WAZIRI Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, amekutana na waandishi wa habari na kusema anashangazwa na kauli kwamba Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, analo jina la mgombea Urais kupitia chama hicho 2015, maana itakua chama kimegeuka cha Kisultani.
Sumaye aliwataja kwa majina Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi na kumtaja kwa cheo, Kaimu Katibu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM bila kumtaja jina. Anayeshikilia nafasi hiyo ni Tambwe Hiza.
“Chama cha Mapinduzi ni chama cha kidemokrasia na kina katiba, kanuni na taratibu zake kufanya mambo yake. Nimeshtushwa sana na kauli ya Baraza Kuu la UVCCM mkoa wa Pwani kuwa ‘suala la rais ajaye liko mikononi mwa Mwenyekiti Rais Jakaya Kikwete, ndiye anayemjua Rais wa mwaka 2015.
“Hili ni la hatari sana na nilitarajia Baraza Kuu la UVCCM lingerekebisha kasoro hiyo au hata Katibu Mkuu wa chama. Mimi siamini kama Rais Kikwete anamjua rais ajaye labda kama chama chetu kimebadilika kuwa cha Kisultani. CCM ninayoijua mimi ni chama cha kidemokrasia na Rais Kikwete asisingiziwe mambo ambayo najua hawezi kuyafanya. Naamini hili litarekebishwa na kukemewa katika vikao vijavyo vya chama,” anasema.
Akijibu mashambulizi dhidi yake yaliyotolewa na wana CCM wenzake, wakiwamo viongozi waandamizi na wale wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Sumaye amekana kuwa na mpango wa kukihama chama chake na badala yake atakiimarisha.
Alianza kwa kurejea kauli zilizotolewa akianzia na ile ya UVCCM mkoani Pwani na hapo alisema kauli iliyotolewa kwamba kauli aliyoitoa inalenga kuutaka urais na kwamba wameshiba na kuvimbiwa ilikuwa ni matusi, kejeli lakini pia ni ya kutisha.
“Ukiachia mbali matusi na kejeli iliyopo ndani ya lugha, maudhui yake yanatisha hasa ukiunganisha na ile kauli ya awali kwamba Rais ajaye anafahamika tayari. Maana yake ni kuwa hao vijana wanaye mgombea wao ambaye wanampigania ili na wao sasa iwe zamu yao ya kula.
“Kwa hiyo unaweza kusema madongo yote tunayopigwa sisi wengine ni kwa sababu inaonekana tunaweza kuwa kikwazo kwa anayesafishiwa njia. Vijana kama wanapigania watu ili na wao wale basi hata amani na usalama na mshikamano wan chi yetu uko hatarini sana kwa sababu itakuwa ni kudra ya Mwenyezi Mungu kumpata kiongozi bora kwa sababu tutakuwa tunampima anayetaka kuongoza si kwa uwezo wake wa uongozi bali kwa uwezo wake wa kutushibisha matumbo yetu,” anasema.
Sumaye amesema si lazima kwa kila jambo lipelekwe kwenye vikao na kwamba hata waliomshutumu baadhi hawakutumia vikao na badala yake walitumia vyombo vya habari.
“Nilishutumiwa na Kaimu Katibu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM kuwa mimi ni mchochezi, ninakivuruga chama na kumbebesha gunia la misumari mwenyekiti wa chama kwa kuongea barabarani badala ya vikao. Nililijibu nikadhani yameisha kumbe ndio yakaanza,” anasema Sumaye, ambaye ameapa kutohama CCM na kwamba hajaamua kuwania ama kutowania Urais 2015.
Alisema alichoshauri ni CCM kumsaidia Rais kama chama kwa kufanya siasa kujibu mapigo ya wenzao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao wamekuwa wakifanya maandamano nchi nzima na kupata washabiki.
Katika hitimisho lake, Sumaye amesema;
“Demokrasia maana yeke ni chetu kwa ajili yetu. Penda tusipende chochote ambacho watu wamekiweka wao kwa ajili yao na ni chao, lazima watakisema au kukisemea, serikali kama ni ya kidemokrasia wataisema na/au kuisemea, na Rais kama wamemchagua wao kidemokrasia, watamsema na/kumsemea.
Kila Rais aliyepita alisemwa na kusemewa, aliyeko anasemwa na kusemewa na atakayekuja atasemwa na kusemewa. Mfumo au taasisi ambayo haisemwi wala kusemewa ni ya kiimla. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema waacheni waseme, Mungu amewapa midomo ya kusema wewe utawazuiaje?
“Nawaomba Watanzania, yeyote atakayejaribu kutumia njia za udanganyifu kwa rushwa, kutenganisha watu, tumkatae kwa nguvu zote. Tunakosa muda wa kujielekeza katika mambo ya msingi tunaanza siasa za kupakana matope.”