Madiwani 22 wa CCM ‘kutimkia’ Chadema

Jamii Africa

TUHUMA nzito zinazoiandama Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, zimeanza kuchukuwa sura mpya, baada ya zaidi ya madiwani 22 kati ya 36 wa CCM wilayani humo kudaiwa kujiorodhesha wakitaka kukihama chama hicho kisha wajiunge na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Taarifa zilizopatikana jioni hii kutoka Misungwi, zinadai kwamba madiwani hao wamefikia uamzi huo kutokana na madai ya kuchukizwa kwao na tuhuma za ufisadi wa fedha za umma zinazomkabili mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Benald Polcarp (CCM).

Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo zimethibitishwa na baadhi ya madiwani hao, tayari madiwani hao wameshajiorodhesha majina yao na kata wanakotoka, kisha dhamira yao hiyo kuipeleka Makao Makuu ya CCM mjini Dodoma leo.

“Kwanza leo, madiwani hawa walitaka kufanya maandamano kwenda ofisi za CCM wilaya kudai mali zao walizokuwa wakichangia. Lakini waliogopa kuandamana baada ya magari ya FFU kuonekana wakizagaa kwa lengo la kupambana nao”, kilisema chanzo cha habari kutoka Misungwi.

Imeelezwa kwamba, madiwani hao wamechukizwa na kitendo cha mwenyekiti wao kuandamwa na tuhuma hizo nzito, na kwamba kamati ya siasa imeshindwa kufuata maazimio ya baraza la madiwani la kutaka ufanyike kwanza uchunguzi wa kina juu ya tuhuma hizo.

Mmoja wa madiwani hao (jina tunamhifadhi kwa sasa), alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba, wamechoshwa na tuhuma zinazomwandama mwenyekiti wao, na kwamba wanajiandaa muda wowote kuihama CCM kisha wahamie Chadema.

Hivi karibuni, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kupitia ripoti yake, aliituhumu halmashauri hiyo ya Misungwi inayoongozwa na madiwani wa CCM kufuja zaidi ya sh. bilioni tano za miradi mbali mbali ya maendeleo.

Baada ya ripoti hiyo ya CAG, Mei 9 mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliagiza kushushwa vyeo kisha kukamatwa na kufikishwa mahakamani Mkurugenzi wa halmashauri hiyo ya Misungwi, Exavier Tilweselekwa pamoja na Mkurugenzi wa Sengerema, Erika Musika.

Tayari kuna taarifa zainazodai kwamba, Wakurugenzi hao walishachushwa vyeo vyao, lakini bado hawajafikishwa mahakamani kujitu tuhuma za ubadhilifu wa mali za umma.

“Tumechoka na mwenyekiti wetu tuliyemchagua sisi madiwani kuandamwa kwa tuhuma za ufisadi. Sisi kwenye baraza tuliazimia uchunguzi ufanyike na ikibainika ashtakiwe mahakamani.

“Kwa maana hiyo, tumejiorodhesha madiwani 22 na mwingine yupo wa 23 anataka ajiorodheshe naye kwa lengo la kuhamia Chadema. Tumeshapeleka orodha yetu makao makuu ya CCM Dodoma wakaione huko”, alisema diwani huyo kwa njia ya simu yake ya kiganjani.

Alisema, katika waraka wao walioupeleka makao makuu ya CCM, wanamtaka Katibu mkuu wao aende haraka sana Misungwi ili akakutane nao kabla hawajafikia uamzi wa kutimkia Chadema.

FikraPevu inayo majina 15 ya madiwani na kata zao wanakotoka, wakiwemo madiwani wa viti maalumu ambao wametishia kukihama chama hicho tawala.

Mwenyekiti Polcarp pamoja na katibu wa CCM wilaya hiyo ya Misungwi, Marco Kahuluda walipotafutwa jioni hii ya leo kwa simu zao za viganjani ili kuzungumzia taarifa hizo, simu zao zilikuwa zimezimwa.

Lakini taarifa nyingine zinadai kwamba, tishio la madiwani hao kutaka kuhamia Chadema, limechochewa na kigogo mmoja wa halmashauri hiyo kwa lengo la kutaka kukikomoa chama hicho tawala.

Habari hizi zimeandaliwa na Sitta Tumma – FikraPevu, Mwanza.

3 Comments

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *