Maji yageuka anasa kwa wakazi Songea

Simon Mkina

KWA Raphael Millanzi, mkazi wa Manispaa ya Songea, maji yamekuwa anasa kutokana na kutopatikana kwa uhakika katika maeneo anayoishi na yale ya jirani.

Millanzi anasema, kitendo cha kufuata maji umbali wa takriban kilometa 15 ndani ya manispaa hiyo hakitoi tasiwra chanya ya yeye kuishi mjini, huku ndoo moja ya maji yenye ujazo wa lita 20 ikiuzwa kwa Shs. 500 kwa wale wasukuma mikokoteni na wenye baiskeli.

“Afadhali hata wanaoishi vijijini ambao wanategemea maji ya visima, lakini hapa mjini hali ni mbaya sana, huduma ya maji inapatikana kwa wachache tu,” analalamika.

Millanzi, ambaye ni mmoja kati ya asilimia 24 ya wananchi wa Manispaa ya Songea ambao hawapati huduma ya maji, anasema serikali isipochukua hatua za haraka kunusuru hali hiyo, huenda tatizo likazidi kuwa kero kubwa na hata kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Taarifa zilizopo zinaeleza kwamba, wakazi wa Manispaa ya Songea wenye uhakika wa kupata maji ni asilimia 76 tu, huku robo nyingine wakihangaika kutafuta huduma hiyo, ambayo licha ya kupatikana kwa shida, lakini maji siyo safi na salama.

“Kama huna muda inabidi ununue kwa wenye mikokoteni ndoo moja Shs. 500, lakini hujui kama maji hayo ni safi wala salama, hapo kweli hatuwezi kupata magonjwa ya milipuko?” anahoji Millanzi.

Millanzi anasema, msimu pekee ambao ni nafuu yao ni wa masika ambapo walau wanaweza kukinga maji ya mvua kwa huduma mbalimbali, vinginevyo kipindi cha kiangazi hali ni mbaya zaidi.

Inaelezwa kwamba, mahitaji halisi ya maji kwa mji huo kwa sasa ni zaidi ya meta za ujazo 12,868 kwa siku, hali ambayo inahitaji jitihada za makusudi zifanyike ili kuweza kunusuru hali hiyo.

Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kwamba, upatikanaji wa maji safi na salama ni tatizo ambalo limekuwa likiitesa jamii katika maeneo mengi nchini na kusababisha maendeleo kurudi nyuma.

Hata hivyo, uharibifu wa vyanzo vya maji katika Milima ya Matogoro ni sababu kubwa inayolikuza tatizo la ukosefu wa maji katika Manispaa ya Songea, licha ya juhudi zinazofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Songea (SOUWASA) za kuvilinda vyanzo hivyo.

Vyanzo hivyo, ambavyo vinazalisha meta za ujazo 1,200 wa maji, vimeharibiwa na wananchi kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi, hali ambayo inavifanya wakati wa kiangazi vizalishe meta za ujazo 640 tu kwa siku, kiasi ambacho hakitoshelezi mahitaji hata kwa wakazi walio kwenye mtandao wa maji.

Vyanzo vingi vimeanza kupoteza maji na vingine kukauka kutokana na baadhi ya wananchi kuendesha shughuli za kilimo, kuchungia mifugo na ukataji wa miti ovyo.

Salum Abdallah, mkazi wa Matogoro Kati, anaeleza kuwa uchomaji moto wa misitu hiyo ambayo huzunguka milima ya Matogoro, unasababishwa kwa kiasi kikubwa na watu wanaoendesha shughuli za uchomaji wa mkaa.

“Shughuli zisizo rasmi katika vyanzo sita vya chemchem vilivyopo katika milima ya Matogoro ambavyo ndio tegemeo la uzalishaji wa maji ambayo husafirishwa kwa njia ya mtiririko (Gravity) hadi kwenye mtambo mkuu wa kutibu na kuchuja maji uliopo katika eneo hilo la Matogoro zimeharibu upatikanaji wa maji,” anasema Abdallah.

Abdallah anaongeza kuwa, uchomaji wa moto misitu katika milima hiyo ambako ndio kuna vyanzo hivyo, limekuwa suala la kawaida jambo ambalo linasababisha tatizo hilo kuendelea kuwa sugu.

“Sheria za kulinda vyanzo hivi zipo, lakini uongozi wa eneo hili umekuwa hauwajibiki ipasavyo, watu wamekuwa na kiburi kiasi ambacho huingia katika misitu na kufanya shughuli za kibinadamu,” anasema Abadallah.

Anasema kinachotakiwa ni kuwepo kwa udhibiti mkali na kwamba uongozi wa Kata ya Matogoro kwa kushirikiana na SOUWASA lazima wahakikishe wanawajibika ipasavyo kulinda vyanzo hivyo ikiwemo suala la upandaji wa miti ambalo linapaswa kupewa kipaumbele.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Matogoro, Peter Mapunda, anakiri akisema utunzaji wa mazingira katika Milima ya Matogoro umekuwa tatizo sugu na kuongeza kwamba, miti iliyo rafiki wa maji ndiyo huteketezwa kwa kukatwa na wananchi mara kwa mara.

“Upandaji wa miti kwa maeneo yaliyoharibiwa umekuwa ukifanywa kwa asilimia chache, lakini bado tunaendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti, tukiwa makini kusimamia tatizo hili ikiwemo hili la upandaji miti, nina uhakika tunaweza kurejesha uoto wa asili wa Milima ya Matogoro,” anasema.

Mapunda anaeleza kuwa, licha ya kutunga sheria za kuwabana wananchi wasiharibu vyanzo hivyo na kutoa elimu ya kutofanya shughuli za kibinadamu, bado limekuwa tatizo na watu wamekuwa wakiendelea kufanya uharibifu.

“Maji ni kitu muhimu ambacho kiumbe chochote kilicho hai hapa duniani, hutegemea kuendesha maisha yake ya kila siku kwa kutumia nishati hiyo muhimu na ndio maana wananchi husisitizwa kutunza vyanzo vya maji ili visiweze kupotea,” anabainisha.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa SOUWASA, Mhandisi wa Mipango na Ujenzi, Jaffary Yahaya, anathibitisha kuwepo kwa tatizo hilo la uhaba wa maji katika manispaa hiyo, huku akisema hali hiyo inasababishwa na uharibifu huo wa vyanzo jambo ambalo linachangia kuwepo kwa mgawo mkali wa maji kwa watumiaji.

 Pamoja na mambo mengine, Yahaya anasisitiza kuwa ufumbuzi wa tatizo hilo ni kujenga kitega maji kitakachoweza kuyatunza ili kupata maji ya kusukuma kwenda katika mitambo ya kusafisha maji iliyopo Matogoro na hivyo kuongeza uzalishaji kufikia meta za ujazo 12,000 ambazo zinahitajika kwa siku kwa ajili ya kulisha wakazi wa manispaa hiyo walio katika mtandao.

Mhandisi Yahaya anasema kuwepo kwa ukosefu wa maji wakati wa kiangazi katika Manispaa ya Songea kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na aina ya miti ambayo ipo katika misitu ya Milima ya Matogoro ambayo hunyonya maji kwa kiwango kikubwa kwa kipindi cha mwaka.

“Miti hii inatakiwa ivunwe yote kama kweli tunataka vyanzo vya maji viendelee kudumu kwenye milima hii, vinginevyo kuna hatari ya maji kukauka na hivyo mito mikuu, ukiwemo Ruvuma unaoanzia kwenye milima hii, kutoweka,” anasema Yahaya.

Msitu wa Milima ya Matogoro wenye ukubwa wa kilometa za mraba 48 ulipitishwa na Serikali ya Tanganyika mwaka 1951 chini ya Notisi ya Serikali Na. 260 kuwa kama shamba la mbao na kati ya mwaka 1967 – 1979 serikali ikapanda miti ya kigeni katika eneo la hekta 867 ambazo awali zilikuwa zikikaliwa na wananchi kabla ya kuhamishwa.

Lakini mwaka 2000 Serikali ikautangaza msitu huo kama wa Hifadhi ya Vyanzo vya Maji, ambapo SOUWASA ina jumla ya vyanzo tisa vinavyotumika kukusanya maji yanayotumiwa na Manispaa ya Songea huku pia ukiwa vyanzo vya mito mitatu.

Mito hiyo muhimu ni Ruvuma, Mto Luhira ambao unamwaga maji yake kwenye Mto Ruhuhu (mto mkuu unaomwaga maji Ziwa Nyasa), na Mto Luwegu ambao unamwaga maji yake kwenye Mto Rufiji katika makutano yake mkoani Morogoro.

 

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *