitali teule ya Ilembula, Sylivester Udope

 Katibu wa hospitali teule ya Ilembula, Sylivester Udope

Huduma za afya kwa wajawazito ambazo serikali imejitwisha, hupaswa kutolewa bure hospitalini, katika vituo vya afya na katika zahanati.

Kifungu 5.4.8.3 cha Sera ya Afya ya Taifa ya Juni 2007 kinazungumzia msamaha wa uchangiaji gharama za huduma za afya kwa makundi maalum ya kijamii wakiwemo wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa sera hiyo, vituo vya huduma ya afya vinapaswa kutoa dawa, vipimo vya maabara, huduma ya sindano na kutakasia, huduma ya kujifungua kawaida na upasuaji, vifaa wakati wa kujifungua na usafiri kwa wajawazito.

Katika makubaliano yao kuiendesha hospitali hiyo,  Udope alisema serikali ilikubali kulipa mishahara ya watumishi, kutoa ruzuku ya vitanda na bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba, dawa na ukarabati.

Hospitali teule ya Ilembula inavyoonekana kwa mbele

 Hospitali teule ya Ilembula inavyoonekana kwa mbele

Hata hivyo tangu mkataba huo usainiwe Mei 7, 2010, serikali imeshindwa kutekeleza baadhi ya vifungu vya mkataba huo ikiwemo kulipa mishahara kwa watumishi wa hospitali hiyo na kusababisha makundi maalumu yakose huduma wanzostahili kupata bure.

Katika makubaliano hayo, Udope alisema serikali ilikubali kuwalipa watumishi 185 wenye sifa hata hivyo hadi Desemba mwaka jana ahadi hiyo ilitekelezwa kwa watumishi 52 tu.

Wakati Sh 25,000 zinachangwa na wajawazito wa uzao wa kawaida na Sh 60,000 kwa wale wanaofanyia upasuaji, Udope alisema gharama hizo zingeweza kuondolewa kama serikali ingeanza kuwalipa mishahara watumishi hao.

Alisema kwa wastani hospitali hiyo inahuduma wajawazito kati ya 35 na 40 kila siku ambao wote hulazimika kuchangia huduma mbalimbali ili kufanikisha huduma wanazohitaji.

Mhandisi Greyson Lwenge, Naibu Waziri wa Ujenzi ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Njombe Magharibi ilipo hospitali hiyo, anakubaliana na madai ya utawala wa hospitali kuwa serikali imeshindwa kulipa wafanyakazi.

“Tumeanza kulipa baadhi ya watumishi; na hali ya serikali itakaporuhusu…wengine wataanza kulipwa,” alisema na kuongeza kuwa lakini hilo lisiwe sababu ya hospitali kushindwa kutekeleza sera ya afya inayotaka makundi maalumu kupata huduma bure.

Mjamzito akisubiri huduma katika hospitali teule ya Ilembula

Mjamzito akisubiri huduma katika hospitali teule ya Ilembula

Mhandisi Lwenge alisema serikali inaipa Ilembula ruzuku ya zaidi ya Sh. milioni 400 kila mwaka, huku ikipewa dawa moja kwa moja kutoka Bohari Kuu na kuongeza, “…katika hali hii hawana budi kutazama upya suala la gharama ya matibabu.”

Katibu wa Hospitali hiyo anakiri hospitali yao kupokea Sh Milioni 400 kila mwaka kutoka serikali kuu, hata hivyo fedha hizo zote ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi 46 tu ambao serikali imeanza kuwalipa.

“Hospitali inahitaji zaidi ya Sh Milioni 119 kila mwezi kwa ajili ya mishahara ya watumishi wake zaidi ya 200, lakini serikali inatoa wastani wa Sh Milioni 40 kila mwezi kwa ajili ya watumishi 46 tk,” alisema.

Wakati hospitali hiyo inatumia wastani wa Sh Milioni 30 kila mwezi kununua madawa, Udope alisema Serikali Kuu kwa kupitia Bohari ya Madawa (MSD) imekuwa ikichangia dawa zenye thamani ya kati ya Sh Milioni 10 na Milioni 15 ambazo wakati mwingine hazitolewi kwa wakati.

“Tangu tuingie mkataba na serikali zaidi ya miezi 30 iliyopita, hospitali imepata milioni 168 na kidogo badala ya zaidi ya milioni 300 kwa ajili ya ununuzi wa dawa MSD,” alisema.

1 Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *