Hakimu wa Mwanza adaiwa kutishia mtuhumiwa bastola

Jamii Africa

MWANZA IJUMAA APRILI 6, 2012, HAKIMU Mkazi  Mfawidhi Mkoani Mwanza , Angelo Rumisha,  amejitoa kusikiliza kesi  baada ya kutuhumiwa ndani ya mahakama hiyo kwamba alimtishia bastola mtuhumiwa katika viwanja vya mahakama, tuhuma ambazo hakimu huyo ameziita majungu.

Hakimu Rumisha amejitoa katika kesi ya jinai  namba   81/2011; kesi  ya  kughushi nyaraka za serikali  kwa ajili ya kujipatia kiwanja kwa njia   ya udanganyifu na kesi hiyo kuhamishiwa kwa  hakimu Godfrey Mwambapa, wa mahakama ya mkoa  wa Mwanza.

Hakimu Rumisha  alijitoa Aprili 2 mwaka huu baada ya wakili wa mshtakiwa kuieleza mahakama  kwamba mteja  wake, Shida Manyama (ambaye anadaiwa kutumia jina la Selemani Mabuba),  hana imani na hakimu Rumisha kwa sababu aliwahi kumtishia  kwa bastola katika varanda ya mahakama hiyo.

Kabla ya kujitoa kwa maandishi, hakimu  Rumisha aliiambia mahakama kwamba madai hayo hayana ukweli  wowote, ni majungu  na  kuongeza kuwa mtuhumiwa katika kesi hiyo ana lengo la kuchelewesha kesi inayomkabili.

“ Kwa  ujumla hayo ni majungu ambayo lengo lake ni kutaka kuchelewesha maamuzi  ya mahakama . Hata  hivyo mimi ninajitoa  kusikiliza kesi hii  kwa sababu sioni  sababu ya kuing’ang’ania,” Rumisha  aliiambia mahakama  huku akihoji  iwapo  mlalamikaji  alishatoa taarifa kituo chochote cha  polisi juu  ya kitendo hicho.

Alisema  kitendo  kilichofanywa   na mtuhumiwa siyo cha kiungwana  kwa sababu kinalenga kumchafulia jina ndani ya jamii.

Wakili  huyo, Deo  Mgengele, aliieleza mahakama  kwamba Rumisha alimtishia  mteja wake wakati  wakiwa  kwenye  korido  ndani ya jengo la  mahakama.

Katika  hatua nyingine, Mgengele  aliiomba mahakama  hiyo isiendelee kusikiliza kesi hiyo  kwa maelezo kwamba alishaandika barua ya malalamiko kwenda kwa jaji.

Kwa  upande  wake, hakimu Mwambapa  alitupilia  mbali ombi hilo kwa maelezo kuwa  faili lake halikuwa na nakala ya barua hiyo na wala hakuna kifungu chochote cha sheria kinachoweza kuzuia  kesi hiyo isiendelee  kusikilizwa.

Hakimu  Mwambapa  aliitaja kesi hiyo hadi Aprili 30 mwaka huu.

Kesi  hiyo ambayo imefikia hatua ya utetezi ndiyo imesababisha mtumishi wa ardhi  katika halmashauri ya Jiji la Mwanza, Asubuhi Otieno, akamatwe  na kufikishwa kortini  kwa tuhuma za kutoa  ushahidi wa uongo mahakamani.

Imeandaliwa na na Juma  Ng’oko,  Mwanza

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *