SIMON Lwena anaonekana akikunjua nyavu zake zilizowekwa viraka na kuzipanga vizuri kwenye mtumbwi. Ni asubuhi na upepo katika Pwani ya Mbamba-Bay umetulia, hivyo wavuvi wengi, kama alivyo Lwena, wanaendelea na kazi hiyo wakijiandaa kwa safari ya usiku ya uvuvi ndani ya Ziwa Nyasa.
Wengi wanaonekana hawana zana bora za uvuvi, mavazi yao nayo yanaashiria ufukara mkubwa wanaouogelea japo wanaishi katika mwambao wa ziwa linalodaiwa kuwa na samaki wengi na adimu duniani wanaopatikana humo tu.
“Tusingekuwa na maisha magumu kama hivi ikiwa tungekuwa na zana bora za uvuvi,” anasema Lwena akiendelea kukunjua vizuri nyavu zake na kuzipanga tena. “Hali kama hii ni ya aibu sana kwa sisi tunaoishi kwenye mwambao wa ziwa hili, maisha ni magumu na tunaogelea kwenye ufukara.”
Lwena anasema, kama wangalikuwa na vifaa bora vya uvuvi katu kusingekuwa na uhaba wa samaki kwani ziwa hilo bado lina hazina kubwa.
Anasema uhaba wa samaki unaosababishwa na ukosefu wa zana bora ndio unaofanya bei ya kitoweo hicho ipande katika sehemu nyingi, zikiwemo za jirani na ziwa hilo.
“Tungekuwa na bodi nzuri ambazo zinaweza kufika kwenye kina cha meta 250 ambako ndiko waliko samaki wengi, pia tungekuwa na nyavu bora, hakika tungeweza kupata samaki wa kutosha na kubadilisha maisha yetu,” anasema Lwena.
Uhaba huo wa samaki umefanya bei ipande karibu maradufu ambapo samaki aina ya mbufu wanauzwa kwa kati ya Shs. 5,000 na 6,000 wakati dagaa wamekuwa wakiuzwa kwa Shs 22,000 kwa ndoo yenye ujazo wa lita 10.
Lwena anasema, samaki wa Ziwa Nyasa ni wazuri na wanapendwa na watu wengi, na kwamba kuna samaki wa aina nyingi, lakini anashangaa kuona serikali inashindwa kutumia ziwa hilo kama kivutio cha watalii na kufanya biashara kubwa ya samaki kama ilivyo katika Ziwa Victoria.
“Serikali itupatie mikopo nafuu ya ama fedha au zana za uvuvi i kupitia vikundi vyaetu vya uvuvi ambavyo vimesajiliwa kisheria ili tuweze kununua zana bora na hatimaye kuondokana na usumbufu tunaoupata sasa,” anasema.
Vifaa duni zinaelezwa kuwa kikwazo kikubwa kwa shughuli za uvuvi kwenye mwambao wa ziwa hilo, ambapo hali ya uchumi ya familia nyingi imezorota.
Bupe Kalikene, ambaye anajishughulisha na uchuuzi wa samaki na dagaa, anasema tatizo wanalokabiliana nalo ni ukosefu wa soko la uhakika.
Anasema wamekuwa wakiuza kwa mtindo wa kuwasafirisha kwa marafiki na jamaa zao walioko Mbinga na Songea na baada ya siku kadhaa hurejeshewa fedha mara baada ya mauzo kufanyika.
“Hakuna soko la uhakika, hakuna wafanyabiashara wanaokuja kununua hapa moja kwa moja, jitihada za kutafuta soko la bidhaa zetu tunalifanya sisi wenyewe, serikali ingeliangalia hili na kulipatia ufumbuzi yakinifu ili tuweze kuondokana na adha hii,” anasema.
Uvuvi ndiyo shughuli kuu ya uchumi kwa wakazi wa Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, wanaoishi kwenye mwambao wa ziwa hilo, licha ya baadhi yao kujishughulisha na kilimo za mihogo, mpunga, mbogamboga na matunda.
Hata hivyo, jitihada zao za uvuvi zinakwamishwa na zana duni wanazofanyia kazi, hali inayosababishwa na ukosefu wa elimu na mitaji hivyo kushindwa kumudu gharama za kununulia zana hizo, hasa boti za kisasa na nyavu nzuri.
Kutokana na changamoto inayowakabili, wavuvi wameunda umoja wao unaojulikana kwa jina la Samaki Business, ambao upo katika mji mdogo wa Mbamba Bay wilayani Nyasa na unatambulika baada ya kusajiliwa kisheria mwaka 2009.
Agrey Ngonyani, ambaye ni katibu wa umoja huo, anasema samaki aina ya Katoga, Kambale na dagaa Nyasa wanawavua kwa mtindo wa kutega nyavu ndani ya ziwa hilo ambapo hutumia nyavu zenye kuanzia nchi nne na kuendelea.
Anasema changamoto kubwa wanayokabiliana ni mikondo ya maji katika Ziwa Nyasa ambayo imekuwa ya kasi, hivyo kusababisha wavuvi kushindwa kuvua samaki ipasavyo kutokana na kuwa na vifaa duni kama vile mitumbwi ambayo haina uwezo wa kuhimili vishindo katika maji yenye kina kirefu, jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.
“Wengi wamepoteza maisha kwa sababu ya kutumia mitumbwi, kwa mwaka hujitokeza vifo vya wavuvi wasiopungua watatu hadi wanne kutokana na uduni wa vifaa vyetu hivi vya uvuvi,” anasema.
Ngonyani anasema wavuvi waliopo katika kikundi hicho ni zaidi ya 100 hivyo wanaiomba serikali iwasaidie vifaa vya kisasa vya uvuvi kama vile boti zenye kusukumwa kwa injini maalum, na siyo kutumia mitumbwi kama wanavyofanya sasa ambapo huwafanya washindwe kutimiza mahitaji yao ya kuvua samaki wengi.
Anabainisha kuwa kwa siku wamekuwa wakivua samaki tani 4 au zaidi na kuwahifadhi kwa mfumo bora unaokubalika kitaalamu, tayari kwa kusafirishwa kwenda kuuzwa.
Changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni kukosa meza za kuanikia ambapo kwa sasa hutumia matete kutengenezea meza kwa ajili ya kuanikia samaki, tekinolojia ambayo imepitwa na wakati.
“Tunaishukuru Halmashauri yetu kutufikishia elimu sahihi ya uvuvi, hivyo wavuvi wengi wanavua kwa kufuata taratibu husika,” anasema Ngonyani.
Anaongeza kuwa suala la mikopo kwao limekuwa shida hivyo wanaziomba taasisi mbalimbali za kifedha kama vile benki kuwakopesha ili waweze kuendesha umoja wao na kuinua kipato.
Ofisa Uvuvi Wilaya ya Nyasa aliyejitambulisha kwa jina la Mwasaga anasema serikali inafanya utaratibu wa kuboresha mazingira ya wavuvi hao kwa kuleta wataalamu ambao watatengeneza boti ambazo zitafungwa injini kwa ajili ya kuwarahisishia wavuvi kufanya shughuli zao kwa ufasaha zaidi.
Kuhusu suala la mikopo, Mwasaga anasema wavuvi hao wanapaswa kufanya jitihada zao binafsi za kuomba mikopo kupitia taasisi za kifedha ili waweze kuboresha shughuli zao na siyo kuitegemea serikali peke yake.