Madiwani: Tunahitaji katiba mpya kuboresha elimu

Jamii Africa

BAADA ya uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwaka jana, mabaraza mengi ya madiwani yameibua sura mpya zenye kila dalili ya kiu ya mabadiliko FikraPevu imebaini.

Madiwani hawa ni ambao imani yao inakwenda hadi nje ya misimamo ya vyama vyao kwa ajili ya masilahi ya wananchi, wale wanaovaa ujasiri wa kuikosoa serikali hadharani.

Baraza la madiwani wa wilaya ya Muleba mkoani Kagera ni mchanganyiko wa wakongwe na damu mpya. Kundi la pili linaonekana kutumia ushawishi wa hoja za mabadiliko na kuponda staili ya baraza dhaifu linalofanya kazi kwa mazoea ya kusubiri maelekezo ya  wataalamu wa halmashauri.

Kudorora kwa elimu wilayani humo ni moja ya mambo yaliyomshawishi diwani mpya wa kata ya Kamachumu Danstan Mutagaywa (CCM) kuomba kiitishwe kikao cha dharura ili kuweka mikakati ya kuondokana na aibu iliyopo.

Diwani huyu mdogo kuliko wote na mwanasheria kitaaluma  mara zote ameibua malumbano ya hoja kwenye vikao na kuibuka mshindi huku akitaka watendaji kuwajibishwa.

Pendekezo lake la kikao cha dharura liliungwa mkono na katika mkutano wao wa 28,March walipendekeza kujivua gamba la aibu ya kudorola kwa elimu kwa kutenga milioni 168 kwa ajili ya kazi hiyo.

Kabla ya kufikia makubalino wakiwepo wataalam wa wilaya  walijiridhisha kuwa kiasi hicho kilitosha kugharimia mapungufu mbalimbali yaliyopo ikiwa ni pamoja na kuwalipa walimu wa kujitolea kutokana na upungufu mkubwa wa walimu.

Madiwani  waliamini kama yanatumika mamilioni ya shilingi kwa ajili ya miradi ambayo tija yake haiko wazi katika kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi,basi kiasi hicho kilikuwa mwanzo mzuri wa kurudisha heshima ya elimu wilayani humo.

Hata hivyo madiwani hao baada ya wiki chache walipokea habari mbaya juu ya mpango wao kuwa hauwezi kutekelezeka mpaka serikali kuu ijiridhishe ambayo kwa kawaida hutoa maelekezo kwa wilaya zote na sio sehemu moja ya nchi.

Kwa mujibu wa Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Pastory Kajuna aliwaambia kuwa wazo lao lilikuwa la msingi ila utekelezaji wake lazima usubiri uamuzi wa viongozi wa kitaifa ambao huchukua miaka kadhaa kukubaliwa.

Mbele ya madiwani alidai hii ndiyo sababu ya ombi la kutaka kuboresha masirahi ya wafanyakazi walioko katika mazingira magumu ya visiwani halikufaulu.Viongozi wa juu kwa miaka kadhaa sasa wamekalia ombi lao bila kutoa majibu kwa madai kuwa utaratibu huo hauwezi kuruhusiwa katika eneo moja tu.

Hii ina maana kuwa wafanyakazi hawa wanaendelea kuteseka kutokana na uamuzi wa viongozi walioko Dar es salaamu ambao wanasubiri maombi kama hayo kutoka wilaya nyingine hata kama hazina ulazima wa kufanya hivyo.

Kiongozi huyo ambaye ni ofisa elimu wa wilaya anathibitisha ugumu wa mazingira  ya visiwani kwa wafanyakazi kwani hata yeye alidai amewahi kuzungukia visiwa vya wilaya hiyo mara moja kwa boti ya kukodi kwa miaka minne iliyopita.

Diwani wa Kata ya Kamachumu Danstani Mutagaywa anaamini mpango huo umekwamishwa na mfumo mbovu ambao  unatoa madaraka makubwa kwa viongozi walioko ngazi za juu kutoa uamuzi kwa wananchi ambao hawako karibu nao.

Kukwama kwa mpango wa hoja yake kunamfanya agusie umuhimu wa nchi kuwa na katiba mpya kuwa itatoa nafasi kubwa kwa serikali za mitaa kujadili,kuamua na kutekeleza mambo muhimu yanayolenga kuwakwamua wananchi bila kusubiri utashi wa viongozi wa kitaifa.

Anadai mfumo mbovu wa ugawanyaji wa madaraka umetufikisha hapa tulipo na kuwa haiingii akilini madiwani kulazimika kupata kwanza kibali cha serikali ili kutatua kero za elimu ambazo athari zake huwarudia wananchi masikini.

uji shuleni utoro
Pichani: Unywaji wa uji unachangia mahudhurio mazuri shuleni; kama wanavyoonekana wanafunzi wa shule ya msingi Nshamba wilayani Muleba ambapo hata hivyo ni wachache wanaoupata kutokana na kulazimika kuchangia gharama zake.Naye msemaji wa kambi ya upinzani kwenye baraza hilo Julius Lwakyendera anasema hatua hiyo inazima matumaini ya kuinusuru wilaya hiyo na matokeo mabaya katika mitihani ya kitaifa na kuwa fedha hizo sio nyingi ikilinganishwa na matokeo yanayotegemewa.

Alisema madiwani kama wawakilishi wa karibu wa wananchi wanafahamu hali ya kielimu ilivyo taabani  katika maeneo.Kwamba yasitegemewe maajabu kama hoja za kuwakwamua wananchi kama ilivyokuwa ile ya elimu zitaendelea kuwekewa vikwazo.

Kukataliwa kwa mpango wa madiwani kunaongeza hofu ya kuzidi kuporomoka kielimu. Kwa mujibu wa program ya Uwezo katika ripoti yake, Muleba iliongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wasiojua kusoma na kuandika kati ya wilaya 38 zilizofanyiwa utafiti Mei mwaka 2010.

Pamoja na mkuu wa wilaya hiyo Angelina Mabula kudai kuwa hakuwahi kuipata taarifa hiyo, alikiri kuwa katika tahimini ya darasa la saba iliyofanyika mwaka 2009,ilibainika baadhi ya wanafunzi waliomaliza darasa la saba hawawezi kufanya mtihani wa darasa la tatu.

Kwamba inachangiwa na mazingira duni hasa maeneo ya visiwani na utoro huku akibainisha changamoto kubwa ya uhaba wa nyumba za walimu ambao pia ni wachache ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanafunzi.

Kwa mujibu wa Mabula kiwango cha ufaulu kwa shule za msingi kimeshuka kutoka asilimilia 70 mwaka 2008,asilimia 57.2(2009)na asilimia 56.4 mwaka jana,takwimu  zinazothibitisha umuhimu wa hoja ya madiwani.

Katika ziara yake mkoani Kagera mwezi March,Waziri mkuu Mizengo Pinda aliwataka madiwani kutafuta ufumbuzi na suruhisho la matatizo ya wananchi.Bila shaka madiwani wa wilaya ya Muleba waliitikia wito wake kwa kuanza na kujivua gamba la udhaifu wa elimu.

Pia  alisisitiza umuhimu wa taifa kuwekeza katika elimu, kama hivi ndivyo basi hoja ya madiwani hawa haipashwi kupuuzwa kwani itafungua milango kwa maelfu ya wanafunzi wanaotaka kufikia ndoto za mafanikio kielimu.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *