Dr. Slaa, Chadema wamtesa Kikwete

Islam Mbaraka
Dk Willibrod Slaa

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa maandamano na mikutano ambayo chama hicho imefanya na inaendelea kufanya ni mwanzo tu wa shinikizo la umma dhidi ya Serikali ya Rais Kikwete kuitaka serikali hiyo kuchukua hatua mara moja na kali dhidi ya ufisadi, mfumo wa bei, na kuweka ratiba wazi ya mchakato utakaohakikisha kuwa uchaguzi mkuu ujao wa 2015 unafanyika chini ya Katiba mpya.

Akizungumza na Fikra Pevu mapema siku ya Jumatatu Katibu Mkuu wa chama hicho na aliyekuwa mgombea wa Urais katika uchaguzi uliopita Dr. Willibrod Slaa amesema kuwa chama chake kimefikia uamuzi wa kutumia nguvu ya umma kuongeza shinikizo hilo hasa baada ya kuona kuwa serikali ya CCM haichukulii kwa uzito unaostahili madai na malalamiko ya wananchi.

“Tumezungumza mambo yale yale kwenye ukumbi wa Bunge lakini serikali imeendelea kuwa kiziwi na sasa tumejikuta tunalazimika kutumia nguvu ya sauti ya wananchi ili ujumbe wetu ufikie” alisema Dr. Slaa

Akijibu swali ya kwanini wanafanya maandamano hayo sasa badala ya kusubiri uchaguzi mkuu ujao kwani nchi imetoka tu kwenye uchaguzi mwingine Dr. Slaa alisema kuwa “uchaguzi siyo mwisho; mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa maandalizi ya mwingine na shughuli za kisiasa hazikomi kwa sababu uchaguzi umefanyika.”

Dr. Slaa aliendelea kusema kuwa “chama tawala kimekuwa kikitutuhumu kuwa hatuendi vijijini kujijenga sasa tunaanza kwenda kila miji, na wilaya wanakuja na kutuambia kwanini tunaenda vijijini kuzungumza na wananchi. Hawakosi sababu”

Kiongozi huyo wa Chadema ambaye katika ziara hizi za maandamano ameungana na Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Freeman Mbowe na wabunge kadha wa kadha amesema kuwa hoja ambazo wanazijengea hoja sasa hivi zinahitaji maamuzi ya haraka. “Mambo mengi tunayoyazungumza katika maandamano haya na mikutano yanahitaji utendaji wa haraka. Suala la ufisadi kwa mfano. Tunapoona serikali imelala kila mtu anastahili kusimama na kulaani hali hiyo bila ya kujali tafsiri itakayotolewa” alisema Dr. Slaa katika mahojiano yaliyochukua karibu nusu saa.

Dr. Slaa ambaye katika uchaguzi uliopita chama chake kilifanya vizuri kwa kuchukua majimbo kadhaa mapya na kuonekana kukubalika zaidi kuliko uchaguzi wa 2005. Dr. Slaa alishika nafasi ya pili huku Rais Kikwete na chama chake wakiongoza kitaifa lakini kwa kiasi kidogo cha kura kulinganisha na uchaguzi wa 2005.

Dr. Slaa alizungumzia pia suala la malipo ya Dowans na kwanini chama chake kimechukua msimamo wa kutaka majenereta ya kampuni hiyo yakamatwe mara moja. “Hili linaendana na ukweli kuwa suala la Dowans limefungamana na kuingia kwa kampuni ya Richmond nchini na vile vile hoja nzima ya jinsi gani kampuni ya Dowans iliweza kuchukua kiulaghai mkataba wa Richmond na Tanesco”. Dr. Slaa alisema pia kuwa “serikali ina jukumu la kukamata mitambo hiyo na hakuna sababu ya kuilipa kampuni hiyo”

Akifafanua kama itakuwa vizuri kukatama mitambo hiyo wakati kuna tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Usuluhishi wa kibiashara Dr. Slaa alisema kuwa “kwa vile Dowans ilitumia ulaghai kushinda kesi hiyo serikali haitakiwi kufungwa na hukumu hiyo”. “Ni bora kuzuia malipo hayo sasa badala ya kusubiri miezi sita au saba baadaye ndipo tuje kugundua tumefanya makosa kuwalipa. Fedha hizo zingeweza kutumiwa katika kuboresha maisha ya watu wetu, wanafunzi, wafanyakazi na wakulima wa nchi yetu”.

Vile vile, Dr. Slaa alizungumzia suala la haraka ya kuwasha mitambo ya Dowans hata ikibidi kwa mkataba wa muda mfupi kama inavyopendekezwa na baadhia ya watu  ili kupunguza ukali wa tatizo la ukosefu wa nishati kwa maisha ya watu na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Dr. Slaa hata hivyo alitupilia mbali pendekezo hilo.

“Ni lazima kuelewa kwanza maudhui ya mambo yanayoendelea kabla ya kufikia hitimisho hilo. Tayari nchi inapoteza kiasi kikubwa cha fedha kwa kulipia gharama ya kutumia mitambo ya IPTL. Serikali ilishauriwa karibu miaka mitano iliyopita inunue moja kwa moja mitambo ya IPTL lakini haikufanya hivyo. Mwaka 2007 serikali iliambiwa kuwa mitambo ipo na kuwa ifanye ununuzi wa kimataifa lakini serikali haikufanya lolote vile vile.”

Dr. Slaa aliendelea kusema kuwa “tunaamini kabisa kuwa juhudi za kutaka mitambo ya Dowans iwashwe na mkataba mwingine uingie ni sehemu ya ufisadi ule ule unaondelea nchini. Tukumbuke kuwa mwezi wa Machi umeshafika na ndio kipindi cha kuanza kwa mvua za masika nchini na hivyo ni wazi baada ya muda si mrefu mabwawa yetu ya kufua umeme yatakuwa yamejaa maji. Sasa kwanini tuingie mkataba wakati huu?” aliendelea “tukumbuke pia kuwa wakati majenereta haya hatimaye yanaanza kufanya kazi mwezi Machi mwaka 2007 mvua zilikuwa zimeanza na mabwawa yalikuwa yamejaa maji lakini tulikuwa tumefungwa na mkataba. Fedha ambazo tungetumia kuingia mkataba na Dowans wakati huu zingeweza kabisa kutumika kununua mitambo mipya tena ya kwetu bila ya kuja kulazimika kulipia gharama ya matumizi ya mitambo hiyo”.

Dr. Slaa akizungumza kwa umakini mkubwa alisema kuwa “tayari nchi inapoteza umeme sasa hivi, ni bora basi kupoteza umeme huo kwa wiki mbili zijazo na kupata suluhisho la kudumu kuliko kujiingiza katika mkataba mwingine utakaotugharimu kwa muda mrefu ujao.”

Akizungumzia suala la Katiba Mpya Dr. Slaa alisema kuwa chama chake kiliandika katika ilani yake ya uchaguzi suala la Katiba mpya na kiliweka ahadi ya kuwa uchaguzi ujao ungefanyika chini ya Katiba mpya endapo chama hicho kingeshika madaraka. “Sasa kwa vile serikali imekubali kimsingi suala la Katiba Mpya hakuna jinsi nyingine isipokuwa kuhakikisha kuwa kunakuwepo na Katiba mpya ambayo itaweka vyombo na taratibu ambazo zitazuia kabisa uwezekano wa kutokea machafuko na umwagikaji damu nchini”.

Dr. Slaa alizungumzia hekima na umakini mkubwa uliotumika kuzuia munkari wa vijana wengi baada ya uchaguzi ambao walikuwa wanataka kuingia mitaani kupinga kile ambacho waliamini kuwa kilikuwa ni uchakachuaji wa matokeo ya uchaguzi yaliyompatia ushindi hafifu Rais Kikwete kulinganisha na ushindi wake wa 2005. “Watu walikuwa wanasubiri kabisa wasikie nitasema nini, lakini sikuwa tayari kusukumiza watu katika kudai kwa nguvu haki yao. Sasa kama hatukufanya hivyo wakati ule hatuna sababu ya kutumia nguvu sasa hivi” alisema Dr. Slaa.

Akizungumzia kile ambacho serikali inaonekana kukihofisa sasa hivi hasa baada ya matukio ya Misri na Tunisia ambapo viongozi wa muda mrefu wa nchi hizo walijikuta wanaondolewa madarakani kwa nguvu za umma Dr. Slaa alisema kuwa wakati wowote wananchi wanaona kuwa haki zao zinapuuzwa wanaweza kujikuta wanalazimika kuzidai kwa nguvu.

“Kile kilichotokea Misri ndicho kilichotokea Arusha vile vile, na ndicho kilichotokea Geita na sehemu nyingine nchini mara baada ya uchaguzi mwaka jana na katika maeneo mbalimbali wananchi walikuwa tayari kwenda kudai haki zao na kama siyo hekima tuliyotumia kwa kweli hali ingekuwa mbaya kwani hata watu waliotaka tuitishe maandamano makubwa tuliwakatalia kwa sababu hatukuwa tayari kufanya hivyo wakati huo”.

Dr. Slaa alisema kuwa “ili kuepusha yanayotokea huko Misri, Bahrain, Yemeni na nchi nyingine za kiarabu ni lazima serikali na chama tawala kisikilize kilio cha wananchi na mara moja wakianza kutenda kufuatana na madai tunayoyatoa kwani hatutoi madai ya kibinafsi bali madai ambayo ni maslahi ya taifa. Sisi sote ni wadau katika maslahi ya taifa hili; tunataka kuona amani na utulivu lakini wakati huo huo hatuwezi kuwaacha watu wachache waendelee kuliharibu taifa letu”.

Pamoja na hayo Dr. Slaa amesema kuwa wamejaribu mara kadhaa kuanzisha mawasiliano na serikali ya Kikwete ili kusaidia kutoa ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayoendelea nchini. “Hata hivyo Rais Kikwete amemteua mtu ambaye ana kiburi kushika nafasi ya wizara inayoshughulikia masuala ya kisiasa. Bw. Wassira ambaye ameshika nafasi hiyo ni kikwazo kikubwa katika kutafuta utulivu wa kisiasa kwani hata alipoenda Arusha baada ya matukio ya Januari 5, alikutana na watu wengine wote, mashehe, maaskofu, CCM lakini watu pekee waliokuwa wanalalamika yaani Chadema hakukutana nao; sasa watu kama hawa tutaweza vipi kukaa nao chini wakati hata kwenye masuala haya mengine hawako tayari kukaa chini kuzungumza”?

Dr. Slaa na timu nzima ya viongozi wa Chadema wameendelea na maandamano na mikutano huko Shinyanga na baadaye wanaendelea na mikutano hiyo huko Kagera kabla ya kurudi Dar-es-Salaam kwa mapumziko mafupi siku chache zijazo.

6 Comments
  • Anacho fanya Dk Slaa nikitendo cha kipekee sana kweli chadema mungu awape nguvu na afya njema jamani watanzania kwanini sisi tu wakati tuna kila utajiri ?

  • e bwana tunasubiri, Iringa, mbeya, dar, arusha, singida,kilimanjaro safari tunataka kufika Tabora kule mzee mirambo. tumechoka na maisha haya, nguvu ya umma ndiyo silaha iliyobaki

  • Ukweli ni kwamba hali ya uchumi wa Tz ni mbaya sana. Simfahamu Kikwete ila nafikiri washauri wake ni bure!

    Anakosa strategic plans ambazo zitatoa nchi katika umasikini. Anafanya hata national security iwe hatarini! Inakuwaje mtu anaingia Tanzania na anadiwa kuwa mmiliki wa kampuni tapeli (Dowas) na anatamba ndani ya nchi kwa sababu ana hela?

  • Nimeisoma habari hii sijaona ubaya wowote sababu mambo yote yaliyozungumzwa na Dkt Wilbrod Slaa ni ya kimsingi na faida kwa wananchi wa Tanzania wenye umri wa uhuru wa miaka 50 lakini badala ya kusonga mbele ni kurudi nyuma Kama wapumbavu au wajinga.Mungu ibariki Tanzania

  • Wanaotamani nchi iingie katika machafuko kama Tunisia, Misri Libya nk, ni sawa na fisi wanaotamani mkono wa binadamu, Miongoni mwenu wamo mafisadi wa kitaasisi wanaomiliki shule, vyuo, na hospitali na pia waendesha madanguro. Mnatumia vibaya misamaha ya kodi na kukwepa kulipa kodi, Si mbaya harakisheni tamaa yenu ili tugawane mlivyotudhulumu na ndio itakuwa mwisho wa udhalimu wenu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *